Rais wa Tanzania Dk. John Magufuli |
RAIS John
Magufuli amesema anataka wala rushwa wengi, wafungwe na ameiagiza Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kufanya kazi bila kumwogopa mtu ili
siku moja kuwe na Tanzania isiyo na rushwa na maendeleo yafi ke kwa wananchi wa
kawaida.
Amesema
mkazo zaidi kwa Takukuru unapaswa kuwekwa kwenye eneo la uchunguzi na
uendeshaji wa mashauri ya rushwa na ingawa kauli yake inaweza kutowafurahisha
wengi, lakini anataka wala rushwa wafungwe. Rais Magufuli alisema hayo jana
Ikulu, Dar es Salaam katika hafla ya kumwapisha Naibu Mkurugenzi Mkuu wa
Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo.
“Kasimamie
jukumu kwa uadilifu mkubwa, hasa katika suala la uchunguzi na uendeshaji,
nataka wala rushwa wengi wafungwe, hilo mimi nalitaka, najua maneno kama haya
hawayataki wengi kuyasikia, nataka wala rushwa wengi wafungwe, wakifungwa hawa
hapatakuwa na rushwa. “Hawa wamekuwa ni walimu wa wala rushwa na msimwogope mtu
yeyote, anayehusika na rushwa ni adui wangu na wa Watanzania wote.
Tunataka
manufaa yanayopotea kwenye rushwa yaende kwa wananchi wa kawaida,” alisema Dk
Magufuli na kuongeza kuwa anatamani ifike mahali Tanzania iwe watu wanaishi
bila rushwa. “Watu wanakosa dawa, wanakosa barabara, wanakosa vitu muhimu
sababu ya rushwa, hii ni dhambi kubwa, nafikiri ni dhambi kubwa, dini yoyote,
mtu yeyote mwenye kupenda watu wake hawezi kutetea suala la rushwa,”
alisisitiza Rais Magufuli.
Rais
alihimiza ushirikiano wa Takukuru, serikali kwa ujumla wake na wananchi kila
mmoja katika eneo lake kupambana na rushwa kwa nguvu zake zote. “Tukifanikiwa
kupunguza rushwa kwa angalau asilimia 80, nchi yetu itafanikiwa kutatua
matatizo mengi, na ni vema mtambue kuwa hatua hizi tunazochukua zimeanza
kuwavutia wafadhili wengi na wawekezaji.
Na mimi
nikiwa kiongozi wenu nimeamua kupambana na rushwa kikwelikweli, na ninawaomba
nyote mshirikiane kuondoa rushwa katika maeneo yenu ya kazi,” alifafanua.
Aidha, Rais Magufuli aliwataka viongozi wote nchini kushirikiana katika jukumu
la mapambano dhidi ya rushwa ili kuepusha madhara ya tatizo hilo katika uchumi
na ustawi wa jamii.
“Ukiangalia
mambo makubwa tunayopambana nayo yanasababishwa na rushwa iliyosambaa kila
mahali, watumishi hewa chanzo ni rushwa, dawa za kulevya ndani yake kuna
rushwa, vyeti feki ndani kuna rushwa, mikataba mibovu ndani kuna rushwa,
pembejeo za ruzuku ndani kuna rushwa na huko mahakamani nako ni rushwa tu,”
alisisitiza.
Aidha,
pamoja na hali ya kukithiri kwa rushwa, Dk Magufuli aliipongeza Takukuru kwa
kazi iliyoanza kuifanya, lakini ametaka juhudi zaidi ziongezwe ili watu wote
wanaojihusisha na vitendo vya kutoa na kupokea rushwa washughulikiwe kwa mujibu
wa sheria.
Mara kwa
mara katika hotuba zake, Rais Magufuli amekuwa akieleza dhamira ya serikali
kupambana na rushwa katika kila eneo ili kuhakikisha huduma za jamii na maendeleo
yanapatikana. Katika eneo la watumishi hewa pekee, Mei mwaka jana, Rais
Magufuli alinukuliwa akisema kuwa serikali imebaini watumishi hewa zaidi ya
10,295 na wanalipwa Sh bilioni 11.63 kwa mwezi na kama wangeendelea kulipwa kwa
miaka mitano, hasara ingekuwa Sh bilioni 696.1.
Awali,
Brigedia Jenerali Mbungo alimshukuru kwa kuteuliwa kushika nafasi hiyo na
aliahidi kufanya kazi kwa ushirikiano na viongozi wengine wa taasisi hiyo
katika mapambano dhidi ya rushwa. Kamishna wa Maadili wa Sekretarieti ya
Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji mstaafu Harold Nsekela, aliwataka viongozi
wote wa umma, kuhakikisha wanajaza fomu za tamko la mali kwa wakati na pia
aliwataka kutoa ushirikiano kwa sekretarieti hiyo, inapochukua hatua ya kufanya
uhakiki wa taarifa zilizojazwa katika fomu hizo.
Kwa
upande wake, Waziri Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Angella Kairuki pamoja na kumshukuru Rais kwa uteuzi, alisema
katika mapambano dhidi ya rushwa, hakuna jiwe linalojihusisha na rushwa
litakalosalia. Kairuki alisema kuna weledi na utayari wa kufanya kazi katika
mapambano hayo na kuwataka wananchi wazalendo, kutoa taarifa za wala rushwa kwa
namba 113 (ujumbe mfupi au kupiga) ili hatua zichukuliwe.
Kuhusu utumishi wa umma, Waziri
Kairuki alimweleza Rais kuwa wataendelea kusimamia weledi na utashi kwa kufuata
taratibu, sheria na kanuni katika utumishi wa umma ili kuleta tija na maslahi
kwa wafanyakazi yaboreke. Naye Mkurugenzi wa Utawala wa Takukuru, Alex Mfungo,
pamoja na kumshukuru Rais Magufuli kwa uteuzi wa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa
Takukuru, alimhakikishia kuwa wataendelea kufanya kazi kwa bidii. Pamoja na
kula kiapo cha kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali Mbungo
pia amekula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma kilichoongozwa na Kamishna
wa Maadili, Jaji mstaafu Nsekela.
No comments:
Post a Comment