Tuesday, 11 July 2017

JPM ASHTUKIA UBADHIRIFU WA SH.42 BILIONI PEMBEJEO ZA KILIMO.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameshtukia ubadhirifu wa Sh42 bilioni kwenye fedha za pembejeo za kilimo baada ya kuelezwa kwamba Serikali inadaiwa Sh50 bilioni, lakini baada ya uhakiki kwenye mikoa 11 ilibainika madai halali ni Sh8 bilioni.
Alisema Serikali itafanya uhakiki nchi nzima kwenye fedha za ruzuku na pembejeo za kilimo, baada ya kugundua njama za kuongeza majina ya watu wasiostahiki kupata fedha hizo wakiwamo marehemu. Rais Magufuli alisema hayo jana wilayani Chato mkoani Geita kwenye hafla ya kukabidhi nyumba 50 kati ya 450, zilizojengwa na Taasisi ya Mkapa.

Nyumba zilizokabidhiwa, 20 ziko Geita, 10 ziko Kagera na 20 ziko Simiyu. Alisisitiza kwamba tatizo la ubadhirifu wa fedha za umma limeenea kwenye halmashauri zote nchini. Rais Magufuli alizitaka halmashauri hizo kuwa na nidhamu katika matumizi ya fedha za Watanzania kwa kuhakikisha zinafanya kazi katika maeneo yaliyokusudiwa. Mkuu huyo wa nchi aliwataka viongozi wa Serikali kufanya kazi kwa uzalendo na kusimamia vizuri fedha. Alisema mgogoro mkubwa upo kwenye fedha za ruzuku ya pembejeo za kilimo na watu waliokufa nao wameorodheshwa kuzipata.
 
“Na wanaohusika wengine ni viongozi, viongozi wa ndani ya Serikali na viongozi ndani ya halmashauri. Hata hapa Chato, sitaki nizungumzie sana, sifahamu kama kesi imekwisha, fedha za pembejeo zililiwa Sh1.5 bilioni,” alisema Rais Magufuli. Alisema siku moja alimuuliza mama yake “mama mbona nawe uko kwenye orodha, ulichukua vocha?” yeye akafikiri vocha ni ile ambayo wanamnunulia wajukuu zake kuweka kwenye simu. Alisisitiza kwamba mchezo huo uko karibu kila mahali.
 “Tunafanya auditing ya Tanzania nzima, nayo tutayasema hadharani. Pamekuwa na hewa nyingi, mara uhangaike na hewa ya wafanyakazi, hewa ya watu wa elimu feki, hewa ya Tasaf lakini niwaombe viongozi wote Tanzania, tushirikiane,” alisema Rais Magufuli. Aliwataka viongozi kuiga mfano wa Taasisi ya Mkapa katika kutekeleza miradi kwenye halmashauri zao. Aliwapongeza wakandarasi kwa kutekeleza ujenzi wa nyumba hizo ndani ya wakati na kwa ubora.

Rais Magufuli alisisitiza kwamba ataendelea kuwa upande wa Watanzania hasa wale maskini, ndiyo maana Serikali imepunguza bei ya dawa na ushuru wa mazao kwa wakulima. “Mwaka huu kwa mfano, kupitia Bunge, tumetoa na kufuta tozo zaidi ya 80 kwenye kilimo, tozo zaidi ya saba kwenye mifugo na tozo zaidi ya tano kwenye uvuvi. Kwenye kilimo ilikuwa ukitoka na gunia moja lazima ulipe ushuru lakini sasa ukitoka na tani moja kutoka wilaya moja kwenda nyingine utapita bure,” alisema Rais Magufuli.

 Aliwataka wananchi waendelee kusimamia rasilimali za Taifa kwa manufaa yao na yeye kama kiongozi yuko mstari wa mbele kuzilinda rasilimali za nchi ziwanufaishe wote. “Ninalishukuru Bunge kwa kufanya mabadililiko kwenye sheria mbalimbali.
 Limefanya mabadiliko na siku wamemaliza waliniletea, siku hiyo hiyo tarehe 5 nikasaini, na keshokutwa wataanza mazungumzo na wale wale waliokuwa wanatuchukulia,” alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli alisisitiza msimamo wake, kwamba wanafunzi watakaopata mimba hawataruhusiwa kurudi shuleni na taasisi zinazowatetea waige mfano wa Taasisi ya Mkapa kwa kuleta maendeleo badala ya kupiga kelele.

