Waziri wa Habari, Utamaduni na michezo, Dk Harrison Mwakyembe
amesema Serikali imefungua milango ya majadiliano na wanahabari kuhusu
changamoto zao.
Akizungumza katika
maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari, leo Mei 3, Waziri Mwakyembe
amesema Serikali imetoa haki ya kupelekwa mahakamani mashauri mbalimbali
kuhusiana na sheria ambazo zimepitishwa lakini bado kuna fursa nzuri ya kufanya
mazungumzo miongoni mwa wadau.
“Serikali itaendelea
kusimamia sheria zilizotungwa katika kuhakikisha wanahabari na wamiliki wa
mitandao ya kijamii wanafanyakazi kwa weledi na kujali maslahi ya taifa na
tamaduni,” amesema.
Amesema Serikali
itahakikisha inasimamia kuundwa kwa vyombo vitatu katika kutekeleza sheria ya
huduma za habari, ambavyo ni baraza huru la habari, Bodi ya Ithibati na kuwepo
kwa mfuko wa kusaidia wanahabari.
"Sheria sasa
inatambua uandishi wa habari kama taaluma hivyo lazima masilahi ya wanahabari
kutazamwa ikiwepo kulipiwa bima na kuingizwa katika mifuko ya hifadhi ya
jamii,"amesema.
Amesema ni muhimu
waajiri kutoa masilahi bora kwa wafanyakazi kwani badala ya kuendelea kuwa na
idadi kubwa ya wafanyakazi ambao hawalipwi vizuri ni bora kuwa na wachache
ambao wanalipwa vizuri.
Hata hivyo, amesema
suala la matangazo kwa vyombo vya habari linafanyiwa kazi lakini pia serikali
haitarudi nyuma katika utekezaji wa usajili na ulipaji wa kodi mbalimbali kwa
mitandao ya kijamii.
No comments:
Post a Comment