Rais John Magufuli ameonya dhidi ya baadhi ya wanasiasa ambao wamekuwa wakibeza juhudi za serikali katika kupigania maslahi ya nchi pamoja na juhudi za kukabiliana na wahalifu ambao wanawaua raia wasio na hatia pamoja na askari polisi.
Rais Magufuli ametoa onyo hilo leo wakati akiweka jiwe la msingi na kuzindua kazi za mradi wa ujenzi, ukarabati na upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam, hafla iliyofanyika katika eneo la bandari hiyo.
“Wajifunze kufunga midomo yao wakati Serikali inafanya kazi yake, na kwa ujumbe huu nataka Watanzania waelewe kuwa tuna mambo makubwa katika nchi hii tunayoshughulika nayo, na ndio maana wakati mwingine unakuta ni mzahamzaha tu, unakuta wakati mwingine mnashughulikia rasilimali za Watanzania zinazoibiwa, mtu mwingine anapinga hadharani” amesema Rais Magufuli.
Ujenzi, ukarabati na upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam umepangwa kufanyika kwa miezi 30 kuanzia sasa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 926.2 ambapo kati yake Shilingi Bilioni 132 zinatolewa na Serikali ya Tanzania, Shilingi Bilioni 770 ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia na Shilingi Bilioni 24 ni Msaada kutoka Shirika la Maendeleo la Uingereza (DFID).
Kazi za ujenzi, upanuzi na ukarabati huo zitafanyika katika gati namba 1 hadi gati namba 7 ambazo zinaendeshwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na zitahusisha kujenga gati hizo, kuongeza kina cha bahari kwa kuongeza urefu kutoka wastani wa mita 12 hadi kufikia mita 15.5 na kukarabati miundombinu wezeshi ya bandari.
Mradi huo mkubwa utaiwezesha bandari ya Dar es Salaam kuongeza uwezo wa kuhudumia meli kubwa kutoka meli zenye urefu wa meta 243 na uwezo wa kubeba makontena kati ya 2,500 na 4000 hadi kufikia meli zenye urefu wa meta 320 na uwezo wa kubeba makontena kati ya 6,000 na 8,000 na pia kuongeza uwezo wa kuhudumia shehena za mizigo kutoka tani Milioni 18 za sasa hadi kufikia tani Milioni 28 ifikapo mwaka 2022.
No comments:
Post a Comment