Dar es Salaam.
Upande wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya Sh2.4 bilioni inayomkabili Mkurugenzi wa Tathmini ya Madini nchini, Archard Kalugendo na mwenzake, umeieleza mahakama kuwa jadala la kesi hiyo lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP)
Mbali na Kalugendo, mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo ni Mthamini wa Madini ya Almasi wa Serikali, Edward Rweyemamu na wote wanakabiliwa na shtaka moja la uhujumu uchumi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Wakili wa Serikali, Estazia Wilson alisema hayo leo Februari 13, 2018 mbele ya Hakimu Godfrey Mwambapa wakati shauri hilo lilipofika kwa ajili ya kutajwa.
"Upelelezi wa shauri hili umekamilika na jalada la kesi hii tayari lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kwa ajili ya uchunguzi zaidi, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa," amedai Estazia.
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Mwambapa ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 27, mwaka huu itakapotajwa.
Washtakiwa katika kesi hiyo namba wa 94 ya mwaka 2017 wanakabiliwa na shtaka la uhujumu uchumi kwa kuisababisha Serikali hasara ya zaidi ya Sh2.4 bilioni.
Inadaiwa kuwa kati ya Agosti 25 na 31, 2017 katika maeneo mbalimbali kati ya Dar es Salaam na Shinyanga, kwa pamoja na kwa vitendo vyao wakiwa wathamini walioajiriwa na Wizara ya Nishati na Madini waliisababisha Serikali hasara ya kiasi hicho cha fedha.
Chanzo:Mwananchi
#Changia Damu Okoa Taifa
No comments:
Post a Comment