Showing posts with label habari za kitaifa. Show all posts
Showing posts with label habari za kitaifa. Show all posts

Monday, 14 May 2018

Lulu atarudi tena gerezani – Mkuu wa Magereza

Mkuu wa Magereza ya Mkoa wa Dar es salaam, ACP Augustino Mboje amesema muigizaji wa filamu nchini Elizabeth Michael maarufu kama Lulu anaweza kurudi gerezani endapo ataonesha mwenendo usioridhisha wakati ambao atakua chini uangalizi

ACP Mboje amesema hayo leo Mei 14, 2018 alipokuwa anaongea na vyombo vya habari kuelezea sababu za msanii huyo kutoka kabla ya muda kifungo kuisha ambapo amedai kuwa Lulu amenufaika na msamaha wa Rais Magufuli aliotangaza katika sherehe za sikukuu ya Muungano Aprili 26, 2018 mjini Dodoma
“Kama atakiuka masharti ya kuchelewa, kuonesha tabia mbaya, mara siku moja moja haji, akawa haoneshi mwenendo mzuri, community worker atawasiliana na sisi (Lulu) atarudi gerezani kwa kupitia mahakamni kwasababu aliletwa na mahakama” amesema ACP Mboje
Awali ACP Mbonje aliongeza kuwa msanii huyo asingeweza kutoka 26 April 2018 hata baada ya kupewa msamaha na Rais Magufuli kwasababu alikua hajatumikia robo ya kifungo chake ambacho kilikua kinaisha Novenba 12, 2018 baada ya msamaha huo.
Sambamba na hilo ACP Mbonje amedai kwasasa msanii Lulu bado ni mfungwa ila atatumikia kifungo chake nje ya gereza mpaka novemba 12, 2018 kwa kufanya huduma za kijamii.
Kwa mujibu wa sheria ya Mahakama kifungu na. 3 (2) (a) ya huduma ya jamii ya mwaka 2002 inatoa nafasi kwa mfungwa ambae kifungo chake hakijazidi miaka mitatu kutumikia kifungo chake nje ya gereza kwa kufanya kazi zisizo na malipo kwa manufaa ya jamii.
Novemba 13, 2017 Mahakama Kuu kanda ya Dar es salaam ilimtia hatiani msanii Elizabeth Michael (Lulu) na kumhukumu kifungo cha miaka miwili jela kwa kosa la kumuua bila kukusudia msanii mwenzake Steven Kanumba April 7, 2012 nyumbani kwa marehemu Sinza Jijini Dar es Salaam

MVUA KUBWA KWA SIKU TANO YAJA-TMA


Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) imetoa tahadhari ya kunyesha mvua kubwa kwa siku tano kuanzia jana, ambazo zinaweza kuleta mafuriko katika maeneo ya mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara na Visiwa vya Unguja na Pemba.

Katika taarifa ya TMA iliyotolewa Mei 13, mvua hizo zilizoanza kunyesha  zitaendelea mpaka Mei 17 mwaka huu.

TMA imesema athari zinazinaweza kutokea ikiwemo mafuriko ambayo yanaweza kusababisha kuvurugika kwa usafiri, barabara kubwa kutopitika na maisha ya watu kuwa hatarini  kutokana na maji kujaa au kupita kwa kasi.

Aidha imetoa wito kwa wakazi wa maeneo hayo kuchukua tahadhari stahiki na kuendelea kufuatilia taarifa pamoja na tahadhari zitakazotolewa.


