Adhabu kali inawasubiri walioshiriki maandamano ambayo yameikumba Iran kwa kipindi cha wiki moja iliyopita. Na haya ni kulingana na kamanda mmoja mkuu wa jeshi la Iran anayesisitiza kwamba maandamano hayo yamekwisha.
Usemi wake haujathibitishwa baada ya mitandao kadhaa ya kijamii kuonesha video za maandamano katika angalau miji sita hivi.
Kamanda huyo Mohammed Ali Jafari alithibitisha kwamba maandamano hayo yalikuwa yameenea katika miji kadhaa baada ya kuanza Desemba 28 lakini akaongeza kuwa, juhudi walizofanya maafisa wa kuimarisha usalama na hatua ya watu wengi kuamua kutoshiriki yaliyafanya maandamano hayo kuisha nguvu.
Jafari amesema alihesabu kati ya watu 1,500 na 15,000 walioshiriki maandamano hayo katika siku za hivi karibuni na amesema sababu nyengine iliyochangia kwa watu wachache kushiriki ni kule kuzimwa kwa baadhi ya mitandao ya kijamii kama Telegram na Instagram. Waziri wa mawasiliano wa Iran Mohammad-Javad Azari Jahromi, alisema Telegram itafunguliwa tena pale ujumbe wa kigaidi utakapotolewa katika mtandao huo.
Maandamano hayo yalishuhudia watu 21 kufariki dunia
Huku hayo yakiarifiwa mshindi wa tuzo ya Nobel kutoka Iran Shirin Ebadi amewasisitizia Wairan kuendelea na maandamano kote nchini humo. Gazeti linalomilikiwa na Saudi Arabia la pan Arab daily, limemnukuu wakili huyo maarufu wa haki za kibinadamu nchini Iran akisema Wairan wanastahili kuendelea na maandamano kwani katiba inawapa haki ya kufanya hivyo.
Maandamano hayo ya siku sita ambayo yalianza kutokana na ugumu wa kiuchumi wanaopitia vijana na watu wanaofanya kazi yamegeuka na kuwa vuguvugu dhidi ya uongozi hususan kiongozi mkuu Ayatollah Ali Khamenei.
Parvaneh Alizadeh anafanya kazi ya uhasibu nchini Iran na hapa anaelezea jinsi maisha ya mwananchi wa kawaida yalivyo magumu Iran, "viongozi wa nchi wana jukumu la kuwahudumia watu wao. Tunapompigia kura mbunge, ni jukumu lake kutusikiliza," alisema Parvaneh. "Haikubaliki kamwe kwa wao kuketi katika afisi zao na wasijue hata bei ya nyama au kilo ya mchele, au hata kutojua jinsi ilivyokuwa vigumu kwa watu kuishi vizuri," aliongeza mhasibu huyo.
Rais Donald Trump aliunga mkono maandamano hayo
Watu 21 waliuwawa katika maandamano hayo na Marekani imesema itawawekea vikwazo wale waliohusika katika kufanya mauaji hayo dhidi ya waandamanaji. Afisa wa serikali ya Marekani ambaye hakutaka kutambulishwa amesema serikali itaanza kutafuta taarifa kuhusiana na maandamano hayo na iwaadhibu waliohusika katika kukiuka haki za waandamanaji.
Rais Donald Trump alisisitiza Wairan wanajaribu kuichukua serikali yao na akaandika katika ukurasa wa mtandao wake wa kijamii wa Twitter akisema Marekani itaonesha uungaji mkono wake wa hayo yanayoendelea Iran wakati mwafaka.
Siku ya Jumatano kulikuwa na maandamano ya kuiunga mkono serikali katika miji kadhaa ukiwemo mji wa pili mkuu nchini humo Mashhad. Televisheni ya taifa ilionesha maelfu ya waandamanaji wakiwa wamebeba picha ya kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei na mabango yaliyotaka wanaoipinga serikali wauwawe.
Chanzo: Dw swahili
No comments:
Post a Comment