Friday, 15 September 2017

Madiwani sita washikiliwa Geita

Madiwani wa Wilaya ya Geita na wananchi wakiwa
Madiwani wa Wilaya ya Geita na wananchi wakiwa wamefunga barabara ya kuingia Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) wakishinikiza mgodi kulipa Dola 12 millioni za Marekani ambazo ni tozo ya kodi ya huduma tangu mwaka 2003 hadi 2013.
Geita. Polisi inawashikilia madiwani sita wa CCM, miongoni mwao wakiwemo waliokusanyika jana na kufunga barabara zinazoingia katika Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM).
Madiwani hao walifunga barabara  wakishinikiza mgodi kuwalipa deni la Dola 12 milioni za Marekani zinazotokana na ushuru wa huduma.
Kukamatwa kwa madiwani hao kunafanya idadi ya waliokamatwa kufikia wanane baada ya wengine wawili kukamatwa siku ya tukio jana Alhamisi.
Polisi pia inamshikilia Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) wilayani Geita, Ally Rajabu kwa makosa hayo ya uvunjifu wa sheria.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo amethibitisha kukamatwa kwa madiwani hao.
Amesema polisi wanaendelea na uchunguzi na watawakamata wote waliohusika kufunga barabara na kuharibu bomba linalotoa maji Ziwa Victoria hadi GGM lililoko Kijiji cha Nungwe.
“Madiwani wamefanya kosa la uvunjifu wa amani, walichofanya ni kosa la jinai na wamekuwa wahalifu kama wengine. Hawajatunga sheria ili wakae juu ya sheria sisi Jeshi la Polisi tunasimamia na kutekeleza sheria,” alisema Kamanda Mwabulambo.
Alisema baadhi ya madiwani wamekimbia na kwamba, kosa la jinai halina ukomo hivyo wataendelea kufuatiliwa na kukamatwa ili kujibu mashtaka.
 @habari na mwananchi

No comments:

Featured post

MASIKINI WEEE!!!!! KICHANGA CHA SIKU MOJA CHAOKOTWA KATIKA KIWANJA CHA MPIRA AZIMIO

Na;Ezelina Yuda Mtoto mchanga mwenye jinsia ya Kike anayekadiriwa kuwa wa siku 1 ameokotwa akiwa hai kandokando ya uwanja wa azimio  ...