Thursday, 3 May 2018

MATUKIO YA KIKATILI DHIDI YA WANAHABARI YATAJWA KURUDISHA NYUMA TAALUMA HIYO


Matukio ya utekaji wanahabari, kuibuka kundi la watu wasiojulikana, kufungiwa vyombo vya habari na kupigwa faini kwa vyombo hivyo vimetajwa kudunisha  uhuru wa habari nchini.
Mwenyekiti wa Vyombo vya habari kusini mwa  Afrika, tawi la Tanzania, (Misa- Tan) Salome Kitomari 
Wakisoma hotuba zao leo Mei 3  katika  maadhimisho ya Siku  ya Uhuru wa Vyombo vya habari,  Mwenyekiti wa Vyombo vya habari kusini mwa  Afrika, tawi la Tanzania, (Misa- Tan) Salome Kitomari amesema ni muhimu hatua zichukuliwe kukabiliana na hali iliyopo sasa.
Kitomari amesema, takwimu za  taasisi kama waandishi wasio na mipaka na kamati ya kulinda  waandishi wa habari zinaonesha kushuka  viwango vya uhuru wa habari na kujieleza Tanzania.
Amesema mwaka jana zimeripotiwa kesi za kupotea kwa waandishi wa habari, manyanyaso na ukiukwaji wa uhuru wa vyombo vya habari.
Amesema wahabari wanaitaka Serikali kupitia jeshi la polisi kuwatafuta waliohusika na kitendo hicho na kuwachukulia hatua za kisheria.
Kaimu Mwenyekiti wa  Jukwaa la Wahariri, (TEF) Deodatus  Balile amesema mazingira ya kazi ya kuandika habari yamekuwa magumu kutokana na  baadhi ya watendaji wa vyombo vya dola kubugudhi na kuwafanyia uonevu wanahabari, huku kukiibuka kundi la watu wasiojulikana.

Sheria sasa inatambua Uandishi wa Habari kama Taaluma-Mwakyembe

Waziri wa Habari, Utamaduni na michezo, Dk Harrison Mwakyembe amesema Serikali imefungua milango ya majadiliano na wanahabari kuhusu changamoto zao.

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari, leo Mei 3, Waziri Mwakyembe amesema Serikali imetoa haki ya kupelekwa mahakamani mashauri mbalimbali kuhusiana na sheria ambazo zimepitishwa lakini bado kuna fursa nzuri ya kufanya mazungumzo miongoni mwa wadau.
 “Serikali itaendelea kusimamia sheria zilizotungwa katika kuhakikisha wanahabari na wamiliki wa mitandao ya kijamii wanafanyakazi kwa weledi na kujali maslahi ya taifa na tamaduni,” amesema.
Amesema Serikali itahakikisha inasimamia kuundwa kwa vyombo vitatu katika kutekeleza sheria ya huduma za habari, ambavyo ni baraza huru la habari, Bodi ya Ithibati na kuwepo kwa mfuko wa kusaidia wanahabari.
"Sheria sasa inatambua uandishi wa habari kama taaluma hivyo lazima masilahi ya wanahabari kutazamwa ikiwepo kulipiwa bima na kuingizwa katika mifuko ya hifadhi ya jamii,"amesema.
Amesema ni muhimu waajiri kutoa masilahi bora kwa wafanyakazi kwani badala ya kuendelea kuwa na idadi kubwa ya wafanyakazi ambao hawalipwi vizuri ni bora kuwa na wachache ambao wanalipwa vizuri.
Hata hivyo, amesema suala la matangazo kwa vyombo vya habari linafanyiwa kazi lakini pia serikali haitarudi nyuma katika utekezaji wa usajili na ulipaji wa kodi mbalimbali kwa mitandao ya kijamii.




Tuesday, 1 May 2018

NITAONGEZA MISHAHARA KABLA YA KUSTAAFU-RAIS MAGUFULI


Rais John Magufuli ameahidi kuwaongezea wafanyakazi mishahara kabla hajamaliza kipindi chake cha urais.

Rais Magufuli amesema hayo leo Mei Mosi katika Sikukuu ya Wafanyakazi iliyoadhimishwa kitaifa, Iringa.
Akizungumza katika Uwanja wa Samora zilimofanyika sherehe hizo, Rais Magufuli amesema kutokana na changamoto za kimaendeleo  zinazotakiwa kutatuliwa kwa sasa lakini Serikali itahakikisha inampa mfanyakazi maisha mazuri na nafuu kwa kudhibiti mfumuko wa bei ya bidhaa nchini.
"Natamani mwaka huu kupandisha mishahara kwa wafanyakazi lakini kutokana na changamoto zilizopo za kuajiri wafanyakazi 52,000 nitawalipa nini? nikisema natamka kuongeza mishahara, nitazipata wapi?”amesema Magufuli.
Rais Magufuli amesema iwapo wanataka waongezewe mishahara labda vyama vya wafanyakazi viuze miradi yao ili wajiongezee mishahara.

