Waziri Mkuuwa Tanzania, Kassim Majaliwa |
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka Watanzania wote wahakikishe
wanaboresha mshikamano wao pamoja na kuimarisha uzalendo kwa Taifa lao. Alitoa
kauli hiyo juzi jioni wakati akizungumza na wanafunzi wa Tanzania wanaosomea
udaktari nchini Cuba.
Waziri Mkuu yuko nchini Cuba kwa ajili ya ziara ya kikazi yenye
lengo la kudumisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili. Alisema uzalendo kwa
Taifa ni jambo muhimu.
“Uzalendo ni muhimu sana kwa sababu tumekosa fursa
nyingi za kimaendeleo kutokana na baadhi ya wananchi kutokuwa wazalendo kwa
Taifa lao,” alisema Majaliwa kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari
iliyotolewa na ofisi yake. Kutokana na hali hiyo, serikali inawasisitiza
wananchi kuwa wazalendo na washirikiane kuhakikisha fursa za kimaendeleo
zilizoko nchini zinaendelezwa.
Alisema serikali inatekeleza miradi mingi kwa lengo la kukuza
uchumi kutoka wa chini kwenda wa kati, ni vema wananchi wakashirikiana nayo ili
kufanikisha azma hiyo.
Pia Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwasihi wanafunzi
hao, kuzingatia sheria za nchini waliyoko pamoja na kukumbuka kurudi nyumbani
mara wamalizapo masomo yao. Alisema serikali inatambua uwepo wao wa kimasomo
nchini Cuba na kwamba inatarajia kupata mchango mkubwa kutoka kwao punde
wamalizapo masomo yao.
“Nawaomba msome kwa bidii na mfaulu mitihani yenu. Elimu yenu
iwasaidie katika ajira na muweze kurejesha mikopo mliyopewa na serikali ili
iwanufaishe wengine,” alisema. Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwataka
mabalozi wote wanaoiwakilisha Tanzania katika mataifa mbalimbali kuhakikisha
wanatangaza vivutio vya utalii.
Alisema Tanzania imejaaliwa kuwa na vivutio vingi vya utalii,
hivyo ni vema mabaloziwakavitangaza jambo ambalo litasaidia kuongeza idadi ya
watalii wanaokuja nchini. Miongoni mwa vivutio vya utalii vilivyoko nchini ni
pamoja na mlima Kilimanjaro, visiwa vya Zanzibar, mbuga mbalimbali zenye
wanyama wa aina tofauti tofauti.
Awali Mwenyekiti wa wanafunzi hao, Goodchance Tarimo
alimhakikishia Waziri Mkuu kwamba watarejea nyumbani baada ya kumaliza masomo
yao nchini humo. Alisema wao wana imani kubwa na serikali na wanaunga mkono
jitihada zinazofanywa na viongozi wa Taifa kwa lengo la kuboresha maendeleo
pamoja na kukuza uchumi.
“Tunapongeza jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano
katika kujenga uchumi wa viwanda, mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi na ujenzi
wa miundombinu ya kisasa,” alieleza.
No comments:
Post a Comment