Sunday, 3 September 2017

Mabula:Toeni hati kuepusha migogoro

Naibu Waziri wa ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi Angela Mabula akikagua eneo la Igomelo wilayani Kahama ambalo lilikuwa na mgogoro kati ya wananchi na serikali 

 Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angelina Mabula amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri sita za Mkoa wa Shinyanga, kuhakikisha wananchi wanapimiwa viwanja na kukabidhiwa hati ili kuepusha migogoro na usumbufu.
Dk Mabula alisema hayo juzi wakati wa ziara yake ya kukagua mwenendo wa idara ya ardhi mkoani hapa.
Alisema watumishi wanakaa ofisini wakati kazi hazifanyiki kwa viwango jambo ambalo halikubaliki.
Mabula aliwataka wasikae ofisini wakasubiri wizara, wahakikishe maeneo yote yanapimwa na hati zinatolewa kwa wakati.
Alisema hati zinatakiwa kutolewa ndani ya miezi mitatu, zaidi ya hapo ni kumsumbua mwananchi.
“Hakikisheni maeneo yanapimwa na hati zinatolewa kwa wakati bila kusababisha usumbufu kwao, inawezekana mwananchi akawa hana fedha ya kulipia yote kwa wakati, msiikatae fedha yake ichukueni, atakuwa analipa kidogokidogo,” alisema Mabula.
Pia, alirudia kauli ambayo imekuwa ikitolewa na viongozi wenye dhamana ya kusimamia wizara ya ardhi kwamba hakuna kuchukua maeneo ya watu kama hakuna fedha ya kufidia kwa wakati.
Alisema kama kuna eneo halmashauri inalihitaji na kuona linafaa kwa matumizi yake, bora wakafanye mazungumzo na mwenye eneo wakubaliane: “Halmashauri inaweza ikachukua nusu na yeye akachukua nusu ila siyo kumyang’anya mtu eneo lake halali,” alisema.
Awali, akitoa taarifa kwa waziri huyo, Kaimu Ofisa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Shinyanga, Hamis Nkelege alisema idadi ya viwanja vilivyopimwa Januari hadi Juni mwaka huu ni 40,044 na kutolewa hati miliki 1,506.
Alisema kwa kipindi kama hicho, zimetolewa hatimiliki za kimila 137 ikilinganishwa na hati 699 zilizotolewa Januari hadi Desemba 2016.
Kamishna wa Ardhi Kanda ya Ziwa, Idrisa Juma aliwataka watumishi wawe waaminifu wanapowapimia viwanja wananchi na wasigawe kiwanja kimoja kwa watu wawili jambo linaloibua migogoro.
Baadhi ya wananchi, Herman Maige na Ester Piter kwa nyakati tofauti walisema migogoro mingi inasababishwa na watumishi wenyewe wanapopima viwanja mara mbili.  
#habari toka mwananchi 

No comments:

Featured post

MASIKINI WEEE!!!!! KICHANGA CHA SIKU MOJA CHAOKOTWA KATIKA KIWANJA CHA MPIRA AZIMIO

Na;Ezelina Yuda Mtoto mchanga mwenye jinsia ya Kike anayekadiriwa kuwa wa siku 1 ameokotwa akiwa hai kandokando ya uwanja wa azimio  ...