Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza. |
Maonesho hayo yaliyofanyika katika viwanja vya Tempete vilivyopo jijini Bujumbura, yalianza Septemba 28, mwaka huu na yalitarajiwa kukamilika jana, yameandaliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa lengo la kuongeza fursa za kibiashara katika nchi za ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.
“Hii ni ishara ya kukomaa kwa udugu kati ya Tanzania na Burundi, wananchi wa Burundi walikuwa wakisafiri umbali mrefu kufuata bidhaa hadi Dar es Salaam, lakini sasa wameletewa mlangoni.
Kwa muda mrefu tumekuwa tukifurahia bidhaa aina hii, lakini bei zilikuwa kubwa kutokana na gharama za usafiri, kwa sasa mambo yamekuwa mazuri,” alisema Rais Nkurunziza. Rais Nkurunziza aliongeza kuwa: “Uhusiano wetu unazidi kuimarika, naamini ile dhana ya utangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki inatekelezwa kivitendo. Naahidi kuunga mkono juhudi zote za kuimarika kiuchumi kati ya nchi mbili hizi.”
Ubalozi wa Tanzania nchini Burundi kwa kiasi kikubwa umeshiriki kufanikisha maonesho haya chini ya Balozi Rajabu Gamaha ambaye ndiye aliyewashawishi maofisa wa TanTrade kuwa na maonesho aina hiyo kutokana na maombi ya kupata bidhaa kutoka Tanzania kuwa mengi ofisini kwake. Awali katika hotuba yake ya ufunguzi Septemba 27, mwaka huu, Makamu wa Pili wa Rais wa Burundi, Dk Joseph Bitore alisema biashara ni kitu kinachounganisha mataifa mawili kiuchumi hivyo watachukulia maonesho hayo kujifunza, lakini pia kutanua wigo wa mahusiano ya kiuchumi kati ya Tanzania na Burundi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TanTrade, Christopher Chiza alisema uamuzi wa kupeleka bidhaa Burundi ulipofika mezani kwake hakutaka kusita kwa sababu alijua hiyo ni njia pekee ya kufikisha mbali bidhaa za Kitanzania. “Tunapofanikiwa kufika Burundi maana yake tunalenga soko pana la ukanda huu, tunatarajia kufikia soko la Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa sababu hata wao tumearifiwa kuwa wananunua bidhaa kutoka Burundi,” alisema Chiza.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Edwin Rutageruka aliahidi kuendeleza biashara kati ya Tanzania na Burundi hata baada ya kumalizika kwa maonesho hayo. “Huu ni mwanzo, tayari wafanyabiashara tulioongozana nao wamechukua mawasiliano ya wateja wao na watawauliza wanahitaji nini ili walete.”
@habari na habari leo
@habari na habari leo
No comments:
Post a Comment