Mamluki wamejaribu kuipindua serikali ya Equatorial Guinea, kwa mujibu wa serikali ya nchi hiyo.
Takriban wanaume 30 waliojihami kutoka Chad, Cameroon na Jamhuri ya Afrika ya kati walikamatwa mwezi uliopita, kulingana na waziri mmoja.
Walipatikana wakiwa roketi, bunduki na risasi kwenye mpaka nchini Cameroon.
Serikali ya Rais Teodoro Obiang Nguema, imekuwa ikilaumiwa kwa ufisadi na ukiukaji wa haki za binadamu.
Wanajeshi nchini Equatorial Guinea walimuua kwa kumpiga risasi mamluki wakati wa makabiliano siku ya Jumatano karibu na mpaka na Cameroon, kwa mujibu wa runinga ya taifa TVGE.
Bw. Obiang amekuwa madarakani kwa karibu miaka 40, baada ya kutwaa madaraka kwa njia ya mapinduzi ya kijeshi mwaka 1979 na kumuondoa madarakani mjomba wake Francisco Macias Nguema ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi.
Katika taarfa iliyosomwa kupitia radio ya taifa, waziri wa ulinzi Nicholas Obama Nchama aliwalaumu mamluki waliokuw wamepewa kazi na makundi ya upinzani na kusaidiwa na mataifa ambayo hayakutajwa.
Alisema kuwa mapinduzi hayo yalizimwa kwa msaada wa idara za usalama za Cameroon.
Equatorial Guinea imekumbwa na madai ya mapinduzi ya kijeshi siku za awali.
Mwaka 2004 mwanajeshi wa zamani raia wa Uingereza Simon Mann alihusishwa na jaribio la kumpindua Obiang.
Mwanajeshi huyo wa zamani wa Uingereza na mafanyabiashara alikamatwa nchini Zimbabwe mwaka 2004 na kusafishwa kwenda Equatorial Guinea miaka minne baadaye.
Mwaka 2008 Bw. Mann alihukumiwa miaka 34 jela, lakini mwaka mmoja baadaye aliachuliwa baada ya kusamehewa na Bw. Obiang.
Equatorial Guinea ni moja ya nchi wazalishaji wakubwa wa mafuta lakini asilimia kubwa ya watu wake wanaishi katika hali ya umaskini.
Chanzo:Bbc swahili
No comments:
Post a Comment