TANZANIA imetajwa kuwa nchi iliyofanikiwa kuwa na mfumo wa Kielektroniki uliojengwa na wataalamu wake wa ndani wenye uwezo wa kuunganisha vituo vya kutolea huduma kama Zahanati ,Shule, Vituo vya Afya na Hospitali zote nchini hali itakayowezesha kuongezeka kwa ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi katika maeneo yao.
Hayo yamesemwa na Mtaalam wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa Mradi wa Uimarishaji wa mifumo ya Sekta za Umma (PS3), Desderi Wengaa kuwa Tanzania imeonyesha mafanikio makubwa kwa kuwa na wataalamu wenye uwezo wa kujenga mifumo ya kielektroniki itakayosaidia kuchochea maendeleo.
“Tanzania imekuwa nchi ya mfano Afrika Mashariki, Kusini mwa Afrika na Afrika kwa kuwa na mfumo unaowezesha wananchi kutoa mrejesho wa huduma wanazopata katika maeneo ya kutolea huduma hali itakayoongeza uwazi na uwajibikaji,” amesema Wengaa.
Mafunzo kwa watumiaji wa mfumo wa PlanRep yanawahusisha Waganga Wakuu wa Mikoa, Halmashauri, Wachumi, Maafisa Mipango, Wahasibu, na Makatibu wa Afya, kutoka mikoa ya Manyara, Tanga, Dodoma, Singida na Tabora.
Mikoa minginine nchi nzima tayari imeshapatiwa mafunzo hayo ambapo uzinduzi rasmi wa matumizi yake unataraji kufanyika mapema mwezi huu. Mradi wa PS3 unatekelezwa na Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) na umejikita katika maeneo ya Utawala Bora na Ushirikishwaji wananchi, Rasilimali watu, Rasilimali Fedha, Mifumo ya TEHAMA pamoja na Tafiti Tendaji, Tathimini na ufuatiliaji.
No comments:
Post a Comment