Friday, 20 October 2017

Chiloba ang’oka IEBC.



Nairobi, Kenya. 
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Ezra Chiloba ambaye amekuwa akipigwa vita na muungano wa upinzani wa Nasa, hatimaye ameamua kuchukua likizo na kupisha uchaguzi mkuu wa marudio wa Alhamisi ijayo.
Kwa mujibu wa vyanzo kutoka ndani ya IEBC, Chiloba amechukua “uamuzi binafsi kwenda nje ili kujenga hali ya kujiamini kwa wadau” waliokuwa wakimlalamikia.
Ofisa huyo amekuwa katika shinikizo kali kutoka kwa wafuasi wa Nasa wakimtaka ajiuzulu, huku mgombea urais kupitia muungano huo Raila Odinga akiitisha maandamano yenye lengo la kumlazimisha aondoke ofisini pamoja na maofisa wengine wakishutumiwa kwa kuhusika kuvuruga uchaguzi wa Agosti 8 ambao Rais Uhuru Kenyatta alitangazwa kuwa mshindi.
Baadaye matokeo ya uchaguzi huo yalifutwa na Mahakama ya Juu baada ya kujiridhisha kwamba haukuwa umeandaliwa kwa kuzingatia Katiba na sheria.
Chiloba ameamua kuchukua likizo siku chache baada ya mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati kuwataka maofisa wanaosema “vibaya” baada ya uchaguzi kubatilishwa wajiuzulu. Mwenyekiti huyo aliwaambia maofisa hao kwamba uchaguzi hautaweza kuwa wa kuaminika wao wakiwa ofisini.
Katika uamuzi wake, Mahakama ya Juu haikubaini ushahidi wowote maofisa hao kuhusika kutenda makossa lakini wanasiasa wamekuwa wakilalamika na kuishutumu tume kwa kuhusika kudanganya, kuvuruga na kuiba kura.
Jana jioni, vyanzo hivyo vilisema uamuzi wa kuchukua likizo ulifikiwa baada ya majadiliano kati ya mwenyekiti na kwamba Chiloba anaamini hata baada ya yeye kujiondoa bado uchaguzi huo utakuwa wa kuaminika kwa sababu maandalizi yaliyofanyika yalifanyika katika msingi wa kutatua dosari zilizotajwa na Mahakama ya Juu.
@habari  na mwanachi

No comments:

Featured post

MASIKINI WEEE!!!!! KICHANGA CHA SIKU MOJA CHAOKOTWA KATIKA KIWANJA CHA MPIRA AZIMIO

Na;Ezelina Yuda Mtoto mchanga mwenye jinsia ya Kike anayekadiriwa kuwa wa siku 1 ameokotwa akiwa hai kandokando ya uwanja wa azimio  ...