Rais Mstaafu Jakaya Kikwete akimpongeza Rais John Magufuli baada ya kuapishwa kuwa rais. |
Vyama tawala katika Bara la Afrika vimeonywa kuacha kasumba ya
kuvichukulia vyama vya upinzani kuwa maadui na badala yake viwaone kama
washindani.
Rais
mstaafu Jakaya Kikwete wa Tanzania ambaye tangu astaafu baadhi ya wapinzani
wamekuwa wakimkumbuka na hata kufuta kumbukumbu za mashtaka ya kufinya
demokrasia, kutokana na kile wanachodai kubanwa zaidi na uongozi wa sasa.
Kikwete
aliyasema hayo wakati akichangia mada ya Utawala Bora na Utawala wa Sheria
iliyowasilishwa na Profesa Barney Pityana, ambaye ni Makamu Mkuu Mstaafu wa
Chuo Kikuu cha Afrika Kusini kwenye Kongamano la Uongozi barani Afrika yaani
‘African Leadership Forum 2017’.
Kikwete
aliliambia kongamano hilo la siku mbili lililomalizika Ijumaa Johannesburg
nchini Afrika Kusini na kukutanisha viongozi mbalimbali akiwamo mtangulizi
wake, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, kuwa vyama tawala viache
kasumba ya kuwa upinzani ni maadui kwani huleta chuki na uadui usiokuwa na
faida.
Katika
hilo, Kikwete alivitaka vyama vya upinzani barani Afrika kutokurudi nyuma
katika kunadi sera zao kwa wananchi.
Vyanzo
vya habari nchini Afrika Kusini vimesema aliongeza kuwa vyama vya upinzani
vinapaswa kuelezea vyema sera zao kwa wafuasi wao ili wazielewe na ufikapo
wakati wa uchaguzi wapiga kura wawe na uelewa wa kutosha kuhusu mipango yao ya
kuongoza nchi.
Akielezea
umuhimu wa vyama vya upinzani katika Taifa lolote lile, Kikwete alisema ni
kuvifanya vyama tawala kuwa macho si kulala.
“Pia
kazi ya upinzani ni kuiambia Serikali kile inachofanya ni kibaya, ambacho
katika chama chako hawawezi kuona au wanaweza kuona lakini wasiwe na ujasiri wa
kusema kipi sahihi.
Pamoja
na hayo, Kikwete alipongeza baadhi ya nchi ambazo zimekuwa mstari wa mbele
kuhakikisha kuwa zinatilia maanani misingi ya utawala bora.
“Si
kweli kuwa barani Afrika hakuna utawala wa sheria au kila kitu Afrika ni kibaya
hapana. Kumekuwa na juhudi nyingi za kuhakikisha kuwa migogoro inayozikumba
baadhi ya nchi inatatuliwa ili kuwe na amani na utulivu katika nchi hizo,”
alisema Kikwete.
Kauli
hizo za Kikwete zilionekana kumvutia mwanasiasa na kiongozi wa upinzani wa
chama cha Democratic Alliance (DA) cha Afrika Kusini, Mmusi Maimane.
Maimane
aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa: “Rais
Kikwete ameibua hoja ya umuhimu wa upinzani Afrika kama kazi ya utawala bora.
Si maadui lakini washindani.”
Hoja
hiyo ya Maimane ilimwibua mmoja wa wanasiasa wa upinzani hapa nchini, ambaye
pia na mwanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) ambacho kipo kwenye mgogoro
mkubwa wa kiuongozi, Ismail Jussa.
Jussa
kupitia ukarasa wake wa Twitter aliandika kuwa: “Ni uongo wa hali ya juu,
maneno matupu. Ni Kikwete ambaye alituma jeshi kwenda Zanzibar, Oktoba 2015 na
kufuta uchaguzi kwa sababu CUF ilikuwa inashinda.”
Akizungumza
na wanahabari jana jijini Johannesburg, Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, alivitaka
vyombo vya habari barani Afrika kuwa wazalendo kwa kuandika habari
zitakazosaidia kutatua migogoro na kuleta maendeleo.
Mkutano
huo wa siku mbili ulihudhuriwa pia na marais wastaafu Olusegun Obasanjo (Nigeria),
Thabo Mbeki (Afrika Kusini), Mohamed Marzouki (Tunisia), Hassan Mohammed
(Somalia), Bakili Mulizi (Malawi), Mwanasheria Mkuu wa Uganda, Bart Katureebe.
Ulimalizika
jana kwa kuwataka viongozi barani Afrika kuunganisha nguvu zao katika kujenga
amani na utulivu barani humo.
No comments:
Post a Comment