Friday, 3 November 2017

EU yatoa bilioni 130/- kwa umeme vijijini.


UMOJA wa Ulaya (EU) umetoa Euro milioni 50 (takribani Sh bilioni 130) kwa ajili ya miradi ya usambazaji wa umeme vijijini inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Makubaliano ya msaada huo yalisainiwa Dar es Salaam jana kati ya EU ikiwakilishwa na Kamishna wa Maendeleo, Neven Mimica na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Fedha na Mipango ikiwakilishwa na Katibu Mkuu wake, Dotto James. Kamishna Msaidizi anayeshughulikia Nishati Jadidifu, Edward Ishengoma aliiwakilisha Wizara ya Nishati.
Akizungumza kabla ya kusaini makubaliano hayo, Katibu Mkuu James alisema kiasi hicho cha fedha ni sehemu ya awali ya kiasi cha Euro milioni 180 zilizotolewa kwa ajili ya kuboresha sekta ya nishati na kufafanua kuwa fedha hizo zitatolewa katika awamu mbalimbali.
Alisema kati ya Euro milioni 180, Euro milioni 90 zitatumika kwa ajili ya mpango wa kusambaza umeme vijijini kupitia REA na nyingine Euro milioni 90 zitatumika kwa ajili ya kuboresha sekta ya nishati kupitia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) pamoja na REA.
Aliongeza kuwa msaada huo usio na masharti ni moja ya mikakati ya EU kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli, katika usambazaji wa umeme vijijini.
Aliishukuru EU kwa msaada huo na kusisitiza kuwa serikali itautumia msaada huo katika kuhakikisha kuwa vijiji vyote Tanzania vinapata umeme ifikapo mwaka 2020. Awali akielezea mafanikio ya REA, Katibu Mkuu alisema wakati REA inaanzishwa mwaka 2008, asilimia mbili tu ya vijiji vyote vilikuwa vinapata umeme, lakini hadi kufikia Desemba, 2016 ni asilimia 49.3 wananchi waishio vijijini wanapata umeme.
Aliongeza kuwa mwaka 2008, asilimia 10 ya wananchi kitaifa walikuwa wanapata umeme, lakini hadi kufikia Desemba, 2016, asilimia 67.5 wanapata umeme wa uhakika. “Mafanikio haya ni makubwa na ninaamini kupitia msaada huu na ongezeko la kasi ya usambazaji wa umeme vijijini, ifikapo mwaka 2020 vijiji vyote nchini Tanzania vitakuwa na umeme wa uhakika na kupelekea kwenda kwenye uchumi wa viwanda,” alibainisha Katibu Mkuu Hazina.
Naye Kamishna wa Maendeleo wa Umoja wa Ulaya, Mimica alisema umoja huo unatambua juhudi zinazofanywa na serikali kupitia Wizara ya Nishati katika usambazaji wa umeme vijijini hivyo wapo tayari kuisaidia itimize malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa yenye lengo la kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.
Mimica alisema nishati ya umeme ni muhimu hususan katika maeneo ya vijijini kwa kuwa inachangia uboreshaji wa huduma za jamii kama shule, vituo vya afya, hospitali, viwanda vidogo vidogo na kilimo. Alisema kupatikana kwa umeme wa uhakika vijijini kutawezesha ongezeko la ajira kwa kuwa wananchi watajiajiri kwa kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya kusindika mazao.
@habari toka habari leo

No comments:

Featured post

MASIKINI WEEE!!!!! KICHANGA CHA SIKU MOJA CHAOKOTWA KATIKA KIWANJA CHA MPIRA AZIMIO

Na;Ezelina Yuda Mtoto mchanga mwenye jinsia ya Kike anayekadiriwa kuwa wa siku 1 ameokotwa akiwa hai kandokando ya uwanja wa azimio  ...