Rais john
Magufuli na mkurugenzi wa shirika la maendeleo la kimataifa (DFID)
nchini,Elizabeth Arthy ,wengine ni waziri wa mambo ya nje wa uingeleza
anayeshugulikia masuala ya afrika picha na ikulu.
|
UINGEREZA
imetoa msaada wa Dola za Marekani milioni 450 (sawa na takribani Sh trilioni
moja) kwa ajili ya kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.
Waziri wa Nchi
anayeshughulikia Maendeleo ya Kimataifa na Masuala ya Afrika katika Ofisi ya
Mambo ya Nje na Jumuiya ya Madola ya Uingereza, Rory Stewart aliyatangaza hayo
jana baada ya kukutana na Rais John Magufuli, Ikulu jijini Dar es Dar es
Salaam.
Kwa mujibu wa
taarifa ya Ikulu, Stewart alisema fedha hizo zitaelekezwa katika maeneo
mbalimbali ya maendeleo hususani katika kuinua ubora wa elimu na kuongeza idadi
ya watoto wanaopata elimu, kuimarisha miundombinu hasa barabara na bandari,
kuinua kilimo cha kibiashara na viwanda kama vile viwanda vya pamba na nyama.
Taarifa hiyo
ilieleza kuwa Stewart alimpongeza Dk Magufuli kwa kazi kubwa iliyofanywa na
serikali katika mapambano dhidi ya rushwa na hatua zilizochukuliwa, kuimarisha
elimu kwa kuwapa nafasi Watanzania wengi zaidi kupata elimu.
“Nimetembelea
shule moja hapa Dar es Salaam jana, na nimejionea jinsi sera ya kutoa elimu
bila malipo ilivyoleta mabadiliko makubwa katika kuongeza idadi ya wanafunzi,
nimezungukia shule, nimezungumza na wazazi na nimezungumza na walimu, idadi ya
wanafunzi imeongezeka karibu mara mbili, hili ni jambo kubwa sana kutokea kwa
muda mfupi na linaleta mabadiliko makubwa katika maisha ya watu, elimu ni kila
kitu,” alieleza Stewart.
Alibainisha
kuwa wananchi wa Uingereza wanaipenda Tanzania na serikali yao itaendelea
kushirikiana na Tanzania katika masuala mbalimbali ya uhusiano na ushirikiano.
Alisema kwamba ana matumaini kuwa msaada ilioutoa, utasaidia kuinua uchumi na
maisha ya Watanzania.
Kwa upande
wake, Dk Magufuli alimshukuru Stewart kwa kuja nchini na amemuomba ampelekee
shukrani zake kwa Malkia Elizabeth II na Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May
kwa msaada mkubwa uliotolewa kwa lengo na kuunga mkono juhudi za maendeleo
zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano.
Rais Magufuli
alisema Uingereza ndio nchi inayoongoza kwa uwekezaji nchini na alimhakikishia
Stewart kuwa Tanzania inatambua mchango mkubwa wa nchini hiyo katika maendeleo
ya Tanzania.
Aidha, Rais
Magufuli amewataka Watanzania waelewe kuwa hatua zinazochukuliwa na serikali
dhidi ya rushwa zina manufaa makubwa kwa nchi, na alisema serikali itahakikisha
fedha za msaada zilizotolewa na Uingereza zinasimamiwa vizuri.
“Na ndiyo
maana tuwaomba Watanzania waendelee kutuunga mkono katika mapambano dhidi ya
rushwa, rushwa ni ugonjwa mbaya sana, tukijisafisha katika rushwa nchi yetu
itakwenda mbele, katika juhudi tunazofanya wapo wengine wanalalamika lalamika
lakini matokeo yake ni makubwa na ndiyo maana ndugu zetu Waingereza wanaona.
“Pia nitoe
mwito kwa Watanzania kulipa kodi, hatuwezi siku zote tukawa tunategemea kodi za
kutoka kwa nchi marafiki kama Uingereza, ni lazima tujenge mazingira ya
Watanzania kuamini kuwa kulipa kodi ni kitu muhimu katika maendeleo yao,”
alisisitiza Rais Magufuli.
Mazungumzo
hayo yalihudhuriwa na Balozi wa Uingereza nchini, Sarah Cooke, Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Augustine Mahiga, Waziri wa Fedha
na Mipango, Dk Philip Mpango na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto
James.
Uingereza ni
moja ya nchi tano duniani zinazoongoza kwa uwekezaji nchini na katika biashara
na sekta binafsi. Nyingine ni pamoja na China, Afrika Kusini na India. Pia,
Uingereza ni moja ya wahisani wakubwa, wanaosaidia Mfuko Mkuu wa Bajeti wa
Tanzania kila mwaka.
Katika mwaka
wa fedha wa 2010/11, Uingereza ilitoa asilimia 29.4 ya bajeti na katika bajeti
ya 2015/16, Uingereza ilipanga kutoa msaada wa zaidi ya Sh bilioni 622. Kiasi
hicho kiliongezeka pia katika mwaka wa fedha 2016/17.
Mbali na Uingereza,
wahisani wengine wakubwa wanaochangia bajeti ya Tanzania ni Benki ya Maendeleo
ya Afrika (AfDB), Canada, Denmark, Umoja wa Ulaya (EU), Finland, Germany,
Ireland, Japan, Norway, Sweden na Benki ya Dunia.
Hali
kadhalika, kwa miaka mingi Serikali ya Uingereza imekuwa mstari wa mbele
kusaidia mapambano dhidi ya rushwa na imejitahidi kujengea uwezo Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB) na idara ya mahakama.
No comments:
Post a Comment