Mwadhama kardinali Polycarp Pengo.
|
Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam limekabidhi kisima
chenye thamani ya Sh milioni 11.8 kwa serikali ili kutatua tatizo la maji
katika Mahabusu ya Watoto iliyopo Upanga jijini Dar es Salaam.
Akiongea katika hafla ya makabidhiano ya kisima hicho jana, Askofu
Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo alisema
lengo kuu la mchango wa kanisa katika ujenzi wa kisima hicho ni kuonesha kuwa
kanisa haliko mbali na serikali katika shughuli mbalimbali za ujenzi wa Taifa.
Alisema Kanisa Katoliki Tanzania linashirikiana na serikali katika juhudi zake
za kuwaletea wananchi maendeleo bila kujali itikadi za kidini, siasa au kabila
ili kusudi wanapotoka kwenye vituo hivyo watambue wamesaidiwa kutokana na
mapenzi mema ya kanisa hilo kwa watu wote.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy
Mwalimu alisema ujenzi wa kisima hicho utasaidia serikali kupunguza gharama ya
kulipia bili ya maji ambayo kwa mwezi mmoja serikali ilikuwa inalipa Sh 400,000
kwa ajili ya gereza hiyo.
Waziri Ummy alisema kutokana na ujenzi wa kisima hicho tatizo la
maji limekwisha kwa asilimia 100 kwa sababu kisima hicho kina uwezo wa
kuzalisha lita 5,000 kwa saa. Aidha alisema kuwa fedha ambazo zimeokolewa na
ujenzi wa kisima hicho, zitatumika kwa ajili ya kuwakatia Bima ya Afya watoto
wanaozuiliwa katika vituo hivyo ili kuwahakikishia upatikanaji wa matibabu.
Alisema ni muhimu kwa jamii kufahamu kuwa ni mahakama tu ndiyo yenye uwezo wa
kutoa amri ya watoto kuhifadhiwa katika mahabusu hiyo na siyo mtu au chombo
chochote kingine.
Waziri wa afya,maendeleo ya jamii,jinsia ,wazee na watoto mh. Ummy Mwalimu |
Waziri Ummy alimwambia Kardinali Pengo kuwa hapa nchini kuna
mahabusu tano ambazo ni Mahabusu ya Watoto Dar es Salaam (Upanga), Mahabusu ya
Watoto Tanga, Mahabusu ya Watoto Moshi, Mahabusu ya Watoto Arusha na Mahabusu
ya watoto Mbeya.
Alizitaja huduma zinazotolewa na wizara yake kwa watoto walioko
kwenye mahabusu hizo kuwa ziko za aina tatu ambazo ni uhifadhi na utunzaji wa
watoto, huduma za maadilisho kwa watoto ambao tayari mahakama imewahukumu, na
huduma za kijamii za marekebisho ya tabia kwa watoto waliokinzana na Sheria.
Mkurugenzi wa Mashirika ya Kipapa kwa Mkoa wa Dar es Salaam ambaye
pia ni mwakilishi wa watoto na vijana wa Injili mtandaoni, Padre Thimotheo
Nyasulu alisema kuwa wameamua kutoa msaada huo baada ya kuona changamoto hiyo,
walipotembelea kituo hicho Desemba, 2016 kama sehemu ya matendo ya huruma kwa
kanisa.
No comments:
Post a Comment