Maadhimisho Ya Sherehe Za Mei Mosi

                       Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani DRr,John Magufuli 


Mpanda Radio Fm tunakutakia maadhimisho mema ya siku ya Wafanyakaz Duniani 

Kitaifa maadhimisho hayo yanafanyika Mkoani Iringa na Mgeni Rasmi ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani DRr,John Magufuli 

Monday, 19 February 2018

Waziri wa Elimu, Profesa. Joyce Ndalichako amesema kuwa serikali itagharamia shughuli za mazishi ya Mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwiilina Akwiline ambaye ameuawa kwa kupigwa risasi Februari 16, 2018 eneo la Mkwajuni DSM.

Waziri wa Elimu, Profesa. Joyce Ndalichako 


DAR ES SALAAM
Waziri wa Elimu, Profesa. Joyce Ndalichako amesema kuwa  serikali itagharamia shughuli za mazishi ya Mwanafunzi  wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwiilina Akwiline ambaye ameuawa kwa kupigwa risasi Februari 16, 2018 eneo la Mkwajuni DSM.
Waziri Ndalichako amesema kuwa viongozi mbalimbali wameguswa na kifo hicho kwani mwanafunzi huyo hakuwa na hatia yoyote na kusema kifo chake ni pigo kubwa kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 
Ndalichako amedai kuwa kifo cha mwanafunzi huyo kimetokea wakati akiwa kwenye harakati ya kupeleka barua ya maombi ya mafunzo kwa vitendo ambayo alikuwa akitegemewa kuanza Februari 26, 2018 na kudai kifo hicho kimezima ndoto yake.
 Aidha  Kwa mujibu wa kamanda wa Kanda maalamu ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa  amesema maafisa sita wa polisi wamekamatwa kuhusiana na kifo cha mwanafunzi huyo.

Chanzo:Mwananchi

Sunday, 18 February 2018

Polisi sita washikiliwa kwa uchunguzi kifo cha mwanafunzi NIT


Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa


Dar es Salaam. 
Polisi inawashikilia askari wake sita na silaha zao kwa ajili ya uchunguzi kuhusu tukio la kuuawa kwa risasi mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akweline.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema hayo leo Februari 18,2018 alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu ulinzi wakati wa kampeni, upigaji kura, na utangazaji matokeo ya uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Kinondoni uliofanyika jana Februari 17,2018.
Amesema polisi iliunda timu ya upelelezi kuchunguza chanzo cha kifo cha mwanafunzi huyo kilichotokea Februari 16,2018 wakati polisi wakiwatawanya wanachama wa Chadema waliokuwa wanakwenda ofisi za mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni kushinikiza mawakala wao kupatiwa barua za viapo vyao.
Kamanda Mambosasa amesema polisi pia inawachunguza watuhumiwa 40 ili kubaini iwapo miongoni mwao walikuwepo waliokuwa na silaha za moto.
Amesema pia wanaendelea kuwatafuta wafuasi na viongozi wa Chadema walioshiriki kushawishi wafuasi wao kushiriki kwenye maandamano.  
Wakati huohuo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole katika taarifa aliyoitoa jana Februari 17,2018 alisema chama hicho kinalitaka Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina kuhusu aliyehusika na tukio la kuuawa kwa mwanafunzi huyo.
Polepole alisema polisi imhoji Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na viongozi wenzake walioshiriki maandamano aliyosema hayakuwa halali yaliyosababisha uhai wa Mtanzania kupotea.
Chanzo:Mwananchi

SERIKALI imesema itasambaza magari 120 ya wagonjwa yenye thamani ya Sh bilioni 10 katika vituo vya afya nchi nzima, ikiwa ni nyongeza kwa magari mengine 70 ambayo yalishasambazwa hivi karibuni katika vituo kadhaa vya afya.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa


