MAWAZIRI na manaibu waziri walioapishwa jana Ikulu, jijini Dar es Salaam, wameapa kufanya kazi kwa kasi inayoendana na utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli inayokwenda sambamba na kauli ya `Hapa Kazi Tu’.
Miongoni mwa mawaziri hao ni Angellah Kairuki aliyeweka rekodi ya kuwa mwanamke wa kwanza kuiongoza wizara ya madini nchini. Ameteuliwa kuiongoza wizara hiyo iliyotenganishwa na Wizara ya Nishati inayojitegemea huku ikitarajiwa ataimudu kutokana na rekodi yake ya uchapakazi akiwa waziri katika Ofisi ya Rais akishughulikia Menejimeti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Pamoja na Waziri huyo, mawaziri wengine wapya walioapishwa Dar es Salaam jana na Rais John Magufuli, wamebainisha wazi hatua watakazochukua katika utendaji kazi wao ili kuhakikisha Tanzania inakua imara kiuchumi na watanzania wanapata maendeleo. MWENYEWE AZUNGUMZA Akizungumza na gazeti hili mara baada ya kuapishwa rasmi kuwa Waziri wa wizara hiyo, Kairuki alimshukuru Dk Magufuli kwa kuendelea kumuamini na hata kumpata wizara ya madini, huku akibainisha wazi kuwa yupo tayari kukabiliana na changamoto za wizara hiyo na kwamba, atahakikisha Watanzania na taifa kwa ujumla wananufaika na rasilimali hiyo ya madini.
“Nashukuru sana nimeingia kwenye wizara hii ya madini tayari kuna sheria imepitishwa juzi ya kulinda rasilimali, ipo sheria ya madini na sera ya madini. Hizi ndiyo nyenzo nitakazotumia kikamilifu katika kufanya kazi zangu na kwa kushirikiana na wenzangu,” alisema. Aidha, alisema kwa kuwa changamoto nyingi zinazoikabili wizara hiyo zinagusa zaidi eneo la mikataba, atahakikisha anajenga uwezo wa majadiliano ili kuweza kuwa na uwanja mpana wa uelewa katika kuingia mikataba hiyo na kuepusha mgogoro wa kimaslahi na kiuchumi.
Kairuki pia alieleza kuwa madini ndiyo injini ya uchumi wa Tanzania, hivyo ataangalia namna ya kuiboresha sekta hiyo ya madini ili iweze kuchangia katika kukuza uchumi wa Tanzania. Akiwa Utumishi, Kairuki ameacha historia katika wizara hiyo kutokana na utendaji wake kwa kufanikiwa kudhibiti watumishi hewa na kuondoa watumishi wenye vyeti feki. “Sijawahi kufanya kazi kwenye madini, ngoja niende nichape kazi,” alisema Kairuki ambaye kwa sasa jicho linamtizama kutokana na historia ya mawaziri wanaoteuliwa kuongoza wizara hiyo.
Mawaziri wengi waliowahi kuongoza wizara hiyo, wameishia kuondolewa kabla ya kumaliza muda wao kutokana na changamoto mbalimbali, ikiwemo kuingia mikataba mibovu na kuruhusu kupotea kwa rasilimali ya madini bila kunufaisha nchi. Katika serikali ya awamu ya tano pekee iliyoingia madarakani mwaka 2015, tayari mawaziri wawili wameachia ngazi kutokana na kashfa mbalimbali zinazohusu mikataba ya madini akiwemo Profesa Sospeter Muhongo na George Simbachawene.
MALIASILI NA UTALII Naye Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla alisema amejipanga kutekeleza mambo matatu katika wizara hiyo ambayo ni kudhibiti ujangili, kutangaza vivutio na kuvutia zaidi watalii nchini na kutafuta suluhu la migogoro ya wakulima na hifadhi ukiwemo mgogoro wa Loliondo. “Ki ukweli najisikia uzito wa majukumu niliyopewa na mheshimiwa Rais.
Wizara hii ni nzito na nyeti sana. Kwa sasa inachangia pato la taifa kwa asilimia 17.2, lakini pia asilimia 25 ya fedha zinazoingia nchini za nje zinatokana na wizara hii. Nawahakikishia pamoja na yote hayo sitowaangusha Watanzania,” alisema Dk Kigwangalla. Alisema kwa kushirikiana na wafanyakazi wa wizara hiyo, ataanza na kudhibiti wale wote wanaoshirikiana na majangili hao, lakini wapo ndani ya mfumo wa serikali.
