MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewataka wadau
mbalimbali ikiwemo makampuni, na taasisi za watu binafsi kujitokeza na kujitoa
kwa hali na mali ili kuchangia zoezi la utoaji wa miguu ya bandia kwa watu
wenye uhitaji.
Makonda alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari
jana. Alisema kuwa mipango aliyokuwa ameweka ni ya miguu 200, lakini uhitaji wa
miguu hiyo bandia umeongezeka na kufikia idadi ya watu 650, ambao
walijiandikisha kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya mkoa wa Dar es Salaam.
Alisema, “Wapo waliokuwa mafundi rangi wazuri, madereva na
wafanyabiashara, lakini kazi zao nyingi zimekwamishwa na tatizo walilolipata la
kukosa mguu mmoja, ukimsaidia mtu kama huyo kupata mguu wa bandia itakuwa ni
rahisi kwake kuendelea na kazi zake za kila siku na hata kuwaongezea uwezo wa
kupata kipato kikubwa.”
Mkuu huyo alisema mbali na wale waliokuwa wamelengwa mwanzoni,
haikuwa vyema kuwarudisha wale waliokuwa wametoka kutoka mikoa mingine wakiwa
na uhitaji na tena tayari walishafanyiwa vipimo ili kubaini sehemu ya mguu
ulipokatwa.
Alisema, “Kuna ambao walitoka nje na ndani ya Dar es Salaam
waliofanyiwa vipimo kubaini kama kukatwa miguu yao inatokana na ajali au ni kwa
sababu ya ugonjwa kama wa kisukari ili kuweza kubaini ni aina gani ya mguu
utakaomfaa kwa sababu miguu ya bandia kwa wagonjwa wa kisukari ni tofauti.
“Miguu iliyokuwepo ilionekana kuwa haitawafaa, hivyo italazimika
watengenezewe miguu ambayo itakuwa laini na rafiki kwao, iliyopo ni ya wale
waliokatwa miguu kutokana na ajali”.
Mpaka sasa, CCBRT walikuwa wamechangia miguu 25 wakati msanii wa
muziki nchini, Mrisho Mpoto alishachangia miguu mitatu.
Hata hivyo, Makonda alisema kuwa Taasisi ya
Mifupa Muhimbili (MOI) imekubali kutengeneza miguu hiyo mingine, pamoja na Ajma
Othopedics Medical Service ambao wameunga mkono zoezi hilo.
No comments:
Post a Comment