SERIKALI imesema itasambaza magari 120 ya wagonjwa yenye thamani ya Sh bilioni 10 katika vituo vya afya nchi nzima, ikiwa ni nyongeza kwa magari mengine 70 ambayo yalishasambazwa hivi karibuni katika vituo kadhaa vya afya.
Akizungumza na wakazi wa Kata ya Kahangara, wilaya ya Magu jana, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema serikali imeamua kuhakikisha inakabiliana na upungufu uliopo katika sekta mbalimbali, ikiwemo ya afya na kwamba itahakikisha wananchi wanafikiwa na huduma zenye kiwango.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, ni lengo la serikali kuona huduma muhimu zinaboreshwa kwa wakati na kuongeza kuwa afya ni miongoni mwa maeneo yanayohitaji ufadhili wa kutosha ili kuwa na ubora unaotakiwa.
"Hivi sasa tunajenga vituo vingi vingine vya afya vikiwemo ambavyo tutaweka mahitaji muhimu yakiwemo magari ya wagonjwa.
Karibu tutaongeza magari ya wagonjwa 120, ili kuhakikisha vituo vya afya vinakuwa vimejidhatiti,” alisema. Waziri Mkuu alipongeza Wilaya ya Magu kwa kujenga kituo cha afya cha Kahangara, ambacho kwa mujibu wake ni moja ya kituo cha kisasa kilichotengenezwa kulingana na thamani ya fedha.
Alisema ili kutoa huduma za viwango, usambazaji wa dawa utapewa kipaumbele na kuongeza kuwa Wilaya ya Magu imetengewa Sh milioni 498 na kuzitaka mamlaka za ndani kutumia fedha hizo vizuri.
Aliongeza vituo vya afya sio tu vitajengwa lakini pia vitawekewa vifaa na uhuduma muhimu na kuwa Kahangara itapewa Sh milioni 200 kwa ajili ya kuweka vifaa vitakavyowezesha kufanya operesheni ndogo.
Waziri Mkuu alivitahadharisha vituo vya afya kutonunua dawa zisizohitajika na kuvitaka kuagiza dawa kulingana na mahitaji na si vinginevyo.
Katika kupunguza mzigo wa gharama za tiba, Waziri Mkuu aliwashauri wakazi wa Magu wanajiunge na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ambayo gharama yake kujiandikisha sasa ni Sh 10,000 kwa familia na kufurahia matibabu.
Chanzo:Habari leo

Saturday, 17 February 2018

Baada ya kuwepo kwa dosari kwenye uchaguzi Jimbo la Kinondoni ikiwemo kutolewa nje kwa mawakala wa vyama mbalimbali Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni amejitokeza na kuzimaliza ambapo amewalaumu viongozi wa vyama kushindwa kutekeleza wajibu wao.



DAR ES SALAAM
Baada ya kuwepo kwa dosari kwenye uchaguzi Jimbo la Kinondoni ikiwemo kutolewa nje kwa mawakala wa vyama mbalimbali Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni amejitokeza na kuzimaliza ambapo amewalaumu viongozi wa vyama kushindwa kutekeleza wajibu wao.

Mkurugenzi Aron Kagurumjuli ambaye ndiye Msimamizi wa Uchaguzi Kinondoni amesema kwamba baadhi ya vyama wameshindwa kuwapa barua za utambulishomawakala wao na kutaka kutumia barua za kiapo kama utambulisho.

Mkurugenzi huyo amesema wao kama wasimamizi jukumu lao lilikuwa kutoa barua hizo na pia ni jukumu la viongozi wa vyama kuhakikisha kuwa wanatekeleza wajibu wao kwani huwa ni rahisi kwa wao kukutana na mawakala wao kwani mpaka mawasiliano yao wanakuwa wanayo.

Aidha Mkurugenzi huyo ameweka wazi sababu za wao kutoa barua za utambulisho saa tano usiku ni kuhofia barua hizo kugushiwa.

Hata hivyo amethibitisha kuwa dosari hizo zimeshamalizika na hali ya vituo ni shwari hivyo wananchi wasisite kwenda kupiga kura.
Jimbo la Kinondoni, Siha na kata nane nchini leo yameingia katika zoezi la kupiga kura za kuchagua wabunge watakaoweza kuwakilisha shida za wananchi wa majimbo hayo Bungeni.
Chanzo:Eatv

Friday, 16 February 2018

Rais John Magufuli amewaapisha mabalozi wawili aliowateua kuiwakilisha Tanzania katika nchi za Nigeria na Sweden.



DAR ES SALAAM

Rais John Magufuli amewaapisha mabalozi wawili aliowateua kuiwakilisha Tanzania katika nchi za Nigeria na Sweden.

