Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali mstaafu Emmanuel Maganga |
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali mstaafu Emmanuel Maganga aliongoza uzinduzi rasmi wa kazi hiyo, na kueleza kuwa takribani wakimbizi 12,000 wanatarajia kurudishwa kwao hadi kufikia Desemba 31, mwaka huu ikiwa ni awamu ya kwanza ya utekelezaji wa kazi hiyo. Maganga alisema kwa sasa wakimbizi hao watarejeshwa kwa hiari kulingana na mikataba ya kimataifa ya kuhifadhi na kurejeshea kwao wakimbizi ambayo Tanzania imeridhia.
Wakimbizi 300 wanatarajia kurudishwa kila wiki, kati ya wakimbizi wa Burundi 400,000, wanaohifadhiwa kwenye kambi za Nduta (Kibondo), Mtendeli (Kakonko) na Nyarugusu wilayani Kasulu. Awali, Mratibu wa Idara ya Wakimbizi Kanda ya Magharibi katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tanzania, Tonny Laizer alisema kwa sasa wakimbizi watakaorejeshwa ni wale watakaojitokeza na kuandikishwa kwa hiari kurudi kwao.
Laizer alisema awamu ya pili itafanyika kwa uhamasishaji kwa viongozi wa Serikali ya Burundi kutembelea makambi kuzungumza na wakimbizi hao sanjali na baadhi ya wakimbizi kupelekwa kutembelea Burundi kuona hali ya amani na usalama iliyopo humo ili kuwashawishi wenzao kujiandikisha kurudi nchini mwao kwa hiari.
Makamu Waziri wa Mambo ya Ndani wa Burundi, Terence Ntahiraja alinukuu maneno aliyotoa Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi, Julai 19, mwaka huu Ngara mkoani Kagera nchini Tanzania kuwa Burundi ina amani ya uhakika na watu hao hawana sababu ya kuishi uhamishoni kama wakimbizi. Ntahiraja alisema baadhi ya wakimbizi ambao hawako tayari kurudi kwa madai ya hali ya amani haijatengemaa nchini humo, wanayo fursa kwenda kutembea kuona hali halisi.
No comments:
Post a Comment