Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Stephen Kebwe |
MKURUGENZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero ameagizwa
kumsimamisha kazi Mtendaji wa Kijiji cha Masalawe pamoja na Mtendaji wa kata ya
Luale, tarafa ya Mgeta kwa kushindwa kusimamia majukumu ya kazi zao.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe
Stephen Kebwe baada ya kumaliza operesheni maalumu kukabiliana na kilimo cha
bangi kilichoshamiri katika eneo hilo. Mashamba ya bangi ya zaidi ya ekari 25
yalikutwa kando kando ya mto Mgeta ambayo yalikuwa yanafanyika kwa njia ya
umwagiliaji. Watu kadhaa kutoka vitongoji vya Tagata, Kwa Kododo na Lufuna
vilivyopo kijiji cha Masalawe, kata ya Luale, tarafa ya Mgeta, wilayani Mvomero
walikamatwa kwa kuhusika na kilimo hicho.
Alisema ni jambo la kushangaza kuona kilimo cha bangi inaendeshwa
bila kificho wakati viongozi na Mtendaji wa serikali ya kijiji pamoja na kata
ambao wamepewa dhamana ya kusimamia ulinzi, amani na ustawi wa jamii,
wameshindwa kuchukua hatua kwa wananchi wenye kulima bangi hadi mkoa kuendesha
operesheni ya uteketezaji.
“Katibu Tawala wa wilaya ya Mvomero pamoja na DED (mkurugenzi)
nakuagiza uwasimamishe kazi mara moja watendaji hawa wa kijiji cha Masalawe
pamoja na wa kata ya Luale, wameshindwa kufichua uhalifu wa kilimo haramu cha
bangi,” alisema Dk Kebwe. Pia aliagiza uchunguzi ufanywe kwa viongozi hao wa
kijiji na kata kuona kama na wao wanashiriki katika kilimo hicho.
Kwa upande wake Kamishina wa Operesheni wa Mamlaka ya Kudhibiti na
Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Mihayo Msikhela, aliwapongeza wananchi wa
kijiji cha Masawale kutokana na kuonesha kwao moyo wa uzalendo kujitokeza kwa
wingi kushiriki na askari kuteketeza bangi iliyolimwa mashambani. “Sijawahi
kuona sehemu nyingine nchini tulikopita kufanya operesheni hizi wananchi
kujitokeza kuunga mkono kwa kushirikiana kwenye kazi hii.
Lakini wa eneo hili wamejitokeza kushiriki kwa kusaidiana na
askari kuteketeza bangi mashambani, hawa ni watu wema na wanachukizwa na jambo
hili na wangekuwa ni waharifu wasingejitokeza,” alisema Mihayo.
Wilaya ya
Mvomero imeonekana kuongoza kimkoa kwa maeneo yake mengi kuwa vinara kwa kilimo
cha bangi katika vijiji vya Kata ya Doma, tarafa ya Mlali, vijiji vya Tarafa ya
Mgeta na vijiji vya tarafa ya Mvomero na wilaya nyingine zinazofuatiwa ni
Kilosa na Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro.
No comments:
Post a Comment