Ndoto za
wanandoa wengi wanapooana huwa ni kuishi pamoja hadi kifo kinapowatenganisha.
Vivyo hivyo, wazazi wao, ndugu na jamaa hupenda kushuhudia wanandoa hao
wakifanikiwa katika safari ya maisha yao ikiwamo kuwa na familia imara yenye
watoto wenye afya bora.
Hata hivyo, siyo
wanandoa wote hutimiza ndoto hizo. Kasi ya wanandoa nchini kupeana talaka
imeongezeka mara mbili ndani ya miaka sita ya hivi karibuni, jambo linalotishia
mustakabali wa ‘taasisi’ hiyo muhimu kwa maisha ya binadamu.
Utafiti wa kufuatilia
kaya Tanzania (National Panel Survey) wa mwaka 2014/15 uliofanywa na Ofisi ya
Taifa ya Takwimu (NBS) unaonyesha kuwa kiwango cha talaka kimeongezeka kutoka
asilimia 1.1 mwaka 2008/09 hadi asilimia 2.1 mwaka 2014/15.
Hii ina maana kuwa
kwa sasa kila watu 100 wenye umri wa kuoa au kuolewa waliopo nchini, wawili
wametalakiwa kutoka mmoja mwaka 2008/09. Ikumbukwe kuwa utafiti huo unabainisha
kuwa watu takriban 40 kwa kila 100 wanaopaswa kuoa au kuolewa bado hawajaingia
kwenye ndoa.
Mbali na talaka, kuna
wanandoa takriban wanne kwa kila 100 ambao wametengana, jambo linaloashiria
huenda nao wakatalikiana siku zijazo iwapo hawatapata suluhu ya kudumu ya
tofauti zao.
Kuvunjika kwa ndoa
hizo kunawaweka watoto katika maisha magumu ya kukosa mapenzi ya wazazi wote
wawili na hata baadhi yao kujikuta wakiingia mitaani kuwa ombaomba kutokana na
kukosa huduma stahiki za malezi.
Wataalamu wa masuala
ya saikolojia, takwimu na walimu wa dini wanaonya kuwa mwenendo huu ni hatari
kwa mustakabali wa Taifa ikizingatia kuwa ndoa ni moja ya taasisi muhimu za
kujenga upendo, amani na mshikamano.
Takwimu zinavyoeleza
Matokeo ya utafiti
huo uliochapishwa mwaka huu yanakwenda sanjari na yale ya Sensa ya Watu na
Makazi ya mwaka 2012 yaliyobainisha kuwa watu 715,447 walikuwa wametalikiwa
(sawa na watu watatu kwa kila 100) wenye umri wa kuoa au kuolewa.
Mikoa ya Kusini
Unguja, Mtwara, Mjini Magharibi, Lindi na Kaskazini Unguja inaongoza kwa
kiwango cha talaka huku kiwango kikiwa zaidi ya asilimia nne ambacho ni juu ya
wastani wa kitaifa wa asilimia tatu kwa takwimu za Sensa mwaka 2012.
Siyo wote
wanaotalakiana mahakamani hupeleka matamko ya talaka kwa Wakala wa Usajili,
Ufilisi na Udhamini (Rita) baada ya takwimu za wakala huo kuonyesha idadi ndogo
ya talaka, lakini mwenendo wake unapaa kwa kasi.
Pamoja na kuwa talaka
zilizosajiliwa ni chache, Rita inabainisha kuwa zinaongezeka mwaka hadi mwaka
kwa kuwa Dar es Salaam pekee zimeongezeka kutoka 106 mwaka 2014 hadi 149 mwaka
jana jambo linalosadifu hali halisi iliyotolewa na NBS.
Rita, WLAC
zinasemaje?
“Inawezekana kabisa
talaka ni nyingi kuliko takwimu zetu kwa kuwa wengi hawaji kusajili matamko ya
talaka kutoka mahakamani ili tuwapatie vyeti,” anasema Meneja wa Masoko, Habari
na Elimu kwa Umma wa Rita, Josephat Kimaro.
“Tumeanza mchakato wa
kuwasiliana na mahakama ili baada ya kutoa tu matamko ya talaka watuletee
takwimu zote ili tupate picha kamili.”
