Tuesday, 25 July 2017

MIRADI YAIPAISHA MKOA WA TABORA.

Raisi John Pombe Magufuli

RAIS John Magufuli ameweka jiwe la msingi katika miradi mikubwa miwili ambayo ni mradi wa maji kutoka Ziwa Viktoria kwenda miji ya Tabora, Igunga na Nzega, na mradi wa ukarabati na upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Tabora, na kufungua barabara mbili za Tabora – Nyahua na Tabora – Puge – Nzega, miradi ambayo ikikamilika, itabadilisha kwa kiasi kikubwa maisha ya wakazi wa Tabora na maeneo jirani.

 Mradi wa maji kutoka Ziwa Viktoria utatekelezwa kwa muda wa miezi 30 kwa gharama ya Sh bilioni 600 ikiwa ni mkopo kutoka Serikali ya India na utazalisha takribani lita milioni 80 za maji kwa siku kwa ajili ya wakazi wa Tabora ambao kwa sasa wanahitaji lita milioni 36 na pia utamaliza tatizo la maji katika miji ya Igunga, Nzega, Tinde, sehemu ya Wilaya ya Uyui, Shinyanga Vijijini na vijiji 89 vilivyo kando ya mabomba ya mradi huo. “Waziri Mkuu wa India ametoa Sh bilioni 601 kwa ajili ya kusadia usambazaji wa maji nchini hususani mkoani Tabora. Mradi huu ukikamilika utawanufaisha watu takriban milioni mbili,” alieleza Rais Magufuli wakati akizungumza na maelfu ya wananchi katika mkutano wa hadhara kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi jana jioni.

 Dk Magufulia alisema usambazaji wa maji mkoani humo ni matokeo ya ahadi ya Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi aliyoitoa mwaka jana alipofanya ziara nchini. Pia alimuomba Balozi wa India nchini, Sandeep Arya kumfikishia shukrani zake na za Watanzania kwa Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi kwa kutoa mkopo wa Sh bilioni 600 kwa ajili ya kufanikisha mradi huo wa maji na pia kutoa fedha nyingine Sh trilioni 1.2 kwa ajili ya kutekeleza miradi mingine 17 nchini.

 Dk Magufuli amemtaka mkandarasi anayejenga mradi wa maji kutoka ziwa Viktoria kuharakisha kazi hiyo na kuikamilisha kabla ya miezi 30 ili wananchi wa Tabora na maeneo yanayosubiri maji ya mradi huo waanze kunufaika mapema. Kwa mujibu wa hotuba ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji Bungeni kwa mwaka 2017/18, serikali imejipanga kuwapatia huduma ya maji wakazi wa miji ya Tabora, Igunga, Uyui, Nzega, Tinde na Sikonge pamoja na vijiji 89 vilivyopo kwenye eneo la kilometa 12 kutoka bomba kuu la mradi wa Kashwasa.

 “Mradi ni wa malengo ya muda mrefu ya kuwapatia huduma ya maji ya uhakika wananchi wapatao milioni 1.1. Mradi huu ukikamilika utaongeza hali ya upatikanaji wa maji katika Mji wa Tabora kutoka asilimia 80 hadi asilimia 100; Uyui (asilimia 30 hadi asilimia 100); Igunga (asilimia 62 hadi asilimia 100).

 “Nzega kutoka asilimia 58 hadi asilimia 100 na Mji wa Tinde kutoka asilimia 45 hadi asilimia 68. Awamu ya pili ya mradi itahusu kupeleka maji katika Mji wa Sikonge kutoka Ziwa Victoria,” alisema Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge alipowasilisha hotuba yake bungeni.

 Ili kuhakikisha wananchi wa Tabora wanapata maji safi na salama kwa haraka, Rais Magufuli alisema kwamba mradi huo umekabidhiwa kwa wakandarasi watatu ili ukamilike ndani ya muda wa miaka miwili na nusu. Kukamilika kwa mradi huo wa maji, siyo tu utawapatia wakazi hao zaidi ya milioni mbili maji safi na salama, lakini pia utawaepushia wananchi na maradhi yaliyokuwa yakiwasumbua kutokana na maji yasiyo salama kama vile kichocho, homa ya matumbo na kipindupindu.