 “Taasisi zote ziige mfano wa Taasisi ya Mzee Mkapa. Tunaviona vitu ambavyo ni tangible (vitu vinavyoonekana), siyo taasisi za kuonekana kwenye majukwaa tu, kila siku wanahubiri majukwaani tu, wameletewa hela nyingi, impact (matokeo) huku hakuna.
“Hata kwenye familia yangu wapo waliopata mimba. Yupo mtoto wa mdogo wangu alipata mimba wala hakubakwa, akazaa katoto akakaita John, nimekaa baada ya muda akazaa kengine akakaita Samia. Tunae, wala hakubakwa. Ni ukweli ukweli ukweli!” alisema Rais Magufuli huku wananchi wakicheka. Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa aliyekuwa mgeni rasmi, taasisi yake ndiyo iliyofanikisha ujenzi wa nyumba 450 kati ya 480 huku ujenzi wa nyumba nyingine 30 unatarajiwa kukamilika mwezi ujao.

 Mkapa alimpongeza Rais Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya. “Watu wananipongeza mimi kwa kumuibua Rais Magufuli, naomba pongezi hizo zirudi kwake mwenyewe kwa sababu amewafanyia kazi nzuri. Ushirikiano wenu na upendo wenu kwake ndiyo vilivyomfanya ang’are ndani ya chama. Tumshukuru Mungu kwa kutupatia kijana wetu huyu,” alisema Mkapa. Aliwataka wataalamu wa afya wazingatie maadili ya kazi yao, kwa kuheshimu utu wa Watanzania ambao wengi wao ni maskini na wanahitaji msaada wao.

“Wakati tunatekeleza haya, ni vema kukumbuka maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliyosema ‘ili kujiletea maendeleo hatuna budi kupambana na maadui watatu ambao ni umaskini, ujinga na maradhi’. Hiyo ndiyo kazi tunayoifanya kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo,” alisema Mkapa. Awali, akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema wizara yake inafuata maelekezo ya Rais Magufuli ikiwa ni pamoja na kupunguza bei ya dawa. Mwalimu alisema sasa Serikali itakuwa inanunua dawa kutoka viwandani na punguzo la bei litakuwa la asilimia 15 kwa dawa muhimu 101 kati ya 135.

 Alisema Serikali inaendelea kuongeza kasi ya kuhakikisha hakuna mgonjwa atakayepelekwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu, na kwamba idadi imepungua kutoka wagonjwa 553 waliopelekwa nje mwaka jana mpaka wagonjwa 357 mwaka huu. Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Mkapa, Dk Ellen Mkondya-Senkoro alisema taasisi hiyo imekuwa ikipata ushirikiano wa Serikali katika kipindi cha miaka 11 tangu kuanzishwa kwake.
 Alisema katika kipindi hicho, Taasisi ya Mkapa imeweza kujenga nyumba 450 na kusomesha wataalamu wa afya 949 ambao kati yao, wanafunzi 104 watakwenda mikoa ya Geita, Kagera na Simiyu. Naye Balozi wa Japan nchini, Masaharu Yoshida alisema nchi yake inashirikiana na Serikali ya Tanzania katika miradi mbalimbali ya maendeleo ukiwamo mradi wa ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza mafuta ya alizeti ambacho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha lita 700 za mafuta kwa siku. Yoshida alisema wamefadhili ujenzi wa kiwanda hicho ili kuunga mkono jitihada za Rais Magufuli za kujenga viwanda.
 Alibainisha kuwa miradi mingine ni ujenzi wa barabara ya juu ya Tazara, mradi wa umeme wa Kinyerezi na barabara mbalimbali.

No comments:

Featured post

MASIKINI WEEE!!!!! KICHANGA CHA SIKU MOJA CHAOKOTWA KATIKA KIWANJA CHA MPIRA AZIMIO

Na;Ezelina Yuda Mtoto mchanga mwenye jinsia ya Kike anayekadiriwa kuwa wa siku 1 ameokotwa akiwa hai kandokando ya uwanja wa azimio  ...