Saturday, 14 October 2017

UNESCO kuchagua kiongozi mpya

Irina Bokova UNESCO Generaldirektorin (picture-alliance/ dpa)

Kiongozi anayeondoka wa UNESCO Irina Bokova

Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu elimu sayansi na utamaduni UNESCO, litamchagua kiongozi mpya Ijumaa atakayetoa mwongozo bora katika shirika hilo baada ya kujiondoa kwa Marekani na Israel.

Wagombea wa Ufaransa na Qatar ndio watakaoshiriki raundi ya mwisho ya uchaguzi baada ya mgombea wa Misri kushindwa.
Mgombea wa Ufaransa Audrey Azoulay alipata kura 31 katika kura ya mchujo iliyofanywa na bodi ya utendaji ya shirika hilo la Umoja wa Mataifa naye Moushira Khattab wa Misri akapata kura 25. Azoulay sasa atakuwa anashindana na Hamad bin Abdulaziz Al-Kawari wa Qatar.
Audrey na Hamad walikuwa mawaziri wa zamani wa utamaduni na wanakumbana sasa baada ya siku tano za kura iliyopigwa kwa njia ya siri katika makao makuu ya UNESCO huko Paris. Iwapo wawili hao watapata kura sawa basi bodi hiyo itaamua ni nani atakayeliongoza shirika hilo kwa kipindi cha miaka minne ijayo.
China itaendelea kuwa mwanchama wa UNESCO
Lakini mchakato huo wa kura ulitiliwa doa na uamuzi wa Marekani kujiondoa katika shirika hilo la Umoja wa Mataifa. Lakini China kupitia msemaji wa wizara yake ya nchi za nje, Hua Chunying, ilitangaza Ijumaa itaendelea kuwa mwanchama wa shirika hilo na kuzitaka nchi zengine kutoa uungaji mkono pia.
UNESCO Wahl Kandidat Hamad bin Abdel Aziz al-Kawari, Katar (Getty Images/AFP/K. Sahib)
Mgombea wa Qatar Hamad bin Abdulaziz al-Kawari
"Lengo la UNESCO ni kuendeleza ushirikiano wa kimataifa katika nyanja za elimu, sayansi na utamaduni, pamoja na kuongeza uelewano na muungano wa jamii tofauti, kuilinda amani ya dunia kwa ajili ya kuwepo maendeleo," alisema Chunying. "China inataraji nchi zote zinaweza kushiriki katika suala hili. China itaendelea kushiriki katika kazi za UNESCO na tuko tayari kufanya kazi pamoja na nchi zengine katika suala hili," aliongeza msemaji huyo.
Marekani hutoa mchango mkubwa kwa shirika hilo la Umoja wa Mataifa, lakini ilikuwa imesitisha mchango huo tangu mwaka 2011 pale shirika hilo lilipokiri kwamba Palestina ni mwanachama wake kamili. Marekani ilijiondoa Alhamis kwa kulishutumu shirika hilo kwa kile ilichodai ni maonevu dhidi ya Israel. Israel yenyewe ilijiondoa muda mfupi baada ya Marekani kufanya hivyo.
Kura iligubikwa na wingu la mgogoro baina ya Qatar na Misri
Huku Misri na Qatar wote wakiwa wanaiwania kazi hiyo awali, kura hiyo pia ilitatizwa na ule mzozo uliopo baina ya Qatar na majirani zake wa Kiarabu ambao wamekatisha uhusiano wa kidiplomasia na Qatar, kwa kuishutumu kuwa inaunga mkono ugaidi, jambo ambalo Qatar inalikataa.
UNESCO Wahl Kandidat Audrey Azoulay, französische Ex-Ministerin (picture alliance/dpa/ZUMAPRESS/AFBV)
Mgombea wa Ufaransa Audrey Azoulay
Huyo mgombea wa kiti hicho cha uongozi wa UNESCO kutoka Qatar Hamad bin Abdulaziz, amekuwa akirushiwa cheche za matusi katika mtandao na maafisa wa Misri kuanzia wiki iliyopita, ingawa ana imani kwamba atashinda na anasema kuwa anataka kuwaleta pamoja nchi wanachama.
Misri hapo awali ilikuwa inataka uchunguzi ufanywe kutokana na madai ya makosa katika hilo zoezi zima la upigaji kura. Ombi hilo la Misri liliwasilishwa na Waziri wa Mambo ya nje wa nchi hiyo Sameh Shoukry mbele ya Mkuu wa sasa wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa Irina Bokova.
@habari na Dw swahili.

No comments:

Featured post

MASIKINI WEEE!!!!! KICHANGA CHA SIKU MOJA CHAOKOTWA KATIKA KIWANJA CHA MPIRA AZIMIO

Na;Ezelina Yuda Mtoto mchanga mwenye jinsia ya Kike anayekadiriwa kuwa wa siku 1 ameokotwa akiwa hai kandokando ya uwanja wa azimio  ...