Wednesday, 4 October 2017

Samia ataka watumishi Olduvai kujifunza kutoka Dubai.



MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan amemuagiza Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe kuwapeleka maofisa wa Makumbusho mpya ya Olduvai Gorge jijini Dubai kwa ajili ya mafunzo zaidi ya kiteknolojia.

Samia alitoa maagizo hayo wakati akizindua rasmi majengo ya Makumbusho mpya ya Olduvai Gorge ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, mradi uliojengwa kwa gharama ya Sh bilioni 1.7 huku asilimia 80 ya gharama hizo zikiwa ni ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU) na kiasi kilichobaki ni fedha kutoka Serikali ya Tanzania.
“Tuna Makumbusho kubwa zaidi barani Afrika yenye kuweza kutoa historia ya Zamadamu, yaani binadamu wa kale, maisha na zana zake; lakini hii itakuwa bora zaidi ikiwa tutaifanya iwe kiteknolojia zaidi,” alisema Makamu wa Rais, na kuongeza kuwa Waziri Maghembe kupitia uhusiano mzuri alionao na nchi za Saudi Arabia, atafanikisha suala la kuwapeleka wataalamu kwenda kupata mafunzo zaidi Dubai.
Makamu wa Rais pia ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kujenga makumbusho kwenye maeneo mengine ya kihistoria kama Kilwa (Lindi), Amboni (Tanga), Bagamoyo (Pwani) na Zanzibar maana kwa sasa mwelekeo wa watu wengi duniani ni kurudi nyuma wajionee jinsi dunia ilivyokuwa zamani.
Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Maghembe alisema Makumbusho ya Olduvai Gorge ni ya pekee duniani ambapo karibu kila zana za kale, mabaki ya zamadamu na alama halisi zilizoachwa na binadamu zaidi ya miaka milioni 4 iliyopita, vinapatikana; “Hakuna kama hii ulimwenguni kote.”
Naye Mbunge wa Ngorongoro ambaye pia ni Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Ole Nasha ameuomba uongozi wa Wilaya ya Ngorongoro pamoja na Mamlaka ya Hifadhi kuangalia matumizi bora ya ardhi katika eneo hilo ambalo lina mchanganyiko wa hifadhi ya wanyamapori, wafugaji wa jamii ya Kimasai na eneo la historia ya mambo ya kale.
“Na katika kila faida inayoongezeka kupitia Utalii, tungependa kuwa wakazi wa eneo hili pia wawe wananufaika zaidi,” alisema Ole Nasha. Meneja wa Urithi wa Utamaduni katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Joshua Mwankunda alisema Makumbusho ya Oldupai ni moja kati ya mipango mingine mikubwa inayotarajiwa katika eneo hilo, ukiwemo ule wa Makumbusho katika eneo jirani la Laetoli ambako nyayo za binadamu wa kale aliyeishi eneo hilo miaka milioni 4 iliyopita zinapatikana.
@habari na habari leo

No comments:

Featured post

MASIKINI WEEE!!!!! KICHANGA CHA SIKU MOJA CHAOKOTWA KATIKA KIWANJA CHA MPIRA AZIMIO

Na;Ezelina Yuda Mtoto mchanga mwenye jinsia ya Kike anayekadiriwa kuwa wa siku 1 ameokotwa akiwa hai kandokando ya uwanja wa azimio  ...