WENYEVITI wawili wa Serikali ya Kijiji cha Mwamabondo na Songambele, Charles Buligi na Machele Kalele na watu wengine 55 kutoka Kata ya Loya Wilaya ya Uyui mkoani Tabora, wamefi kishwa mahakamani wakikabiliwa na tuhuma nne za kujaribu kuua wanawake wanne.
Watuhumiwa hao walifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Tabora, Emmanuel Ngigwana jana. Wenyeviti waliofikishwa mahakamani hapo ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Songambele, Machele Kalele mwenzake wa Mwamabondo, Charles Buligi.
Upande wa mashitaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Idd Mgeni uliiambia mahakama hiyo kuwa watuhumiwa hao walitenda makosa hayo Septemba 17, mwaka huu. Mgeni alidai kwenye shitaka la kwanza kuwa siku hiyo majira ya mchana, watu hao katika Kijiji cha Mwamabondo wilayani Uyui, walijaribu kumuua Elizabeth Kashindye.
Ilidaiwa katika shitaka la pili, tatu na nne kuwa Septemba 17, mwaka huu majira ya mchana katika Kijiji cha Mwamabondo, watuhumiwa walijaribu kuwaua Manugwa Lutema, Rahel Mkomazwa na Maria Sahani wakiwatuhumu kuwa ni washirikina.
Watuhumiwa wengine waliosomewa mashitaka hayo ni Basu Mitalu, Gwala Mwita, Dettu Macha, Mwandu Samwel, Kapaya Sombi, Masanja Sadi, Yaledi Masegese, Soda Mateman, Masanja Ditu, Samson Kabizo, Jumanne Lugembe, Mayombya Nyanda, Mwandu Masanja, Makoye Madirisha, Juma Charles na Mbulu Chagijo.
Pia wamo Masanganya Sinzo, Shija Jileka, Bala Mangosa, Jitumbi Mboje, Jileke Numbua, Samudi Buchenja, Shaban Saguda, Kaseko Masinzagule, Masanja Magite, Jilala Salum, Shinje Malosa, Japhet Nicholaus, Boniphace Deo, John Yusuph, Chinumbo Jileke, Shija Mayunga, Fred Elia, Haji Kashinje, Haji Ramadhan, Shilinde Jileke na Mashana Matemba.
Wengine ni Masunga Barabara, Shinje Masanja, Mwandu Ndashimu, Sungu Anthony, Rambo Kihanda, Yohana Charles, Said Daud, Basu Mpamwa, Makoleo Kashiwa, Kuba Samwel, Nkuba Zengo, Shigela Ngelela, Sambo Cholamadama, Michael Kashinye, Hamis Makoleo na Mbiji Mwanamila.
Shauri hilo limeahirishwa hadi Oktoba 10, mwaka huu, na dhamana kwa watuhumiwa zitafikiriwa baada ya kujiridhisha juu ya afya za walalamikaji ambao wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kitete kwa matibabu kufuatia majeraha waliyopata.
Septemba 16, mwaka huu, mkazi wa kijiji hicho cha Mwamabondo, Mafumbi Jilawise ambaye ni mume wa Manugwa Lutema, alifariki dunia na ndipo wananchi wakawashambulia akinamama hao wakiwatuhumu kwa ushirikina wakiwahusisha na kifo hicho.
Kutokana na shambulio hilo, Jeshi la Polisi Kikosi cha Kutuliza Ghasia walilazimika kufika kijijini hapo na kuwaokoa akina mama hao ambao walikuwa tayari mikononi mwa wananchi hao wakihukumiwa kwa kuchapwa fimbo na kutaka kuchomwa moto.
@habari na habari leo
No comments:
Post a Comment