Wednesday, 2 August 2017

Bodaboda zatumika kutorosha mahindi mpakani.

Rombo.
Wimbi la usafirishaji mahindi kwa njia za magendo kwenda nchini Kenya limerejea tena mkoani Kilimanjaro, lakini safari hii mahindi hayo yakivushwa mpakani kwa kutumia usafiri wa pikipiki.

Vyanzo mbalimbali vimedokeza kuwa wafanyabiashara wasio waaminifu wamebuni njia hiyo mpya ya usafirishaji, baada ya Serikali kupiga marufuku usafirishaji nje ya nchi wa aina yoyote wa chakula.

 Maeneo ambayo yanatajwa kutumiwa na wafanyabiashara hao wa magendo ni Kikelelwa, Rongai, Motamburu karibu na kituo cha afya na Kijiweni eneo la Lower Road katika mji wa Tarakea. Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, pikipiki moja hubeba kati ya gunia moja na mbili za mahindi na inakadiriwa kati ya pikipiki 50 hadi 100 huvuka mpaka kila siku kupitia njia za panya katika maeneo hayo. “Sisi wenyewe kama raia tunashangaa maana sio jambo la siri.

 Huu ni mradi wa baadhi ya polisi wako kwenye payroll (malipo) na wengi wana pikipiki na ndio huzisindikiza,” kilidokeza chanzo hicho. Awali, utoroshaji huo wa mahindi ulikuwa ukifanywa kwa kutumia malori aina ya Mitsubish Fusso ambayo hubeba magunia kati ya 150 na 300, kabla ya kudhibitiwa na Serikali Juni 30 mwaka huu. Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah, amesema taarifa hizo ni za mtaani, lakini akasema anachojua eneo la Tarakea kuna tatizo la uongozi wa polisi.

 “Ninachojua pale Tarakea hakuna OCS (mkuu wa polisi wa kituo) na ndio tunafanya taratibu za kupeleka OCS mpya. Kama wananchi wana taarifa za hizo pikipiki watuletee tuchukue hatua,” amesema. Juni 26 mwaka huu, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alitoa maagizo mazito ya kutaifishwa kwa malori na vyombo vya moto vitakavyokamatwa vikitorosha mahindi kwenda nje ya nchi.

 “Naomba mnisikilize vizuri. Ni marufuku kwa yeyote kusafirisha chakula kwenda nje ya nchi bila vibali na vibali ni vya kusaga na kusafirisha unga na sio mahindi,”alisisitiza Waziri Mkuu na kuongeza: “Mahindi hayo tutayataifisha tutayapeleka kwenye ghala la taifa na hilo gari lake tutalitaifisha litaishia jeshi la polisi.

Tunafanya haya kwa lengo la kuwalinda watanzania tusikumbwe na njaa.” Waziri mkuu alisema ingawa eneo la Tarakea wilayani Rombo ambako kuna mamia ya malori ya mahindi kuna soko, lakini kata hiyo yenye wakazi 4,000 haiwezi kuhitaji lori 100 zilizojaa mahindi.

 “Tunazo taarifa baadhi ya polisi wanashiriki kupitisha malori hayo. RPC (Kamanda Issah) ukigundua kuna afisa wa polisi anashiriki kuondoa mahindi nje, chukua hicho cheo chake,” alisema. Kauli ya Waziri mkuu ilitokana na hatua ya uongozi wa Serikali ukiongozwa na mkuu wa mkoa Kilimanjaro, Anna Mghwira, kukamata zaidi ya malori 100 yakitorosha mahindi kwenda Kenya.

No comments:

Featured post

MASIKINI WEEE!!!!! KICHANGA CHA SIKU MOJA CHAOKOTWA KATIKA KIWANJA CHA MPIRA AZIMIO

Na;Ezelina Yuda Mtoto mchanga mwenye jinsia ya Kike anayekadiriwa kuwa wa siku 1 ameokotwa akiwa hai kandokando ya uwanja wa azimio  ...