Thursday, 26 October 2017

Mwakyembe: Viongozi wa dini wajengeeni waumini kuwa wazalendo.


SERIKALI imewataka viongozi wa madhehebu ya dini nchini, kuwajengea waumini wao moyo wa uzalendo kwa nchi yao kupitia mafundisho na mahubiri yao.
Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alipokutana na viongozi wa madhehebu ya dini nchini, kujadili mada iliyosema ‘Imani na Uzalendo Kuelekea Uchumi wa Viwanda’ ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kujenga uzalendo na utaifa kwa Watanzania.
Mwakyembe aliwakumbusha viongozi hao wa dini kuwa uzalendo ni hali ya mtu kuwa na uchungu na taifa lake katika kuliletea maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kulitetea.
Kutokana na dhana hiyo ya uzalendo, Serikali imewasisitiza viongozi wa dini kupitia mafundisho yao kuwakumbusha waumini wao kutekeleza mambo kumi kama sehemu ya imani yao, lakini kwa ustawi na maslahi ya taifa.
Mambo hayo kumi ni pamoja na wajibu wa kila muumini kulipa kodi, kuzingatia usafi na utunzaji wa mazingira, kufanya kazi kwa bidii kwa kuwa Watanzania wana sifa nzuri ya kuchapa kazi, wanapokuwa nje ya nchi tofauti na wanapokuwa hapa nchini.
“Mambo mengine ambayo tunawaomba muwakumbushe waumini wenu ni uadilifu, kutii mamlaka, kulinda rasilimali za nchi kwa moyo, nguvu na akili zote, kupinga rushwa na matumizi ya dawa za kulevya pamoja na kuzingatia uaminifu kwa kujieupesha na vitendo vya wizi,” alieleza Dk Mwakyembe.
Waziri Mwakyembe aliwaambia viongozi wa dini kuwa wana jukumu kubwa la kuirejesha jamii ya Watanzania kwenye mstari, kwa kusisitiza uzalendo na utaifa ili taifa liwe na amani na utulivu na liweze kufikia malengo ya kuwa na uchumi wa viwanda.
“Matatizo makubwa katika nchi huanza polepole na tusipoziba ufa tutajenga ukuta. Msichoke kuhubiri amani kwenye nyumba zenu za ibada ili amani tuliyonayo tangu tupate uhuru iendelee kudumu, ,” alieleza Mwakyembe.
@habari na habari leo

No comments:

Featured post

MASIKINI WEEE!!!!! KICHANGA CHA SIKU MOJA CHAOKOTWA KATIKA KIWANJA CHA MPIRA AZIMIO

Na;Ezelina Yuda Mtoto mchanga mwenye jinsia ya Kike anayekadiriwa kuwa wa siku 1 ameokotwa akiwa hai kandokando ya uwanja wa azimio  ...