Maofisa wa tume huru ya uchaguzi nchini Kenya, IEBC, wakiwa katika shughuli ya kuandikisha wapiga kura wapya, 16 Januari 2017.
|
Mahakama ya juu nchini Kenya imetoa uamuzi kuruhusu mawakili wanaomwakilisha kiongozi wa Upinzani Raila Odinga, kumulika mitambo za kompyuta zinazohifadhi hati za uchaguzi wa urais ambazo zimewekwa na tume ya uchaguzi.
Siku ya Jumatatu asubuhi Majaji saba wa mahakama ya juu nchini Kenya walianza kusikiliza kesi ambayo kiongozi wa upinzani Raila Odinga anapinga kuchaguliwa tena kwa rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi wa urais uliofanyika Agosti 8, 2017.
Kesi hiyo ilianza siku ya Jumamosi kwa maelezo ya mwanzo ambayo kila upande ulitoa ili kuhakikisha nafasi kwa kusikilizwa rasmi.
Katika kikao cha kwanza ambacho kilichukua muda wa masaa matano, na kumalizika saa tano usiku, mawakili wa pande zote walitoa maombi yao na matakwa yao ya kisheria.
Ombi kuu alilotoa James Orengo, mmoja wa mawakili wa Raila Odinga lilikuwa mahakama kumruhusu kumulikwa kwa mitambo ya kompyuta ambayo imehifadhi hati rasmi za uchgaguzi uliofanywa mapema mwezi huu.
Hata hivyo ombi la Orengo lilipingwa vikali na mawakili wanaomwakilisha rais Uhuru Kenyatta na pia tume inayosimamia uchaguzi Kenya.
Siku ya Jumapili kuamkia Jumatatu Mahakama ya Juu pia ilikubali kuingizwa kwa ushahidi kwenye kesi ya kupinga matokeo ya urais, hatua ambayo sasa imetenga uwanja wa makabiliano ya hoja kati ya mawakili wa rais Uhuru Kenyatta na wale wa kiongozi wa upinzani Raila Odinga.
Tofauti na ilivyokuwa mwaka 2013, majaji saba wa mahakama hiyo walitupilia mbali mapingamizi yaliyotolewa na mawakili wa pande zote mbili waliotaka kila mmoja ushahidi wake utupwe kwa sababu uliwasilishwa nje ya muda.@habari na rfi swahili
No comments:
Post a Comment