“Hawa ndiyo tutakaoanza nao, wale waliopo ndani ya `mfumo’ na kushiriki kwenye biashara hii muda wao sasa umefika,” Kuhusu kutangaza vivutio vya utalii, alisema kwa sasa bado vivutio vingi na vya kipekee vilivyopo nchini havijatangazwa vya kutosha kuweza kuvutia watalii na kueleza kuwa atatumia mbinu mbalimbali kuweza kutangaza vivutio hivyo ili kuzifikia nchi za magharibi kama vile China na Marekani. Pamoja na hayo, waziri huyo kijana ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, alisema moja ya mikakati yake atakayoanza kuishughulikia ni pamoja na kuumaliza kabisa mgogoro wa Loliondo.
‘WEZI WA MUDA’ Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika, aliwatangazia kiama watumishi wote wazembe kuwa kuanzia sasa, kila mtumishi atapaswa awajibike ipasavyo kwa kuzingatia taratibu na muda wa kazi.
“Nimegundua kuwa kuna watumishi wanalipwa fedha nyingi lakini wanafanya kazi kwa muda mchache kutokana na visingizio mbalimbali. Sasa nitahakikisha kila ofisi ya umma inakuwa na kantini ya chakula ili kudhibiti muda wa kazi,” alisema Mkuchika. Aidha, alisema atahakikisha anapambana na rushwa katika utumishi wa umma na kuwajengea uelewa wananchi kuwa wanastahili kupata huduma bila kutoa rushwa.
“Tena hili nitazungumza na wenzangu tuone namna ya kuanzisha somo la rushwa shuleni,” MPINA AJISHAURI Hali kadhalika, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, alisema alipoteuliwa kushika wadhifa huo wa uwaziri, ilibidi atumie takribani saa 16 kufikiria kutokana na ukweli kuwa wizara hiyo imejaa changamoto mbalimbali ikiwemo migogoro ya wakulima na wafugaji na matatizo ya uvuvi haramu.
Hata hivyo, alisema amejipanga kukabiliana na changamoto hizo ikiwemo kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu. “Nawaahidi sitachoka kufanya kazi na kupambana na changamoto hizi,” AFYA YA WANAWAKE Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema anashukuru kuendelea kuongoza wizara hiyo ya afya ambapo kwa sasa kampeni yake ni kuhamasisha wanawake kupima afya zao ili kukabiliana na saratani ya kizazi ambayo inazidi kuwa tishio.
“Pale Ocean Road saratani ya kizazi ndiyo inayoongoza kwa asilimia 30 na kufuatiwa na saratani ya matiti kwa asilimia 12. Mbaya zaidi kati ya wagonjwa 100 wanaokuja kupima asilimia 80 wanakuwa wako tayari katika hali mbaya. Naombeni wanawake wenzangu tupime afya zetu ugonjwa huu ukiwahwa unatibika,” alisisitiza.
MCHAKAMCHAKA Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, alisema atawasimamia wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi kuhakikisha wanasimamia vyema maendeleo katika maeneo yao. “Nawaomba wakurugenzi wahakikishe kila mkandarasi aliyepo chini yao anatimiza mradi wake kwa ufasaha kama ni barabara au ujenzi wa madarasa, kwa hili nitakuwa mkali,” alisema.
SIJAFUNGWA MDOMO Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Kangi Lugola alisema atasimamia ipasavyo suala zima la utunzaji wa mazingira hususani kuwadhibiti wenye viwanda na migodi inayomwaga kemikali zinazoathiri afya za wananchi na kuharibu mazingira. “Kuteuliwa kwangu kuwa waziri sijafungwa mdomo kama watu wanavyodhani, sasa nakwenda kuwashughulikia waharibifu wote wa mazingira, wajiandae.
Nitataka tufanye kazi kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo si vinginevyo,” alisema. Mara baada ya kuwaapisha mawaziri na manaibu hao mawaziri, Spika wa Bunge Job Ndugai aliwataka mawaziri hao kuwajibika ipasavyo kwa kuwa serikali hiyo ya awamu ya tano sera yake ni hapa kazi tu.
JAJI MKUU ANENA Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Tanzania Ibrahim Juma aliwahimiza viongozi hao kuhakikisha wanafuata Katiba, sheria na kanuni zilizopo ili kuepuka kuibua migongano isiyo na lazima. Dk Magufuli alifanya mabadiliko katika Baraza lake la Mawaziri kwa kuwahamisha baadhi yao kwenda wizara nyingine, kuwapandisha baadhi ya manaibu waziri kuwa mawaziri kamili, kuwaingiza wapya na kuwaacha baadhi yao nje ya Baraza hilo.
@habari na habari leo
No comments:
Post a Comment