Friday, 2 February 2018

Tanzia: Mwanasiasa mkongwe Kingunge afariki dunia.

Mwanasiasa mkongwe Mzee Kingunge Ngombale Mwiru

RAIS Dkt. John Magufuli amepokea kwa huzuni na masikitiko taarifa za kifo cha mmoja wa waasisi wa Taifa na mwanasiasa mkongwe nchini Mzee Kingunge Ngombale Mwiru kilichotokea katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, jijini Dar es Salaam mapema leo Ijumaa, taarifa ya Ikulu yaeleza.
Mzee Kingunge Ngombale Mwiru alikuwa akipatiwa matibabu hospitalini hapo baada ya kushambuliwa na mbwa wake nyumbani kwake Jijini Dar es Salaam Desemba 22, 2017. Taarifa iliyosambazwa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais imemnukuu Dkt. Magufuli akisema staifa limempoteza mtu muhimu ambaye alitoa mchango mkubwa katika juhudi za kupigania uhuru na baada ya kupata uhuru akiwa mtumishi mtiifu wa Chama cha TANU na baadaye Chama Cha Mapinduzi (CCM), na katika nyadhifa mbalimbali za uongozi ndani ya Serikali.
“Mzee Kingunge Ngombale Mwiru ametoa mchango mkubwa sana, sisi kama Taifa hatuwezi kusahau na tutayaenzi mema yote aliyoyafanya wakati wa utumishi wake uliotukuka, ametuachia somo la kupigania maslahi ya nchi wakati wote, kuwa wazalendo wa kweli, kudumisha amani na mshikamano, kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa na kuwa na nidhamu” amesema Mhe. Magufuli.
Hata hivyo, Rais Magufuli amewapa pole wanafamilia wote, wanachama wa CCM, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na msiba huu, na amewaombea kuwa na moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki cha majonzi.
Chanzo:Habari leo
#Changia Damu Okoa Taifa

No comments:

Featured post

MASIKINI WEEE!!!!! KICHANGA CHA SIKU MOJA CHAOKOTWA KATIKA KIWANJA CHA MPIRA AZIMIO

Na;Ezelina Yuda Mtoto mchanga mwenye jinsia ya Kike anayekadiriwa kuwa wa siku 1 ameokotwa akiwa hai kandokando ya uwanja wa azimio  ...