Na Ikulu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.
John Pombe Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Kampuni ya
Barrick Gold Corporation ambayo ni mmiliki mkubwa wa kampuni ya Acacia Mining
Limited Prof. John L. Thornton na kukubaliana kuwa kampuni hiyo ipo tayari
kufanya mazungumzo na Serikali ya Tanzania ili kulipa fedha ambazo Tanzania
imezipoteza kutokana na kampuni hiyo kuendesha shughuli zake hapa nchini.
Prof. John L. Thornton ambaye amesafiri
kwa ndege binafsi kutoka nchini Canada hadi Tanzania amekutana na Mhe. Rais
Magufuli leo Juni 14, 2017 Ikulu Jijini Dar es Salaam na mazungumzo yao
yamehudhuriwa na Balozi wa Canada hapa nchini Mhe. Ian Myles na Waziri wa
Sheria na Katiba Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi.
Baada ya Mazungumzo hayo Prof. John L.
Thornton amesema kampuni yake ipo tayari kufanya mazungumzo na Tanzania
yatakayozingatia maslahi ya pande zote mbili na pia ipo tayari kulipa fedha
zote ambazo inapaswa kulipa kwa Tanzania.
Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli
amesema Serikali inakaribisha mazungumzo hayo na itaunda jopo la wataalamu
watakaofanya majadiliano na kampuni ya Barrick Gold Corporation ili kufikia
makubaliano ya kulipwa fedha zinazodaiwa na namna kampuni hiyo itakavyoendesha
shughuli zake nchini maslahi ya pande zote mbili.
Mhe. Rais Magufuli amesema pamoja na
kukubali kulipa fedha zinazodaiwa Prof. John L. Thornton amekubali kushirikiana
na Tanzania kujenga mtambo wa kuchenjulia dhahabu (smelter) hapa nchini.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli
amevionya vyombo vya habari vinavyowataja Marais wastaafu Mhe. Benjamin William
Mkapa na Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete na kuwahusisha na taarifa za kamati mbili
za uchunguzi wa madini yaliyo katika makontena yenye mchanga wa madini
(Makinikia) ambao ripoti zimekabidhiwa kwake na kamati hizo.
“Nimesoma
ripoti zote mbili hakuna mahali ambapo Mzee Mkapa na Mzee Kikwete wametajwa,
vyombo vya habari viache kuwachafua hawa wazee, wamefanya kazi kubwa ya
kulitumikia Taifa letu, viwaache wapumzike” amesema Mhe. Rais Magufuli.
No comments:
Post a Comment