Thursday, 31 August 2017

MAKONDA AZUIA “UTITIRI” WA BOMOA BOMOA


MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema hakuna bomoabomoa itakayoendelea katika mkoa wake zaidi ya inayoendelea katika Barabara ya Morogoro na inayofanywa kwa ajili ya reli ya kisasa na kwamba, yeyote anayetaka kufanya ubomoaji lazima atoe taarifa kwa mujibu wa sheria.
Alisema hayo jana alipotembelea eneo la Masaki-Toangoma wilayani Temeke na eneo la Kigogo katika Manispaa ya Kinondon alipozungumza na wananchi wa maeneo hayo waliotarajiwa kukumbwa na bomoabomoa. Hivi karibuni, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) lilitangaza kubomoa nyumba zaidi ya 17,000 zilizojengwa katika hifadhi ya Bonde la Mto Msimbazi kuanzia Pugu hadi Daraja la Selander katika Manispaa ya Kinondoni.
Mbali na NEMC, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pia ilizipiga alama ya X nyumba zaidi ya 300 katika eneo la Masaki-Toangoma na kuitaka Manispaa ya Temeke kuanza kuzibomoa. Aidha, Makonda amewataka watu wote waliovamia maeneo ya masoko, shule, viwanja vya mpira na maeneo ya wazi wajisalimishe katika manispaa zao. Aliagiza viongozi wa serikali za mitaa na wananchi waliowadhulumu watu viwanja wakamatwe.
Akizungumzia bomoabomoa ya nyumba 17,000, Makonda alisema watu wanaotaka kufanya bomoabomoa hiyo hawakufuata utaratibu ikiwemo kuwasiliana na ofisi yake kuhusu utekelezaji wake. Makonda alisema mbali na viongozi hao hata Rais John Magufuli amesikitishwa na suala hilo na kumtaka kufuatilia ili kujua taratibu zilizotumika katika utekelezaji huo.
“Baada ya taarifa hizi kuandikwa katika vyombo vya habari rais alinipigia simu kama nina taarifa kuhusu ubomoaji huo nikamwambia sina taarifa na yeye akasema hajapata taarifa, alichokisema yeye hakuchaguliwa kwa ajili ya kubomoa nyumba za watu, bali kuleta maendeleo kwa wananchi,”alisema Makonda.
Akizungumzia suala la alama zilizowekwa na Wizara ya Ardhi Masaki, Makonda alisema baada ya kufuatilia alibaini kuwa viongozi wa serikali za mtaa walichangia kuuza viwanja hivyo ilhali wakijua kuwa maeneo hayo ni ya wazi na mengine ni ya bondeni yasiyopaswa kuwa makazi ya watu.

“Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa siyo muuzaji au mpimaji wa viwanja ukitaka kununua viwanja usiende huko wananchi wengi wamelizwa na watu hawa fuateni taratibu za ununuzi wa viwanja ili kupunguza migogoro hii ambayo imekuwa kero,” alisema. Makonda amewataka wananchi hao kujiepusha na ununuzi wa maeneo hatarishi, wafuate taratibu za ujenzi ili kujiepusha kujenga kiholela

No comments:

Featured post

MASIKINI WEEE!!!!! KICHANGA CHA SIKU MOJA CHAOKOTWA KATIKA KIWANJA CHA MPIRA AZIMIO

Na;Ezelina Yuda Mtoto mchanga mwenye jinsia ya Kike anayekadiriwa kuwa wa siku 1 ameokotwa akiwa hai kandokando ya uwanja wa azimio  ...