Wednesday, 18 October 2017

Mahindi ya Zambia yafurika Rukwa, bei yaporomoka.

Mahindi




MAHINDI yanaendelea kuwadodea wakulima mkoani Rukwa baada ya wafanyabiashara na watu binafsi kuchangamkia mahindi kutoka nchini jirani ya Zambia yanayoingizwa mkoani humo kimagendo, yakiuzwa kwa bei ya kutupwa na kusifiwa kwa ubora na usafi wake.
Mahindi hayo ambayo inadaiwa yanaingizwa kwa wingi mkoani Rukwa kwa kupitia njia za panya wilayani Kalambo, yanauzwa kwa bei ya kutupwa ya Sh 20,000 kwa gunia lenye uzito wa kilo 100 na debe moja likiuzwa kwa Sh 3,000 huku yakisifiwa kuwa yanakidhi vigezo vya ubora na usafi kuliko yanayozalishwa mkoani humo.
Takwimu za hivi karibuni za hali ya uzalishaji zinaonesha kuwa Mkoa wa Rukwa umezalisha ziada ya ya tani 727,496.6 za chakula huku mahindi pekee yake yakiwa ni tani 453,049.2, huku Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Kanda ya Sumbawanga wakipangiwa kununua tani 3,000 tu za mahindi katika msimu wa ununuzi wa mahindi ulioanza Agosti 7, mwaka huu na kumalizika Septemba 4, mwaka huu.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili hivi karibuni, umebaini kuwa shehena hiyo ya mahindi inavushwa kupitia njia za panya kutoka nchi jirani ya Zambia, ambako wafanyabiashara wanatumia kila aina ya usafiri wakiwemo punda, pikipiki na baiskeli kuyavusha na kuingia nayo wilayani Kalambo.
Uchunguzi umebaini kuwa wafanyabiashara wadogo wa mahindi kutoka Zambia na wengine kutoka nchini, wakifanikiwa kuyaingiza mahindi hayo mkoani Rukwa kupitia njia za panya wilayani Kalambo, wanachanganyika na wakazi wa humo ili wasibainike kuwa wametokea Zambia.
Kutokana na kufurika kwa mahindi hayo kutoka Zambia, yamesababisha mahindi yaliyovunwa msimu huu kuendelea kulundikana na kuwadodea wakulima, ambao kwa sasa hawawezi tena kuuza ngunia moja lenye uzito wa kilo 100 kwa Sh 35,000 kwa kuwa ya Zambia yanauzwa kwa bei ya kutupwa ya chini ya Sh 20,000.
Hivi karibuni, Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Uyole mkoani Mbeya, Tulole Bucheyeki alikanusha taarifa zilizozagaa kuwa mahindi yanazaliwa mkoani Rukwa, yamekosa soko kutokana na kutokuwa na ubora stahiki kwa kuwa wakulima wanatumia mbegu bora za mahindi zilizofanyiwa utafiti na kituo hicho.
Aliwataka wakulima mkoani humo kuupuuza uzushi huo, isipokuwa wazingatie namna bora za uhifadhi ya mahindi wanapoyavuna kwa kuwa yana ubora sawa na yanayozalishwa katika nchi jirani.
Baadhi ya wafanyabiashara wadogo wa mahindi kwa nyakati tofauti, walilieleza gazeti hili kuwa mahindi ya Zambia yanayoingizwa nchini kimagendo yanachangamkiwa sana na walaji na wafanyabiashara kwa kuwa wanadai ni matamu na yamehifadhiwa katika hali ya usafi pia yanauzwa kwa bei ya kutupwa.
“Wafanyabiashara wa mahindi wamewageuzia kibao wakulima wa mkoa huu wanadai kuwa hawahifadhi mahindi katika hali ya ubora unaotakiwa kwamba yanakuwa na uchafu sasa wafanyabiashara wanaona shida kununua gunia la mahindi kwa bei ya shilingi 35,000 yakiwa machafu halafu waanze kupepeta.
“Wakati kuna mahindi kutoka nchi jirani ya Zambia licha ya kuuzwa kwa bei ya Sh 20,000 kwa gunia lenye uzito wa kilo 100 lakini pia yamehifadhiwa vizuri na ni masafi sana,” alisema John Mwanakulya ambaye ni mkazi wa mkoani Rukwa.
Kwa upande wao ‘walanguzi ‘ kutoka Zambia, kwa masharti ya kutoandikwa majina yao gazetini wakihofia kukamatwa, walidai kuwa wakulima wa Rukwa kwa sasa hawawezi kuuza mahindi yao Zambia hata kama watafanikiwa kuyapitisha kwa magendo kwa kuwa wakulima wa nchi hiyo wamevuna ziada kubwa ya mahindi msimu huu wa mavuno.
“Nchini kwetu (Zambia ) tunapata shida, soko la uhakika kwa mahindi tuliyovuna halipo ...sasa tumelazimika kwa namna yoyote ile kuyavusha na kuyauza huku kwa bei hii ndogo ili tuweze kukidhi mahitaji yetu muhimu nyumbani hatuuzi ili kupata faida “ alisema mmoja wa ‘walanguzi.’
Hata hivyo, hawakuwa tayari kueleza jinsi wanavyofaulu kuvuka mpaka na kuingia mkoani Rukwa wakiwa na shehena ya mahindi. Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kaskazini, Ally Kessy (CCM) na Mbunge wa Jimbo la Kwela wilayani Sumbawanga, Ignas Malocha (CCM) walieleza kuwa wamejipanga kuonana na Waziri wa Kilimo ili wamfikishie kilio cha wakulima wa mahindi wa mkoa huo.
Mkazi wa Sumbawanga, Zeno Nkoswe alidai kuwa mahindi yamelundikana kwenye nyumba za wakulima, kiasi kwamba wanalazimika kulala juu ya magunia hayo badala ya vitandani, huku akiitaka serikali iingilie kati kwa kuwa msimu wa kilimo umeanza, hivyo itasababisha wakulima wasilime mahindi kwa kuwa bado wana ziada ya kutosha.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo, Simon Ngagani aliitaka serikali kuona uwezekano wa kuipatia uwezo wa kifedha Wakala wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) Kanda ya Sumbawanga ili wanunue ziada ya mahindi yaliyolundikana kwa wakulima mkoani humo, kisha iyauzie kwa Mpango wa Chakula Duniani (WFP).
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Apolinary Macheta aliitaka serikali mkoani Rukwa, ialike wilaya na mikoa yenye uhaba wa chakula nchini, waje kununua mahindi kutoka kwa wakulima kwa bei ya ushindani.
“Wafanyabiashara wanaomiliki viwanda vinavyosindika nafaka yakiwemo mahindi waalikwe kuja mkoani hapa kununua ziada hiyo ya mahindi tena wakulima wapatie bure maghala ya serikali ili wahifadhi mahindi yao ili wafanyabiashara hawa waweze kuyanunua kwa urahisi na kwa haraka tena kwa bei ya ushindani hata ya Sh 500/- kwa kilo moja,” alieleza Macheta.
Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Dk Halfan Haule alisisitiza kuwa serikali haijakataza kuuza mahindi nje, ispokuwa inasisitiza kuuza unga ambao umeongezwa thamani.
@habari na habari leo.

No comments:

Featured post

MASIKINI WEEE!!!!! KICHANGA CHA SIKU MOJA CHAOKOTWA KATIKA KIWANJA CHA MPIRA AZIMIO

Na;Ezelina Yuda Mtoto mchanga mwenye jinsia ya Kike anayekadiriwa kuwa wa siku 1 ameokotwa akiwa hai kandokando ya uwanja wa azimio  ...