Aidha, Rais Magufuli alifanya ufunguzi wa mradi wa ukarabati na upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Tabora, na kuiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kujenga jengo la abiria 500 badala ya jengo lililopo sasa la abiria 50.
 Pia amegiza urefu wa uwanja uongezwe hadi kufikia kilometa 2.5 badala ya kilometa 1.9 zilizopangwa ili ndege kubwa na ndogo ziweze kuutumia uwanja huo. Mradi wa ukarabati na upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Tabora unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu kuanzia sasa na ni miongoni mwa miradi inayotekelezwa kwa awamu tatu katika mikoa ya Kagera, Kigoma, Tabora na usanifu wa viwanja vingine 11 katika mikoa mbalimbali nchini kwa gharama ya Sh bilioni 69.7.

Imeelezwa kuwa uwanja huo kwa sasa unatumiwa na ndege zenye uwezo wa kubeba abiria hadi 70, lakini kukamilika kwa upanuzi wa uwanja huo na kufungwa taa, kutawezesha ndege kubwa zenye uwezo wa kubeba hadi abiria 150 kutua, lakini pia uwanja utakuwa ukitoa huduma kwa saa 24 tofauti na sasa. Imeelezwa kuwa maboresho hayo yataongeza ufanisi katika huduma kwa kuwa usafiri wa ndege utakuwa wa uhakika na gharama zinaweza kushuka kwa kiasi kikubwa.

 Mradi mwingine ulizinduliwa na Rais Magufuli jana katika siku yake ya mwisho ya ziara yake mkoani Tabora ni Nzega – Tabora na Nyahua – Chaya. Dk Magufuli alisema kwamba serikali itakuwa imetumia zaidi ya Sh bilioni 600 kukamilisha miradi ya barabara mkoani Tabora, ambayo pia ilimshuhudia akizindua barabara ya Kaliua – Kazilambwa, Urambo – Tabora, na kuagiza barabara ya Kaliua - Urambo kuanza kujengwa kwa kiwango cha lami ndani ya mwezi mmoja.

Barabara ya lami ya Tabora – Nyahua yenye urefu wa kilometa 85 imejengwa kwa gharama ya Sh bilioni 123.773 na barabara ya Tabora – Puge – Nzega yenye urefu wa kilometa 114.9 imejengwa kwa gharama ya Sh bilioni 160.515, fedha zote zikiwa zimetolewa na Serikali ya Tanzania.

 Aidha, Rais Magufuli amewahakikishia wananchi wa Tabora kuwa serikali yake imejipanga kutekeleza ahadi alizotoa ikiwemo kujenga reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) itakayoanzia Dar es Salaam – Morogoro – Dodoma – Tabora hadi Kigoma ili kurahisisha usafiri na kukuza biashara ya ndani na nje ya nchi na amewataka wote waliojenga majengo katika hifadhi ya reli kujipanga kuondoa majengo yao kwa hiari kwa kuwa serikali haitawalipa fidia yoyote.

 Upanuzi wa uwanja huo wa ndege na ujenzi wa reli ya kisasa utazidi kuufanya Mkoa wa Tabora kuimarika kiuchumi na kufungua fursa za kiuchumi za wananchi wa mkoa huo na mikoa jirani pamoja na nchi jirani hasa zile za Maziwa Makuu. Leo ziara ya Rais Magufuli imeendelea mkoani Singida ambako amefungua mradi wa barabara ya Manyoni – Itigi yenye urefu wa kilometa 89.3.

No comments:

Featured post

MASIKINI WEEE!!!!! KICHANGA CHA SIKU MOJA CHAOKOTWA KATIKA KIWANJA CHA MPIRA AZIMIO

Na;Ezelina Yuda Mtoto mchanga mwenye jinsia ya Kike anayekadiriwa kuwa wa siku 1 ameokotwa akiwa hai kandokando ya uwanja wa azimio  ...