Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango |
DAR ES SALAAM
SERIKALI imetangaza kuwa madai yote sahihi ya watumishi wa umma ya Sh bilioni 43.39 yatalipwa pamoja na mshahara wa mwezi Februari mwaka huu.
Aidha, serikali imeokoa zaidi ya Sh bilioni 84.22 baada ya kubaini madai ya watumishi 64,722 kati ya watumishi 82,111 waliokuwa wakidai zaidi ya Sh bilioni 127.61 za malimbikizo ya mshahara, hayakuwa halali.
Hayo aliyabainisha Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu malipo ya madai ya malimbikizo ya mishahara wa watumishi wa umma waliokuwa na madai.
Alisema, serikali kupitia mfumo wa taarifa za kiutumishi na mishahara kufikia Julai 1, 2017 ilikuwa na madai ya malimbikizo ya mishahara yenye jumla ya Sh 127,605,128,872.81 kwa watumishi 82,111.
Dk Mpango alisema kati ya watumishi hao, walimu walikuwa ni 53,925 waliokuwa wanadai Sh 53,940,514,677.23 ambao ni sawa na asilimia 42.27 ya madai yote na wasiokuwa walimu walikuwa ni 28,186 waliokuwa wanadai Sh 73,664,614,195.58 sawa na asilimia 57.73.
“Madai haya yalijumuisha mishahara isiyolipwa, tofauti ya mishahara kutokana na kukaimu na nyongeza za mishahara zilizotokana na kupandishwa vyeo na kuchelewa kurekebishiwa mishahara,” alisema.
Alisema, baada ya kufanya uhakiki wa kina wa madeni hayo, serikali ilibaini kuwa watumishi 27,389 kati ya 82,111 yenye jumla ya Sh 43,393,976,807.23 ikiwa ni asilimia 34 ya madai yote ya zaidi ya Sh bilioni 127.61 yaliyohakikiwa yameonekana ni sahihi na yanastahili kulipwa bila marekebisho.
Dk Mpango alisema, madai yanayostahili kulipwa yanajumuisha Sh bilioni 16.25 kwa walimu 15,919 na Sh bilioni 27.15 kwa watumishi wasiokuwa walimu ni 11,470. “Kwa matokeo ya uhakiki yaliyofanywa ikiwa ni pamoja na kazi ya kuwaondoa kwenye mfumo wa malipo ya mshahara watumishi hewa, vyeti feki na wasiokuwa na sifa na uhakiki wa madai ya malimbikizo ya mishahara uliofanyika umeweza kuokoa kiasi kikubwa cha fedha cha Sh bilioni 84.22 ambayo ni sawa na asilimia 66.
“Ina maana kama tusingekuwa tumefanya uhakiki deni hili la Sh bilioni 127.61 lililokuwa kwenye mfumo ambalo bila uhakiki kufanyika lingelipwa wakati lilikuwa halistahili kulipwa,” alieleza.
Aidha, Dk Mpango alisema madai yote yaliyoonekana kuwa sahihi ya shilingi bilioni 43.39 yatalipwa pamoja na mshahara wa mwezi Februari mwaka huu kwa mkupuo mmoja. “Madai haya ambayo mengine yana zaidi ya miaka 10 majina ya walipwaji wote yatatangazwa kesho (leo).
Serikali itaendelea kulipa madai ya watumishi kadiri yanavyojitokeza ili kuondokana na malimbikizo ya aina hii ambayo yanaweza kusababishia serikali hasara kwa kulipa madai yasiyostahili,” alifafanua.
Majina ya watumishi watakaolipwa mafao yanapatikana katika tovuti ya Wizari ya Fedha na Mipango www.mof.go.tz na tovuti ya Idara ya Habari (MAELEZO) www.maelezo. go.tz.
Chanzo:Habari leo
#Changia Damu Okoa Taifa
No comments:
Post a Comment