Kundi hili linajumuisha wanaotoa mafunzo ya taaluma mbalimbali na wapo waliopewa majina baada ya kuzaliwa ni Mwalimu.
Lakini, kwa Tanzania ametokea mtu unayeweza kusema mwalimu nambari moja na unapotaja mwalimu kwa hapa nchini au kumzungumzia nje ya nchi siyo mwingine ni Julius Kambarage Nyerere.
Ni miaka 18 tangu Mwalimu Nyerere kuiaga dunia na Wantanzania wa rika tofauti waliomfahamu kwa kumuona au kusikia habari zake wanamuelewa kwa mengi, ukweli na ubunifu.
Nilipotakiwa niandike kumbukumbu ya Mwalimu sikujua nianzie wapi, lakini nilijua vipi nimalizie. Nayo ni mzalendo aliyekuwa hapendi makubwa, hakuwa na majigambo, ujeuri wala kiburi na ni kiumbe aliyefahamu maisha na matarajio ya aliowaongoza. Alichukia mambo ya ufahari na hata misafara yake ilionyesha hivyo na aliwajali masikini ambao zamani walikuwa wakiitwa makabwela, lakini siku hizi wanajulikana kama walala hoi.
Jingine ambalo kwa miaka ya sasa nadra kuonekana kwa wenye mamlaka na madaraka ni uvumilivu, tofauti na viongozi wengine Nyerere alikiri hata kwa shingo upande alipofanya makosa.
Katika siku za mwisho za uhai wake, Mwalimu alikuwa mtu aliyekubali mageuzi ya aina moja au nyingine kama mambo yasiyoepukika katika maisha ya mtu na taifa. Wapo waliosema alikuwa haambiliki, lakini uzoefu niliopata niliposafiri naye kuandika habari za ziara zake, kuhudhuria mikutano yake ya ndani na nje na kuzungumza naye mara nyingi nilimuona kuwa mtu msikivu.
Lililokuwa muhimu ni namna ulivyomhadithia jambo, kwa sababu alielewa hata mambo ya mitaani na hisia za wananchi kwa masuala mbalimbali utadhani kachero.
Kwa ufupi, ilikuwa siyo rahisi kumdanganya na ukienda kumjaza fitna ole wako, utaomba ardhi ipasuke ujifukie kwa vile hakuwa na muhali na watu wa aina hiyo.
Nilipofuatana naye kama mwandishi wa Daily News kuanzia miaka ya mwishoni ya 1960 hadi miaka ya mwanzo ya 1980 na baadaye mwandishi wa aliyekuwa Waziri Kiongozi wa Zanzbar na sasa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad nilijifunza mengi kwake.
Mojawapo ni umuhimu wa mtu kuwa msikivu na kutokubali au kukataa haraka kila unaloambiwa, bali kwanza apime au ajipe muda ndiyo afanye uamuzi.
Jambo jingine, kwa lugha alioitumia hivi karibuni Rais John Magufuli, Mwalimu hakuwa mtu wa kujaribiwa, lakini naye hakuwajaribu aliowaongoza kwa kauli zisizokuwa na kichwa wala miguu au ahadi zisizotekelezeka.
Siku moja, nikiwa kituo changu cha kazi Arusha nilikwenda Mbulu siku mbili kabla ya Mwalimu kuanza ziara ya Mto wa Mbu, Manyara, Upper Kitete, Karatu, Oldeani na vijiji vyengine.
Kilichonishangaza ni Mwalimu kuulizia mambo ambayo waandishi wa habari (tulikuwa watu wanne) hatukuwa na tetesi nayo, wala kusikia yakigusiwa tulipofika Mbulu siku mbili kabla ya Mwalimu kuanza ziara.
Tukio moja huwa silisahau. Nalo ni pale tulipokuwa Mbulu aliposomewa risala iliyolezea maendeleo, ikiwamo kuwaondoa Watindiga waliokuwa wanaishi porini na wengine kulala juu ya miti nusu uchi. Zoezi hili lilienda sambamba na kuwavalisha nguo Wamasai ambao kivazi cha wengi wao siku zile ni cha kuweka “ Mambo hadharani”.