Taarifa iliyotolewa leo na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi inaeleza kuwa walioapishwa ni Muhidin Ally Mboweto ambaye ameteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Nigeria na Dk Willbrod Peter Slaa ambaye ameteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Sweden.

Uteuzi wa Mabalozi hao kuiwakilisha Tanzania katika nchi walizopangiwa umeanza Rasmi Februari 15, 2018.

 Chanzo:mwananchi


Madiwani wa Halmashauri ya Buchosa wamemuomba Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aondoke na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kwa kutoridhishwa na utendaji wake.


Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa


MWANZA

Madiwani wa Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema wamemuomba Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aondoke na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Bw. Cyprian Luanda baada ya kutoridhishwa na utendaji wake.


Wametoa ombi hilo katika kikao cha Waziri Mkuu na watumishi Halmashauri ya Buchosa akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza.

Waziri Mkuu baada ya kupokea ombi hilo amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Bw. John Mongella kwenda katika halmashauri hiyo na kufanya kikao cha pamoja kati ya Madiwani, Mkurugenzi na watumishi ili kubaini changamoto zilizopo na kuzitafutia ufumbuzi.

Mbali na hayo Mh. Majaliwa ameweka jiwe la msingi la hospitali ya Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema, ambapo ujenzi wake hadi kukamilika unatarajiwa kugharimu sh. bilioni 10.55.

Pia Waziri Mkuu amezindua madarasa manne ya Kidato cha Tano na Sita katika Shule ya Secondari ya Nyehunge wilayani Sengerema na kuwataka wanafunzi wasome kwa bidii.

Chanzo:EATV

Mahakama Kuu imemhukumu kifungo cha maisha jela raia wa Lithuania, Christina Biskavskaja baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya kwenda Ubelgiji



MOSHI

Mahakama Kuu imemhukumu kifungo cha maisha jela raia wa Lithuania, Christina Biskavskaja baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya kwenda Ubelgiji.

Christina ambaye ni mwanamuziki katika Jiji la Kaunas, amekamatwa Agosti 28, 2012 saa tisa alasiri katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) akisafirisha gramu 3,775.26 za heroine zenye thamani ya Sh169 milioni.

Hukumu hiyo imetolelwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Aishiel Sumari amesema ushahidi wa mashahidi saba wa upande wa mashtaka ni mzito na umethibitisha shtaka dhidi ya mshtakiwa huyo.

Jaji Sumari aliukataa utetezi wa mshtakiwa kuwa alibambikiwa kesi hiyo na polisi wa Tanzania na kuhoji hilo linawezekanaje wakati mashahidi wa upande wa mashtaka walikuwa hawafahamiani na mshtakiwa.     

Chanzo: Mwananchi


Kamanda Muliro amesema wamemchukulia hatua za kinidhamu askari polisi wake ambaye jina lake halijawekwa wazi kufuatia kuonekana akichukua rushwa kwenye video za mitandaoni.


Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Muliro J. Muliro



DAR ES SALAAM

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Muliro J. Muliro amesema wamemchukulia hatua za kinidhamu askari polisi wake ambaye jina lake halijawekwa wazi kufuatia kuonekana akichukua rushwa kwenye video za mitandaoni.

Akithibitisha juu ya kuchukua za kinidhamu kwa askari huyo Kamanda Muliro amesema ni kweli Jeshi la Polisi limechukua maamuzi hayo kwa askari huyo ambaye hakutaka kutaja jina lake

Hatua hiyo ya jeshi la polisi imekuja masaa kadhaa baada ya Mwanaharakati wa mambo ya siasa mtandaoni, mrembo Mange Kimambi kuposti video ya askari polisi akichukua rushwa ya pesa kutoka kwa raia ambaye alitenda kosa la barabarani.

Chanzo:EATV


Thursday, 15 February 2018

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako ameahidi Sh50 milioni kwa ajili ya ujenzi wa maabara ya shule ya sekondari ya kata ya Rulanda wilaya ya Muleba mkoani Kagera iliyopewa jina lake.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako

KAGERA

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako ameahidi Sh50 milioni kwa ajili ya ujenzi wa maabara ya shule ya sekondari ya kata ya Rulanda wilaya ya Muleba mkoani Kagera iliyopewa jina lake.

