Tuesday, 1 August 2017

Tume ya uchaguzi Kenya yapokea karatasi za kura ya uraisi


Maafisa wa Tume ya uchaguzi Kenya wanatarajiwa kupokea shehena ya mwisho ya karatasi za kupigia kura ya urais tayari kwa uchaguzi mkuu Jumanne wiki ijayo.

Karatasi hizo zinazotarajiwa kuwasilishwa katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta leo jioni, zitakuwa kwenye vifurushi 161 na ni za kaunti kuanzia nambari 31 hadi nambari 47.
Tume hiyo ilikuwa imepokea vifurushi 192 vya karatasi za kupigia kura za majimbo hayo mengine 30.

IEBC inatarajiwa kupokea jumla ya karatasi 20,818,000, ambapo kuna karatasi za ziada takriban milioni moja.
Tume hiyo imesema imeongeza jumla ya kura asilimia moja kila kituo kufidia karatasi za kura ambazo huenda zikaharibika wakati wa upigaji kura.
Baadhi ya wagombea walikuwa wamelalamikia idadi hiyo ya kura za ziada wakisema huenda ikatumiwa kuiba kura.

Lakini mmoja wa makamishna wa IEBC Dr Roselyn Kwamboka ameambia runinga ya kibinafsi ya Citizen kwamba sheria za uchaguzi zinamruhusu mpiga kura anayeharibu karatasi ya kura kabla ya kutumbukiza karatasi yake kwenye debe kupewa karatasi nyingine.

"Akiharibu mara nyingine, anaweza kupewa tena karatasi nyingine.
 Hii ina maana kwamba kuna baadhi ya wapiga kura wanaoweza kutumia karatasi tatu za kura," amenukuliwa na runinga hiyo.


Kwa kura karatasi za kura zimefungwa kwa mafungu ya karatasi 50 kila kifungu, katika kila kituo wanalazimika kuchukua karatasi za kura zinazokaribia 50.
Kwa mfano, kituo chenye wapiga kura 322, ukiongeza kwa hamsini ya karibu utapata 350.

Kulizuka utata kuhusu zabuni ya uchapishaji wa karatasi za kura ya urais lakini Mahakama ya Rufaa iliamua kampuni ya Al-Ghurair ya Dubai ichapishe karatasi hizo.
Wapiga kura 19,611,423 wamejiandikisha kushiriki uchaguzi mkuu Jumanne wiki ijayo.

No comments:

Featured post

MASIKINI WEEE!!!!! KICHANGA CHA SIKU MOJA CHAOKOTWA KATIKA KIWANJA CHA MPIRA AZIMIO

Na;Ezelina Yuda Mtoto mchanga mwenye jinsia ya Kike anayekadiriwa kuwa wa siku 1 ameokotwa akiwa hai kandokando ya uwanja wa azimio  ...