Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Mkewe wamewatembelea wagonjwa waliolazwa katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kuwashukuru Madaktari na Wauguzi kwa juhudi kubwa wanazofanya kunusuru maisha ya watu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiwa anaongea na Mzee Ngosha
Miongoni mwa wagonjwa waliojuliwa hali ni Mzee Francis Maige Kanyasu (Ngosha) aliyelazwa katika chumba namba 310 na Mtoto Shukuru Musa Kisonga aliyelazwa katika chumba namba 312 ambaye hivi karibuni aliripotiwa kuugua ugonjwa usiofahamika uliosababisha aishi kwa kunywa mafuta ya kula, sukari na Maziwa.
Rais Magufuli na Mama Janeth Magufuli wamefanya matembezi hayo leo majira saa moja ya asubuhi wakiwa wanatokea katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Petro liliopo Oysterbay Jijini Dar es Salaam ambako walihudhuria ibada ya Jumapili.
Aidha, Rais Magufuli amesema serikali itaendelea kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili hospitali hiyo pamoja na zile zinazowakabili madaktari na wauguzi hao.
“Jamani, Madaktari tunawashukuru sana, mnafanya kazi nzuri, Madaktari wote nchini pokeeni pongezi zangu, sisi serikali tutaendelea kuzikabili changamoto hizo na siku moja zitakwisha. Kikubwa ni kumtanguliza Mungu mnapofanya kazi ya kuokoa maisha ya watu kwa juhudi kubwa, mnafanya kazi ya Mungu”alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli na Mkewe wakiwa wanaongea na Mtoto Shukuru
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Lawrence Museru ameweza kumshukuru Rais Mgufuli kwa kuwatembelea huku akisisitiza kuwa tayari madaktari wamegundua magonjwa yanayomkabili Ngosha pamoja na Mtoto Shukuru.
Aidha, Prof. Museru amesema hospitali hiyo imepiga hatua kubwa ya kujenga uwezo wa kutibu magonjwa ambayo wagonjwa walilazimika kwenda kutibiwa nje ya nchi na hivyo kuokoa fedha nyingi za serikali.
“Mhe. Rais hospitali yetu sasa imeanza kufanya upasuaji na kutoa tiba ya magonjwa ambayo yalilazimu wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi, mfano hivi sasa tunatoa huduma ya kusafisha figo kwa wagonjwa takribani 250, na kuanzia mwezi Julai mwaka huu tutaanza kupandikiza figo.Huduma hii hugharimu kati ya Shilingi Milioni 60 na Shilingi Milioni 70 kwa mgonjwa mmoja anayekwenda kutibiwa nje ya nchi, lakini hapa nchini gharama zinashuka hadi Shilingi Milioni 21” alisema Prof. Museru.
Kwa upande mwingine Prof. Museru amesema kuwa hospitali ya Muhimbili imejipanga kuanza kutoa huduma ya matibabu kwa watoto wenye matatizo ya usikivu ambao wapo hatarini kuwa viziwi ili kuweza kuokoa fedha nyingi zinazokazo kwenda kuwatibu nje ya nchi, kutoka Shilingi Mil 90 hadi Mil 30.
No comments:
Post a Comment