Friday, 16 June 2017

WATOTO WA KIKE WAKABILIWA NA UKATILI WA KINGONO

Wasichana Nchini Tanzania wanakumbana na changamoto mbalimbali  katika  makuzi yao ikiwemo ukatili wa kingono hususani mimba za utotoni kabla ya kufikia miaka 18.
Akiongea na vyombo vya habari mjini Dodoma katika Kongamano la maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika  Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamis Kigwangalla amesema takwimu zinaonesha kuwa asilimia 51.4 ya idadi ya watoto ni wasichana pia takwimu zinaonesha kuwa mtoto wa kike 1 kati ya 3 na wa kiume 1 kati ya 7 anakumbana na ukatili wa kingono kabla ya kufikia umri wa miaka 18.
Dk. Kigwangala aidha amesema kuwa takwimu zinaonyesha kuwa uwiano wa wasichana na wavulana katika elimu ya msingi na sekondari ni uwiano wa moja kwa moja (1:1), ingawa idadi ya wasichana hupungua kutokana na changamoto wanazokutana nazo ikiwa ni pamoja na mimba na ndoa za utotoni.
“Kwa mujibu wa Takwimu za Elimu kwa Mwaka 2012 hadi 2016  idadi ya watoto wa kike walioacha shule kutokana na  kupata ujauzito  ni 610 (mwaka 2011), 2,433 (mwaka 2012), 247 (mwaka 2013), 265 (mwaka 2014 na 251 (mwaka 2015). Serikali inaendelea kukabiliana na changamoto hizi ili kuhakikisha wanafunzi wa kike wanapata elimu hadi kufikia ngazi ya vyuo,” alisema Dk. Kigwangalla’.
Ametaja madhumuni ya kuadhimisha siku hii kuwa ni  kutoa fursa kwa wazazi, walezi na wadau wote wa haki za mtoto kutafakari changamoto zinazowakabili kama vile ukatili katika Bara letu la Afrika kwa lengo la kuzipatia ufumbuzi.
Maadhimisho ya siku hii hapa Nchini hutumika  kutathmini changamoto zinazowakabili watoto katika upatikanaji wa haki, malezi, elimu, afya na ulinzi kwa lengo la kuboresha huduma hizi ili ziweze kumfikia kila Mtoto nchini.
Aidha amesema siku siku hii inatumika kuwakumbusha na kuwahimiza wazazi, walezi na jamii kwa ujumla  kuzingatia jukumu lao la msingi la utoaji haki na huduma za ustawi wa Mtoto bila ubaguzi wowote. Siku hii hutumika kufanya ushawishi kwa wadau kuwekeza katika maeneo ya malezi, afya, elimu, ulinzi kwa lengo la kuunga mkono jitihada za Serikali za kumwendeleza Mtoto.
Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yametokana na Azimio lililopitishwa na iliyokuwa Jumuiya ya Nchi Huru za Umoja wa Afrika (OAU) kwa ajili ya kukumbuka mauaji ya watoto wa shule  yaliyofanyika  katika kitongoji cha Soweto, nchini Afrika ya Kusini tarehe 16 Juni 1976.
Aidha Katika tukio hilo la kusikitisha, inakadiriwa kuwa takribani watoto 700 waliuawa kikatili wakiwa kwenye harakati za kupinga mifumo ya elimu ya kibaguzi iliyokuwa inataolewa na serikali ya makaburu.

No comments:

Featured post

MASIKINI WEEE!!!!! KICHANGA CHA SIKU MOJA CHAOKOTWA KATIKA KIWANJA CHA MPIRA AZIMIO

Na;Ezelina Yuda Mtoto mchanga mwenye jinsia ya Kike anayekadiriwa kuwa wa siku 1 ameokotwa akiwa hai kandokando ya uwanja wa azimio  ...