WABUNGE wa Bunge la Canada
wameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli kwa
jinsi anavyofanya kazi zake za kuwapambania Watanzania wa chini ili wawe juu
kwa kuwapatia maendeleo yaliyo na tija.
Wamesema Rais Magufuli ni miongoni
mwa marais wachache duniani, wenye kuthamini wananchi wake kwa kuwapambania
kupata mahitaji muhimu, ambayo nchi inastahili kupata kwa kubana mianya ya
wakwepaji wa kulipa kodi, ambayo ndio ingechangia kwa upatikanaji wa maendeleo
kwa kuwa Pato la Taifa limeongezeka kidogo.
Maneno hayo yamesemwa na Mwenyekiti
wa Kamati ya Bunge la Jumuiya ya Madola kutoka Canada, Yasmin Rentasi katika
kikao cha kamati hizo mbili za Canada na Tanzania kwenye Ukumbi Mdogo wa Bunge
jijini Dar es Salaam, huku Kamati ya Bunge la Tanzania ikiongozwa na Mwenyekiti
wake, Dk Raphael Chegeni.
Rentasi alisema Serikali ya Canada
ipo tayari kutoa misaada mbalimbali ya kibunge ili kuhakikisha Bunge la
Tanzania, linakuwa ni Bunge bora katika usimamizi mzuri wa kisheria na
kuishauri serikali juu ya masuala ya msingi yenye kuleta tija katika nchi hiyo.
“Tunaipongeza serikali ya Rais
Magufuli kwa juhudi zake za kupambana na kuinua uchumi wa nchi ya Tanzania kwa
kubana matumizi, kupambana na mafisadi, kudhibiti rushwa hivyo hali hii
inaonesha jinsi Tanzania itakavyofanikiwa kukuza uchumi wake kutoka chini na
kuongezeka, pia kutapelekea kupungua kwa kiwango cha umaskini pamoja na
kuboresha huduma za kijamii kwa muda mfupi,” alieleza Rentasi na kuongeza:
“Mimi nilizaliwa hapa Tanzania (Dar
es Salaam) wakati huo baba yangu alikuwa akifanya kazi hapa enzi za Mwalimu
Nyerere, niliondoka hapa nikiwa mdogo sana, lakini nafarijika leo kurudi hapa
na kuona Tanzania inasonga mbele.”
Aidha, aliwataka Watanzania
kumwombea Rais Magufuli ili apambane na mchwa ambao wana lengo la kutaka
kumkwamisha katika kutekeleza ahadi yake aliyoipanga kuwafanyia Watanzania.
Kwa upande wake, Dk Chegeni
aliwapongeza wabunge hao wa Canada, kwa kuona juhudi zinazofanywa na Rais
Magufuli kupambana na kuinua uchumi. Alisema Tanzania ni nchi yenye utulivu na
siasa safi hivyo aliwaomba wabunge hao kuwekeza zaidi ili wananchi wa Tanzania
wanufaike kupitia serikali yao ya Canada.
Alisema Tanzania na Canada
zitaendelea kushirikiana katika masuala mbalimbali ya maendeleo kwa ajili ya
kuwahakikishia wananchi wake upatikanaji wa huduma bora za kijamii.
No comments:
Post a Comment