Monday, 3 July 2017

Wawekezaji wa madini wabanwe kauli ya wasomi

WAKATI jana Kamati Maalumu ya Pamoja ya Bunge ikikamilisha kupokea maoni ya wadau, miswada mitatu ya madini inasomwa kwa mara ya pili bungeni leo na kuanza kujadiliwa hadi keshokutwa.
Aidha, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimependekeza sheria mpya ya madini iwatake wawekezaji wote kutumia taasisi za fedha na kampuni za bima za ndani ili kuchangia kukua kwa uchumi. Hatua hiyo ni baada ya kamati kupitia maoni yaliyotolewa na wadau kwa siku mbili mfululizo. Muswada ambao utasomwa leo na kuanza kujadiliwa ni Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2017 ambao pia utaendelea kujadiliwa Jumatano.
Kesho utasomwa na kujadiliwa kwa Muswada wa Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba ya Maliasili za Nchi wa Mwaka 2017 na ule wa Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusu Umiliki wa Maliasili wa mwaka 2017. Aidha, wakati wa kutoa maoni, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimependekeza sheria mpya ya madini iwatake wawekezaji wote kutumia taasisi za fedha na kampuni za bima za ndani ili kuchangia kukua kwa uchumi.
Mwakilishi wa chuo hicho, Dk Antidius Kaitu kutoka Shule ya Sheria alisema, “Sheria iwatake wawekezaji kukopa kutoka benki za biashara zilizopo nchini pamoja na kutumia kampuni za bima za ndani, hii mbali na kuchangia uchumi pia itapunguza udanganyifu wa gharama zinazotumika.” Aidha, Dk Kaitu alipendekeza serikali kumiliki hisa kutoka kwenye kila mgodi pamoja na kuwa na kifungu ambacho kitatoa nafasi kwa wawakilishi wa serikali kuingia kwenye vikao vya bodi ya wakurugenzi ili kujua mapato halisi ya kampuni husika zinazoendesha migodi hiyo.
“Serikali ikiwa na wawakilishi kwenye bodi ya wakurugenzi, itasaidia kuongeza uhakika na uhakiki wa mapato ya serikali. Lakini pia kampuni hizi za madini zianze kulipa kodi ya mapato mara tu baada ya kuanza uzalishaji,” alieleza msomi huyo wa sheria. Aidha, wakati sheria ikiwataka wachimbaji wadogo kuanza kulipa kodi kuanzia mwaka huu wa fedha, Dk Kaitu alipendekeza kurudishwa kwa ofisi za madini za kanda ili kuratibu na kusimamia shughuli za wachimbaji wadogo.
Muswada unapendekeza mikataba yote inayohusu rasilimali ambayo serikali itaingia ipelekwe bungeni na kama kutakuwa na mapungufu yoyote hasa yanayotoa masharti yasiyolinufaisha Taifa, Bunge lishauri kufanyika kwa marekebisho. Pia Dk Kaitu alishauri mikataba ya madini ipelekwe bungeni na iwekwe wazi ili serikali ifahamu ni lini hatua hiyo inapaswa kuchukuliwa.
Kwa upande wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), John Seka na Harold Sungusia pamoja na kutaka kuwepo kwa marekebisho kadhaa kwenye baadhi ya vifungu, wameitaka serikali kununua hisa kwenye migodi na kupendekeza sheria iseme hisa zinazonunuliwa zinaenda wapi na kupendekeza ziwe chini ya Shirika la Madini (STAMICO).

No comments:

Featured post

MASIKINI WEEE!!!!! KICHANGA CHA SIKU MOJA CHAOKOTWA KATIKA KIWANJA CHA MPIRA AZIMIO

Na;Ezelina Yuda Mtoto mchanga mwenye jinsia ya Kike anayekadiriwa kuwa wa siku 1 ameokotwa akiwa hai kandokando ya uwanja wa azimio  ...