Huku akimpongeza Rais John Magufuli kupendekeza shule hiyo kuitwa Joyce Ndalichako, waziri huyo ameahidi kutoa fedha hizo alipoitembelea shule hiyo na kuongeza Sh3milioni kwa ajili ya kununua vitabu vya wanafunzi.

Amesema pamoja na ujenzi wa barabara atashirikiana na Halmashauri ya wilaya ya Muleba kuhakikisha zinapatikana samani za kutosheleza shule hiyo, pamoja na huduma ya maji huku akiwaomba wananchi kuendelea kuchangia upatikanaji wa maji.

Mkuu wa shule hiyo, Paul Morigo amesema katika awamu ya kwanza  ujenzi wa shule hiyo ulianzishwa na wananchi kwa kuchangia vitu mbalimbali vyenye thamani ya Sh 67.76 milioni . 



Chanzo: Mwananchi 

Wananchi wa kata za Toloha na Kiria wilayani Mwanga wamemtuhumu mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Aaron Mbogho kwa kushindwa kutatua kero ya maji.


KILIMANJARO


Wananchi wa kata za Toloha na Kiria wilayani Mwanga wamemtuhumu mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Aaron Mbogho kwa kushindwa kutatua kero ya maji.

Wakizungumza mbele ya mkuu wa mkoa huo Anna Mghwira ambaye aliambatana na mkuu wa wilaya hiyo wananchi wakata zote mbili wamesema tangu Dc huyo ateuliwe na Rais hashughurikii kero zao.

Mkazi wa Kata ya Kiria, Ayubu Msangi alimuomba Mghwira aifanye Wilaya ya Mwanga iwe Moshi ili aweze kutatua kero zinazowakabili.

Lakini umati wa wananchi umnenukuliwa ukisema hatumtaki mkuu wa wilaya, ana dharau.

Mghwira hakumpa nafasi mkuu wa wilaya kuzungumza badala yake, amemuagiza mhandisi wa maji Wilaya ya Mwanga, Ernesta Kihwele kufunga mabomba yote yaliyoungwa holela ili maji yaelekezwa kwa wananchi.


Chanzo:Paul 

Tuesday, 13 February 2018

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti amelivunja baraza la ardhi la Kata ya Murray wilayani Mbulu mkoani Manyara baada ya wananchi kulalamika kunyanyaswa, kuombwa rushwa na kunyimwa haki zao.


Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti 



MANYARA

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti amelivunja baraza la ardhi la Kata ya Murray wilayani Mbulu mkoani Manyara  baada ya wananchi kulalamika kunyanyaswa, kuombwa rushwa na kunyimwa haki zao.

Baada ya kulivunja baraza hilo, Mnyeti amesema hawezi kuliacha liendelee kufanya kazi kwenye eneo hilo wakati wananchi wanalalamikia kukosa haki zao.

Amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Mbulu, Anna Mbogo kuanza mchakato wa kupatikana viongozi wapya, waadilifu wa baraza la kata hiyo ili waendelee kuwatumikia wananchi.

Pia, Mnyeti amemuagiza mkuu wa polisi wilaya ya Mbulu, kumkamata Mwenyekiti wa kijiji cha Murray, John Amme kwa kuwanyanyasa wananchi yakiwamo madai ya kuwapiga.