Baada ya kusomwa risala Mwalimu alimuangalia Mkuu wa Mkoa, mzee Aaron Mwakang’ata na kumuuliza ni hayo tu na kabla mkuu wa mkoa hajasema kitu, Mwalimu alituangalia waandishi wa habari. Alitwita sote kwa majina
Hubert (Cheche) wa Maelezo, Patrick (Makomu) wa Uhuru , Salim (mimi) kweli ni haya tu.
Wakati tukitazama na kujiuliza kulikoni, Mwalimu alitaka kujua habari za watoto waliozaliwa kwa “mwendo wa kasi”.
Hapo likazuka jambo kuhusu mkuu wa wilaya aliyetuhumiwa kutumia mdaraka yake kutembea na wake za watu na walimu wa kike. Kufuatia tuhuma hizo Mwalimu alilazimika kumfungisha virago kiongozi huyo kurudi kwao Musoma.
Mwalimu alitumia mchezo wa bao na kucheza na wazee wa Dar es Salaam nyumbani kwake Msasani kuelewa hali halisi nchini .
Mwalimu alikuwa hapendi fitna kuna wakati nilipokuwa na waandishi wenzangu wa Daily News tulifuatilia kashfa katika lililokuwa Shirika la Maendeleo ya Sukari (Sudeco). Waziri mmoja kutoka Zanzibar alifika ofisini kwetu jijini Dar es Salaam na kututaka tuachane na habari ile, kwa vile gazeti la Serikali halitarajiwi kufanya
Tulimpinga na kumwambia hatukuwa tayari kupokea maelekezo yake, kwa vile Mharii Mkuu wa gazeti ni Rais Nyerere na chombo kilichokuwa na mamlaka ya kutoa maelekezo ni Bodi ya Wakurugenzi ambayo Mwenyekiti wake alikuwa J.K. Chande. Waziri alikisarika na kuondoka, baadaye tulielezwa kwamba alikwenda Msasani kutuchomea utambi, lakini Mwalimu alimwambia hakumtuma kufanya kazi hiyo na yeye (Mwalimu) ndiyo Mhariri Mkuu na alikuwa akifuatilia suala hilo kwa makini.
Tuliandika kashfa hiyo ya Sudeco ikiwamo uchambuzi, matokeo yake viongozi waliohusika walifukuzwa kazi na wengine kushtakiwa kwa ufisadi. Kwa upande mmoja huyu ndiye Mwalimu nimjuaye.
Kwa upande wa Zanzibar, Mwalimu aliwahi kukasirishwa na utekelezaji miradi kwa kukurupuka au kutoshirikisha wataaalamu.
Mfano, mwishoni mwa miaka ya 60 alitembelea Zanzibar na kushangazwa na ujenzi wa mradi wa nyumba za wanajeshi uliofanyika eneo la Migombani, huko alikutana na kituko kuwa nyumba hizo alizokwenda kuzindua hazikuwa na vyoo na ilibidi aulize mbona zile nyumba zilikuwa kama viota vya ndege?
Alipoambiwa vyoo vingejengwa baadaye kwa vile wanajeshi walikuwa na hamu ya kuhamia, alibaki kinywa wazi na kuwaangalia kwa mshangao viongozi aliokuwa nao.
Baadaye ilisemekana mkandarasi alipewa ramani iliokuwa na vyumba vya kulala, kumbi za kupumzikia, jiko na stoo. Vyoo havikuwamo na mkataba wa ujenzi haukuzungumzia vyoo.
Alifanya dhihaka iliotoa ujumbe kwa kusema, mara ya pili ukiwapo mradi kama huo vyoo vijengwe kwanza na baadaye yafuate mengine.
Yapo mengi yaliyofanyika visiwani yaliyomkera na baada ya kuvumilia aliyatapika na kuchukua hatua, ijapokuwa kuna lawama ambazo hawezi kukwepa kama vile mauaji ya wana siasa mashuhuri na waliopigania uhuru.
Hata hivyo, Mwalimu alijisafisha, ikiwamo kukataa kuwarejesha Zanzibar watu waliokabiliwa na tuhuma nzito, kama kundi la aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Abdulrahman Babu na wenzake kwa madai ya kuhusika na kuuawa kwa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume.
@habari na mwananchi
No comments:
Post a Comment