Taarifa za Rita
zinaonyesha kuwa baadhi ya ndoa zimedumu muda mfupi chini ya mwaka mmoja
ikiwamo iliyochukua miezi minane iliyojumuisha kipindi cha mashauriano,
kuendesha kesi mahakamani hadi kusajili tamko la talaka Rita. Sheria ya Ndoa ya
mwaka 1971 inaeleza kuwa tamko la kutengana au talaka hutakiwa kutolewa na
mahakama pekee baada ya kujiridhisha na sababu za wanandoa kufanya hivyo.
Kifungu cha 100 cha
sheria hiyo kinaeleza kuwa mahakama haiwezi kusikiliza shauri la talaka kwa
ndoa zenye umri chini ya miaka miwili na ili isikilize ni lazima ijiridhishe
kuwa kuna mmoja wa wanandoa anateseka kupindukia.
Kituo cha Msaada wa
Sheria kwa Wanawake (WLAC) kinaeleza katika kijitabu cha ufafanuzi kuhusu
sheria ya ndoa kuwa, “mazoea ya wanandoa kupeana talaka mitaani aidha kwa
maandishi au kwa mdomo, hizo si talaka kwa mujibu wa sheria ya ndoa.”
“Ni lazima talaka
itolewe na mahakama ili kila haki ya mwanandoa itamkwe bayana,” inaeleza sehemu
ya kitabu hicho ya WLAC kilichotolewa mwaka 2013.
Kauli za mwathirika
Mwananchi limebaini
kuwa ukosefu wa uaminifu na kubadilika tabia baina ya wanandoa ni miongoni mwa
sababu kuu zinazofanya wanandoa kutalikiana.
Esther (siyo jina
lake halisi) alitalikiana na mumewe mwaka jana baada ya kubaini kuwa alikuwa
amebadilika tabia ikilinganishwa na wakati wa uchumba.
“Zamani alikuwa
ananishirikisha kwa kila jambo, msikivu, mpole na mfanyakazi aliyeonekana kuwa
baba bora wa familia. Lakini baada ya kuoana alianza kuwa mkali hata kwa vitu
vidogo licha ya kumwambia kwa upole,” anasema Esther.
Esther (37) anaeleza
kuwa kabla ya kuachana na mumewe waliyeoana baada ya kufahamiana kwa miezi
tisa, aliwashirikisha wazee wa karibu, familia zao hadi viongozi wa dini lakini
bado mwanaume huyo ‘hakuambilika’ jambo lililosababisha waachane.
“Sikupenda
tutalikiane kwa kuwa tuna mtoto mmoja, lakini vitimbi vyake vilifanya maisha
yawe ya mateso wakati wote. Angalau kwa sasa napumua na nasikia ameshaoa mke
mwingine huenda huyo ndiye aliyekuwa akimsumbua,” anasema.
Viongozi wa dini
Viongozi wa dini
ambao hufungisha ndoa na kutatua matatizo yanayowakuta wanandoa wanasema
haishangazi kuona talaka zikiongezeka kutokana na kushuka kwa maadili miongoni
mwa wanandoa ikiwamo uwapo wa muda mfupi wa wachumba kufahamiana vyema.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Baraza Kuu la Kiislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh
Khamis Mataka anasema kuongezeka kwa talaka ni matokeo ya udhaifu katika
taasisi ya ndoa ambayo wahusika wake wanatakiwa wadumu kwa upendo na umoja hadi
kifo kinapowatenganisha.
“Kabla ya ndoa
unatakiwa uone uliyempata kuwa ana vigezo vinavyotakiwa ikiwamo kujiridhisha
tabia na familia yake, uwezo wa kijamii na kama anaweza kuwa mwanajamii,”
anasema.
“Bahati mbaya ndoa
nyingi kwa sasa ni matokeo ya kukurupuka. Unakuta mwanandoa hajui hata historia
ya mwenzie kitu wanachoangalia ni ana mali kiasi gani au anafanya kazi shirika
gani.”
Kuingia kwenye ndoa
wakati wanandoa wakiwa ‘vipofu’ wa historia ya kila mmoja, kwa mujibu wa Sheikh
Mataka kunafanya ndoa ianze kuyumba mara tabia halisi zitakapoanza kujitokeza
na kusababisha watalikiane.
Mbali na kutojua
historia, Padri wa Kanisa Katoliki, Festo Liheta wa Parokia ya Mtakatifu Kamili
ya Kiwalani jijini Dar es Salaam anaongeza kuwa kuongezeka kwa uelewa wa haki
za wanawake, kukua kwa kipato miongoni mwa wanandoa na matatizo ya unyumba
yanachangia ongezeko la talaka.