Chanzo:Mwananchi

#Changia Damu Okoa Taifa

Jalada kesi ya vigogo wa madini lipo kwa DPP





Dar es Salaam. 
Upande wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya Sh2.4 bilioni  inayomkabili Mkurugenzi wa Tathmini ya Madini nchini,  Archard Kalugendo na mwenzake, umeieleza mahakama kuwa jadala la kesi hiyo lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP)
Mbali na Kalugendo, mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo ni Mthamini wa Madini ya Almasi wa Serikali, Edward Rweyemamu na wote wanakabiliwa na shtaka moja la uhujumu uchumi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Wakili wa Serikali, Estazia Wilson alisema hayo leo Februari 13, 2018 mbele ya Hakimu Godfrey Mwambapa  wakati shauri hilo lilipofika kwa ajili ya kutajwa.
"Upelelezi wa shauri hili umekamilika na jalada la kesi hii tayari lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kwa ajili ya uchunguzi zaidi, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa," amedai  Estazia.
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Mwambapa ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 27, mwaka huu itakapotajwa.
Washtakiwa katika kesi  hiyo namba wa 94 ya mwaka 2017 wanakabiliwa na shtaka la uhujumu uchumi kwa kuisababisha Serikali hasara ya zaidi ya Sh2.4 bilioni.
Inadaiwa kuwa kati ya Agosti 25 na 31, 2017 katika maeneo mbalimbali kati ya Dar es Salaam na Shinyanga, kwa pamoja na kwa vitendo vyao wakiwa wathamini walioajiriwa na Wizara ya Nishati na Madini waliisababisha Serikali hasara ya kiasi hicho cha fedha.
Chanzo:Mwananchi
#Changia Damu Okoa Taifa

Monday, 12 February 2018

Mwenyekiti wa Chama cha Wabunge wanawake TWPG, Bi. Magreth Sitta ameitaka serikali kuandaa mazingira na miundombinu itakaowasaidia watoto wa kike kupata elimu bila kukatisha masomo wanapokuwa katika kipindi cha hedhi.


Mwenyekiti wa Chama cha Wabunge wanawake TWPG, Bi. Magreth Sitta



DAR ES SALAAM

Mwenyekiti wa Chama cha Wabunge wanawake TWPG, Bi. Magreth Sitta ameitaka serikali kuandaa mazingira na miundombinu itakaowasaidia watoto wa kike kupata elimu bila kukatisha masomo wanapokuwa katika kipindi cha hedhi.

Mwenyekiti huyo wa TWPG amesema hayo katika Mafunzo maalumu ya baadhi ya wabunge walioteuliwa juu ya hedhi salama kwa watoto wa kike ambapo wabunge hao wametunikiwa ubalozi kuhusu elimu hiyo.

Bi Magreth Sitta amesema kuwa serikali ina wajibu wa kipekee katika kufikisha elimu kwa watoto wa kike huku wabunge wangine wakimuunga mkono juu ya jitihada za serikali katika kufanikisha azma hiyo.

Aidha wabunge mbalimbali wameunga mkono hoja hiyo kwa kuitaka serikali iliangalie suala hili kwa undani kwani kwa makadirio ya watoto wa kike kushindwa kwenda shuleni kwa mwaka mzima lazima ufaulu wake utakuwa chini.

Wiki iliyopita Mbunge wa kuteuliwa upendo Penneza alijaribu kupeleka hoja binafsi kuhusu wanafunzi wa kike kupatiwa pedi lakini hoja hiyo haikufanikiwa kwani hoja hiyo ilikataliwa kwa sababu yakuwa inavunja ibara ya 99 (2) ya Katiba.
 

Chanzo:Eatv
#Changia Damu Okoa Taifa

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa amewapongeza maaskofu kwa kuunga mkono mambo aliyosema wamekuwa wakiyapigania.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa


DAR ES SALAAM

 Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa amewapongeza maaskofu kwa kuunga mkono mambo aliyosema wamekuwa wakiyapigania.

Lowassa ametoa pongezi hizo wakati akimnadi mgombea ubunge jimbo la Kinondoni, Salum Mwalimu katika Kata ya Kijitonyama.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), limetoa ujumbe wa Kwaresima wa mwaka 2018 ndani yake likitoa msimamo kuhusu masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii nchini.

Ujumbe huo ulioandikwa na maaskofu wote 35 wa TEC wakiongozwa na Rais wake, Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa upo katika kitabu cha kurasa 20 ikiwa ni maandalizi ya ibada hiyo ya siku 40, kipindi ambacho ni cha mfungo wa sala kukumbuka siku 40 za Kristo kufunga na kwenda jangwani.


Chanzo:Mwananchi
#Changia Damu Okoa Taifa

Featured post

MASIKINI WEEE!!!!! KICHANGA CHA SIKU MOJA CHAOKOTWA KATIKA KIWANJA CHA MPIRA AZIMIO

Na;Ezelina Yuda Mtoto mchanga mwenye jinsia ya Kike anayekadiriwa kuwa wa siku 1 ameokotwa akiwa hai kandokando ya uwanja wa azimio  ...