Sunday, 4 February 2018

Askofu KKKT awaomba msamaha washarika wa Kanisa Kuu la Mtwara


Askofu KKKT awaomba msamaha waumini








Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kusini Mashariki, Dk Lucas Mbedule akiwa amelala katika mlango wa kanisa kuu la KKKT Mtwara (Jumapili) kabla ya kuomba msamaha. 
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kusini Mashariki, Lucas Mbedule amewaomba msamaha washarika wa Kanisa Kuu la Mtwara ili wasiliumize kanisa.
Amewataka kumaliza tofauti zao na kukutana katika ibada wakiwa na mioyo minyenyekevu kumwomba Mungu.
Baadhi ya waumini wa kanisa hilo wamekuwa na mgogoro wakimpinga askofu huyo kwa takriban miaka miwili.
Waumini hao wamemwomba Askofu Mkuu wa KKKT, Fredrick Shoo kwenda kuzungumza nao na kuunda tume ya uchunguzi.
Agosti 28,2016 baadhi ya waumini na wazee wa kanisa waliingia katika ibada wakiwa na mabango yaliyokuwa na ujumbe wa kumpinga askofu huyo kwa tuhuma za kukiuka katiba, unyanyasaji wa watumishi na ubadhirifu wa fedha za usharika na dayosisi.
Umoja wa wazee ulitoa tamko kumwomba mkuu wa kanisa kufanya uchunguzi.
Akizungumza wakati wa ibada leo Februari 4,2018, Dk Mbedule amewaomba wote aliowakosea wamsamehe, awali akiingia kanisani alilala kifudifudi mlangoni na kusali.
Amesema watakapoweka vizuri utaratibu, Dk Shoo atakwenda kuwasalimia na kuzungumza nao kwa kuwa mazungumzo yanaruhusiwa lakini yasiharibu utaratibu wa ibada.
“Nimewakosea mengi siwezi kuhesabu kabisa, mimi ni mwenye dhambi kabisa kabisa sistahili kabisa. Naomba mnisamehe tusilitese kanisa, kuna jambo njoo uniambie hakuna ambaye nimemkataza awe mzee wa kanisa, mchungaji au yeyote  hakuna ambaye nimemfungia mlango,” amesema Dk Mbedule.
Amesema, “Moyo wangu uko tofauti na sura yangu, naomba nirudie tena tofauti ndogo za sisi za kibinadamu, sisi si malaika zisitufanye tulitese kanisa wala kuliingiza katika gharama kubwa, ukiniambia nimekosa nitasema na kama ni kujieleza nitajieleza, narudia tena wale wote waliojikwaa na mimi kwa kuwatazama au kwa kusema naomba unisamehe tutazame mbele, mimi sijaumbwa kama malaika nimeumbwa kama binadamu wengine yeyote anayekosa kwa kusema, anayekosa kwa kuwaza au kutenda.
Mimi si mtakatifu hizi gwanda (akionyesha mavazi ya kiaskofu aliyovaa) mmenipa ninyi kwa njia ya vyombo vya dayosisi.”
Kabla ya kuomba msamaha jana, baadhi ya  waumini wa kanisa hilo walionekana kwenda kinyume cha mwongozo wa ibada na hata kujikuta wakipishana katika kuimba.
Awali, akihubiri Mkuu wa Jimbo la KKKT Pwani, Mchungaji Zacharia Lyakunge alisisitiza kudumisha amani kwa kanisa na Taifa kwa jumla.
“Amani ni kitu cha thamani mno, amani ni uzima wetu, amani ni baraka zetu, kwenye ndoa zetu kama hakuna amani hakuna furaha ya ndoa; kwenye kazi zetu kama hakuna amani hatutaiona furaha ya kazi; kwenye taasisi, jamii kama hakuna amani hakuna chochote tutakachokifanya.
 Tukitaka baraka na mafanikio katika maisha yetu tumng’ang’anie huyu Yesu, ukiishi na Yesu hutahesabu mabaya, hutakumbuka mabaya, ukiishi na Yesu utakumbuka zuri alilolileta duniani,” amesema Mchungaji Lyakunge.
Chanzo:Mwananchi
#Changia Damu Okoa Taifa

No comments:

Featured post

MASIKINI WEEE!!!!! KICHANGA CHA SIKU MOJA CHAOKOTWA KATIKA KIWANJA CHA MPIRA AZIMIO

Na;Ezelina Yuda Mtoto mchanga mwenye jinsia ya Kike anayekadiriwa kuwa wa siku 1 ameokotwa akiwa hai kandokando ya uwanja wa azimio  ...