Padri Liheta anasema
kiutamaduni wanaume wanapenda kutawala, lakini kwa sasa wanawake wengi
wanazijua haki zao na hawataki zivunjwe kinyume na wenza wao ambao hawajafikia
katika uelewa huo. “Mambo ya kiuchumi yanachangia sana ndoa kuvunjika. Mtu
anavyokuwa na uwezo wa kifedha hawezi kukubali kunyanyasika kwa kuwa anaweza
kujitegemea tofauti na zamani ambapo akina mama walivumilia kutokana na kipato
duni,” anasema Padre Liheta ambaye alifanya utafiti kuhusu kuvunjika kwa ndoa
wakati akihitimu Shahada ya Uzamili.
Mbali na masuala ya
kipato, padri huyo anasema matatizo ya tendo la ndoa nayo yanachochea ukosefu
wa uaminifu hasa pale mmoja anaposhindwa kumridhisha mwenzake.
“Zamani tendo la ndoa
lilikuwa kwa ajili ya kuzaa tu, lakini kwa sasa ni pleasure (starehe) hivyo mtu
asiporidhika anaenda kutafuta nje. Hapa wanaume wanabidi wajitahidi
kuwaridhisha wake zao ili kumaliza mifarakano inayotokana na unyumba,” anasema.
Akifafanua jambo
hilo, Sheikh Mataka ambaye ni mwalimu wa dini ya Kiislamu anaeleza kisa cha
hivi karibuni alichosuluhisha kilichomhusisha kijana mmoja aliyemkuta mkewe
akifanya mawasiliano ya mara kwa mara na mwanaume aliyekuwa na uhusiano naye
miaka ya nyuma.
“Pamoja na kumuonya
hakusikia. Yule mwanaume anayewasiliana naye alimwambia kuwa ni mwanamke
aliyekuwa anamfuata na siyo yeye,” anasimulia Sheikh Mataka akitafsiri kesi
hiyo kama mfano wa wanandoa kukosa uaminifu.
NBS yatia neno
Talaka zinazoongezeka
kwa kasi haziathiri tu wanandoa husika, bali familia nzima ikiwamo zile
zilizozalisha wanandoa.
“Kuongezeka kwa
talaka kunahatarisha kuongezeka kwa familia za mzazi mmoja,” anasema Mtakwimu
Mwandamizi wa NBS, Abbasy Mlemba . “Watoto wanakosa haki ya kuishi na wazazi
wote wawili na hili litaongeza umaskini kwa watoto na kuwafanya wawe ombaomba
mitaani, watumikishwe kazi na kuongeza uhalifu na mimba za utotoni.”
Mwarobaini wa talaka
Ili kupunguza tatizo
la mifarakano ya awali, Padri Liheta anawasihi wachumba kupeana muda wa
kufahamiana vyema kabla ya ndoa ikiwamo kujua asili ya wenza hao, eneo
anapotoka kila mmoja, ukoo na wazazi kufahamiana.
Sheikh Mataka anasema
uchumi hauwezi kuwa sababu ya wanandoa kutalikiana hivyo watu wanaotaka kuoa au
kuolewa wanatakiwa kujitathmini vyema na kuwa na upendo na dhamira ya kweli ya
kuingia kwenye ndoa ikiwamo kuwa tayari kuhimili changamoto.
Serikali inasema kuwa
inafahamu suala hilo na imeshaanza kutekeleza mikakati ya kulipunguza ili
kutengeneza ustawi bora wa familia na Taifa.
Msemaji wa Wizara ya
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto upande wa maendeleo ya jamii, Erasto
Ching’oro anasema wamebaini kuwa mbali na madhara kwa familia, pia ukosefu wa
utulivu baina ya wanandoa unapunguza uzalishaji na kurudisha nyuma jitihada za
kuelekea nchi ya uchumi wa kati.
“Serikali inataka
watoto walelewe na wazazi wote wawili ili kuongeza usalama wao katika kila nyanja
ya maisha yao. Hivyo kwenye mpango kazi miaka mitano tumepanga kupunguza
kiwango cha talaka kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2021,” anasema Ching’oro.
Katika
mpango huo ulioanza kutekelezwa Julai mwaka huu hadi mwaka 2021, Ching’oro
anasema wanawashirikisha viongozi wa dini na kimila, asasi za kiraia na maofisa
ustawi na maendeleo ya jamii katika utoaji elimu ya uhusiano na ndoa ili
kupunguza talaka na ukatili wa wanawake na watoto.tasmini kutokagazeti la mwananchi.
No comments:
Post a Comment