Arusha. Kijana
aliyehusika na matukio ya utekaji watoto mkoani Arusha, Samson Petro (18)
amefariki dunia kwa kupigwa risasi na polisi.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo amethibitisha kutokea kwa kifo hicho
alipozungumza na waandishi wa habari.
Kamanda
Mkumbo amesema kijana huyo ambaye alikamatwa mkoani Geita alikokuwa amekimbia
kabla ya kurejeshwa Arusha alitaka kukimbia alipokuwa anakwenda kuwaonyesha
polisi watuhumiwa wenzake wa utekaji saa tano usiku wa jana Jumatano.
Hivi
karibuni alipokamatwa mkoani Geita, kijana huyo ambaye sasa ni marehemu alikiri
kuwateka watoto wanne mkoani Arusha baada ya kukamatwa mjini Katoro wilayani
Geita alikotekeleza tukio lingine la utekaji.
Akizungumza
akiwa chini ya ulinzi wa polisi wiki iliyopita, kijana huyo alisema watoto
wawili aliwarudisha kwa wazazi wao baada ya kupewa Sh300,000.
Alisema
wengine wawili aliwatelekeza mtaani baada ya wazazi wao kutotoa kiasi cha fedha
walichotakiwa kutoa.
Kijana
huyo alisema alijiingiza katika utekaji watoto kutokana na mahitaji ya fedha.
Alisema aliacha shule akiwa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Lutozo
iliyopo Katoro.
“Naishi
na wazazi wangu lakini nao ni masikini, nilifanyahivi ili nipate fedha na
nilikua nikimchukua mtoto naandika ujumbe kwenye karatasi, naandika na namba ya
simu napeleka karibu na familia ili wanitafute,”alisema.
Awali,
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo alisema walimkamata katika
nyumba ya kulala wageni ya Shitungulu iliyopo mjini Katoro.
Mwabulambo
alisema polisi mkoani Geita kwa kushirikiana na wenzao wa Arusha walifanya
uchunguzi na kubaini mtuhumiwa alikuwa Katoro.
Alisema
walipata taarifa za kutekwa Justin Ombeni (2) Septemba Mosi nyumbani kwao
Shilabela ambako mtuhumiwa alienda na kuwakuta watoto wanne wakicheza nyuma ya
nyumba. Alisema aliwagawia pipi na kuondoka na Justin.
“Baba
wa mtoto alifika kituo cha polisi kutoa taarifa ya mtoto wake kutoweka,
tuliwasiliana na polisi Arusha na makao makuu ambako timu ya watu wanne
walitoka Arusha na kuungana na yetu ambayo imesaidia kumkamata
mtuhumiwa,”alisema Kamanda.
Mwabulambo
alisema polisi ilipata taarifa kuwa kijana huyo yupo chumba namba 103 katika
nyumba hiyo ya wageni ambako waliweka ulinzi kuizunguka.
Alisema
walipoingia chumba hicho walimkuta akiwa na mtoto huyo. Kamanda alisema
mtuhumiwa atafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.
Ombeni
Mshana, ambaye ni baba wa Justin alisema mtekaji huyo alimpatia ujumbe mtoto wa
jirani uliomtaka kutuma Sh4 milioni na walipokuwa wakiwasiliana na mtuhumiwa
alishusha kiwango hadi Sh1 milioni. Alisema polisi walimtahadharisha kwamba
asitume fedha hizo.
Kamanda
Mwabulambo alisema tukio la kutekwa Justin ni la pili katika kipindi cha miezi
minne baada ya mwingine kutekwa. Kesi kuhusu tukio hilo inaendelea mahakamani
baada ya mtoto kupatikana.
Watoto
ambao Petro anadaiwa kuwaua kwa kuwatumbukiza kwenye shimo la choo ambacho
hakijanza kutumika ni Moureen David(6) anayesoma darasa la kwanza shule
ya msingi Lucky Vincent na Ikram Salim(3).
Moureen
alitekwa Agosti 21 saa 11:00 jioni akiwa anacheza nyumbani kwao eneo la
Olasiti, wakati Ikram alitekwa Agosti 26 saa 12:00 jioni akiwa anacheza na
watoto wenzake nyumbani kwao Burka, Olasiti.
No comments:
Post a Comment