Thursday, 2 November 2017

Ummy atoa hofu homa ya kirusi ya marburg.


WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amewatoa hofu Watanzania kwamba hadi sasa hakuna mgonjwa yeyote nchini, ambaye amegundulika au kuripotiwa kuwa na ugonjwa wa marburg uliojitokeza katika nchi jirani ya Uganda tangu Oktoba 17, mwaka huu.
Akizungumza na wandishi wa habari kuhusu ugonjwa huo jana jijini Dar es Salaam, Ummy alisema kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), ugonjwa huo ni mkali na hatari kama ulivyo ebola, lakini umedhibitiwa.
 “Ugonjwa huu ni mkali sana na hatari kama wa Ebola lakini umedhibitiwa na WHO wameahidi kuendelea kutupatia taarifa kadri inavyowezekana... Nawatoa hofu Watanzania kwamba hakuna mgonjwa yeyote ambaye amegundulika na ugonjwa huo hadi sasa,” alisema Ummy.
Aidha, alisema katika kuchukua tahadhari “tumeimarisha vituo vyetu vya kuchunguza wananchi wote ambao wanaingia mipakani hasa katika mikoa ambayo inapakana na Uganda ikiwemo Mara, Kagera na Mwanza.”
 “Ugonjwa huu ni miongoni mwa magonjwa yajulikanayo kwa ujumla kama Homa za Virusi zinazosababisha kutokwa damu mwilini. Ugonjwa huu hauna tiba wala chanjo,” alisema.
Dalili kuu za ugonjwa huo ambazo huanza ghafla ni pamoja na Homa kali, maumivu makali ya kichwa pamoja na mwili kuishiwa nguvu ambapo baadaye huambatana na kuharisha sana (majimaji), maumivu ya tumbo, kichefuchefu na kutapika.
 Alisema dalili zingine za ugonjwa huo ni kutokwa damu katika matundu yote ya mwili yaani pua, njia ya haja kubwa na ndogo, mdomoni, masikioni, machoni, hali inayosababisha kifo kwa muda mfupi.
Kipindi cha kuonekana kwa dalili za ugonjwa ni kati ya siku tatu hadi tisa baada ya kupata maambukizi. 
Ugonjwa huu unaenea kwa urahisi sana na haraka kutoka mtu mmoja hadi mwingine iwapo mtu atakuwa karibu na mgonjwa na kugusana na mate, damu, mkojo, machozi, kamasi, maji maji mengine ya mwili, ikiwa ni pamoja na jasho au kumgusa mtu aliyekufa kwa ugonjwa wa marburg. 
Ugonjwa huu pia unaweza kuenezwa iwapo mtu atagusa nguo au mashuka ya mgonjwa wa Marburg. TFDA yadhibiti dawa duni yaingiza Maabara hamishika.

No comments:

Featured post

MASIKINI WEEE!!!!! KICHANGA CHA SIKU MOJA CHAOKOTWA KATIKA KIWANJA CHA MPIRA AZIMIO

Na;Ezelina Yuda Mtoto mchanga mwenye jinsia ya Kike anayekadiriwa kuwa wa siku 1 ameokotwa akiwa hai kandokando ya uwanja wa azimio  ...