Habari kutoka Tarime.
Baraza la Madiwani la
Halmashauri ya mji wa Tarime mkoani Mara leo Alhamisi, Agosti 17 limewakuta na
hatia na kuwachukulia hatua za kisheria watumishi wanne kwa kutumia vibaya
madaraka yao na kuisababishia halmashauri hiyo hasara ya mamilioni ya fedha.
Akitoa taarifa ya
hatua iliyochukuliwa na kamati ya maadili ya utumishi, mwenyekiti wa
halmashauri hiyo, Hamis Nyanswi amewataja waliochukuliwa hatua hizo kuwa ni
Simion Nyadwera aliyekuwa katibu wa idara ya afya ambaye alihamishiwa katika
Halmashauri ya Maswa anadaiwa kuchota Sh24 milioni na ametakiwa kurejesha kiasi
hicho cha fedha huku Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru)
ikitakiwa kumchunguza utumishi wake.
Nyanswi amemtaja
mtuhumiwa mwingine kuwa ni Laurenti Marwa aliyekuwa afisa utumishi Mwandamizi
wa Halmashauri ya Mji wa Tarime aliyedaiwa kushirikiana na watumishi 60
kuzisababishia hasara taasisi za fedha na kuiingiza halmashauri hiyo kwenye
mgogoro mkubwa.
Amesema kuwa Marwa
atapunguziwa mshahara wake kutoka ngazi ya mshahara ya TGTS F yenye kiwango cha
mshahara wa Sh1.3 milioni kwenda TGTS E, yenye kiwango cha mshahara wa
Sh950,000.
"Pamoja na
adhabu hiyo Marwa atatakiwa kuzilipa cha Sh26 milioni alizosababishia hasara
taasisi hizo," amesema Nyanswi.
Watumishi wengine ni
Sabure Masanja na Quinter Wayoga waliopewa onyo kutokana na makosa yao.
"Walikuwa
akichelewa na pia kuwahi kuondoka kazini na kusababisha usumbufu mkubwa kwa
wananchi kukosa huduma yake," amesema mwenyekiti huyo.
Watumishi hawa
hawakuwa tayari kuzungumzia uamuzi uliochukuliwa na baraza la madiwani licha ya
kupigiwa simu na kuita bila kupokelewa.
Mbunge wa Tarime
Mjini, Esther Matiko amewataka watumishi wa umma kuzingatia maadili ya kazi zao
ili kuwafanya wananchi kupata huduma wanayostahiki badala ya kukutwa na usumbufu
usio kuwa wa lazima.
"Watumishi wa
umma wasimamie vizuri nafasi zao ili kuepukana na matatizo yanayowafanya kuanza
kufuatiliwa na waajiri wao, nasi kama baraza la madiwani hatutasita
kuwachukulia hatua za kinidhamu pale majina yao yanapofikishwa kwetu,"
amesema Matiko.
No comments:
Post a Comment