Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar (SMZ) imesema sababu kuu inayochangia miradi mikubwa ya maendeleo
kushindwa kutekelezeka inatokana na wawekezaji wenyewe kutofuata masharti
yanayohitajika kwa mujibu wa sheria.
Waziri wa Nchi Afisi
ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Issa Haji Ussi ‘Gavu’
amsema Serikali ya Zanzibar imekuwa ikijitahidi kujitangaza ndani na nje ya
nchi kwa lengo la kutangaza fursa zilizopo.
Gavu amesema kuwa
juhudi zao hizo zimekuwa zikizaa matunda kwa kiasi fulani kwa wawekezaji
mbalimbali kujitokeza kwa lengo la kuanzisha miradi ya maendeleo ambayo
itasaidia jamii ya Wazanzibar kutatua tatizo la ajira.
Gavu ametaja baadhi
ya taratibu wanazokosea wawekezaji hao kwamba ni ukosefu wa fedha za kutosha
katika uendeshaji wa mradi ,ukosefu wa watendaji imara katika mradi husika
pamoja na kutofuata taratibu za usajili.
“Sisi kama
Serikali tupo tayari kuona miradi mingi ya maendeleo inafanyika Zanzibar ila
wao wenyewe wawekezaji wanaonekana ni wagumu kufuata taratibu zilizopo,” amesema
Gavu.
Gavu amesema kuwa
pamoja na matatizo hayo yote lakini Serikali itaendelea kutoa kila aina ya
ushirikiano wake kwa kila mwekezaji ambaye atakuwa tayari kuja Zanzibar.
“Mbali ya hali
hiyo lakini pia tunaandaa mipango kabambe ambayo tunadhani inaweza kusaidia
kuwavutia hawa wawekezaji ikiwamo wale wa kizalendo ili waone kuna umuhimu
mkubwa wa kuwekeza Zanzibar bila ya kuwepo kwa mgongano wa masharti yaliopo”
amesema Gavu.
No comments:
Post a Comment