UBINAFSISHAJI wa Kampuni ya
Maendeleo ya Viwanja vya Ndege (KADCO), umehojiwa kutokana na kile
kilichoelezwa kuwa umegubikwa na utata, hali ambayo baadhi ya wajumbe wa Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) wametaka wapewe maelezo ya serikali,
vinginevyo suala hilo litahamishiwa bungeni lijadiliwe.
Hayo yalibainika jana katika kikao
kati ya wajumbe wa PAC na Mamlaka ya Usimamizi wa Viwanja vya Ndege Tanzania
(TAA). Miongoni mwa mambo ambayo wajumbe walisema yana utata, ni pamoja na CAG
kubaini kuwa licha ya serikali kuwa na hisa asilimia 100 katika Kadco, kampuni
hiyo imeendelea kuachiwa kuendesha Kiwanja cha ndege cha Kilimanjaro (KIA).
Utata mwingine ni hatua ya KIA
kuendeshwa tofauti na viwanja vingine, kwa maana ya kuwa chini ya kampuni hiyo
wakati viwanja vya ndege vingine vyote viko chini ya TAA. "Kwa nini hiki
kiendeshwe tofauti na viwanja vingine?
Na TAA wanaendesha viwanja vingine
na siyo KIA... Tutamuita waziri atueleze kuna nini," alisema mwenyekiti wa
kamati, Naghenjwa Kaboyoka ambaye ni Mbunge wa Same Mashariki (Chadema).
Kwa upande wake, Mbunge wa Sikonge,
Joseph Kakunda (CCM) alisema: "Tuwe wazi kuwa huko serikalini kuna watu
wanaendesha Kadco wanamaintain status quo kwa sababu wanapata fedha.
Kama Baraza la Mawaziri halitakuwa
wazi katika hili, tutawasha moto bungeni.” “Kwa nini hawa TAA wawe na
share(hisa) na Kadco wakati hawana mamlaka?” alisema mbunge huyo akirejea
maelezo ya Mkurugenzi wa TAA katika kikao hicho aliyesema kuwa suala la Kadco
haliwahusu ingawa wana hisa.
Awali, Mwenyekitiwa Bodi ya TAA,
Profesa Ninatubu Lema alipoulizwa na wajumbe wa kamati kuhusu masuala kadhaa ya
Kadco, alisema kampuni hiyo iko nje ya mamlaka ya TAA kwa kuwa inaripoti moja
kwa moja kwa serikali.
Miongoni mwa maswali kuhusu Kadco
yaliyoulizwa na Kakunda na kufanya wajumbe wengi kuchangia, ni uhusiano wa TAA
na kampuni hiyo kama kama wana mkataba wowote. Pia alitaka kufahamu kama
kampuni hiyo, imerithiwa na serikali au imeanzishwa upya.
No comments:
Post a Comment