Wakati
hali ya mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu ikiwa bado
haijatengemaa, yameibuka maswali kadhaa kuhusu shambulio dhidi yake lililotokea
Alhamisi iliyopita mjini Dodoma.
Watu
wasiojulikana walimshambulia rais huyo wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika
(TLS) kwa risasi zipatazo 32 akiwa ndani ya gari lake baada ya kuwasili katika
makazi yake eneo la Area D, na ni risasi tano zilizompata na kumjeruhi vibaya.
Lissu, ambaye
ameibukia kuwa mwanasiasa aasiyeogopa kusema analoamini, amelazwa Hospitali ya
Aga Khan jijini Nairobi ambako amewekwa chumba cha wagonjwa wanaohitaji
uangalizi wa karibu.
Taarifa
zilizopatikana jana zinasema mbunge huyo, bado anaangaliwa kwa karibu na
madaktari.
Habari za
shambulio dhidi yake zilitapakaa kwa kasi Ijumaa mchana, na juzi watu walikuwa
wakitoa salamu za pole na kumuombea arudi katika hali yake, lakini jana
kukaibuka maswali.
Gazeti
hili limeyachambua maswali machache kati ya mengi ambayo yamejitokeza katika
mijadala mbalimbali.
Miongoni
mwa maswali hayo ni kwa nini Jeshi la Polisi halikuchukua hatua baada ya Lissu
kutangaza kuwa kuna watu wanamfuatilia kwa muda mrefu.
Agosti 18,
Lissu aliwaambia waandishi wa habari kuwa anafuatiliwa na watu anaowashuku kuwa
ni maofisa usalama kwa takriban wiki tatu mfululizo.
Lissu
alikwenda mbali zaidi kwa kumtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro
pamoja na mkurugenzi wa idara ya usalama wa Taifa (TISS) kuwaeleza wakubwa wao
kuhusu watu hao kwamba wapambane na wahalifu badala ya kutumia rasilimali za
nchi kufuatilia raia wasio na hatia.
Hata
hivyo, juzi IGP Sirro aliwaambia waandishi wa habari mjini Dopdoma kuwa Lissu,
ambaye amekuwa akikamatwa mara kwa mara na polisi kutokana na kauli anazotoa katika
mikutano na waandishi wa habari, hakutoa taarifa hizo katika kituo chochote cha
polisi.
“Hili ni
swali ambalo lingefaa zaidi aulizwe yeye. Hivyo tunaomba apone halafu mumuulize
kama alitoa taarifa kituo chochote cha polisi,” alisema Sirro.
Swali hapo
ni, kama iliwezekana kumkamata kutokana na anachokisema kwenye vyombo vya
habari, ilishindikana vipi kufuatilia madai anayoyatoa katika mikutano hiyo?
Hata
hivyo, mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Patrobas Katambi
amesema jana kuwa walishamuandikia IGP Sirro kuhusu tishio dhidi ya Lissu na
hajawajibu.
Jibu hilo
la IGP Sirro limeibua swali jingine; kwa nini Lissu hakutoa taarifa hizo
polisi?
Swali
jingine ni kitendo cha polisi kutochukua hatua za haraka kuhoji wahusika wa
karibu na tukio. Jana, polisi ilitangaza kuwa inamsaka dereva wa Lissu ambaye
tangu wakati wa tukio alikuwa akionekana na viongozi wa Chadema na alikuwepo
Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.
Ilikuwaje,
polisi walishindwa kumchukulia kama ni mtu muhimu kumuhoji mara baada ya tukio
badala ya kusubiri hadi siku tatu baadaye?
Swali
jingine ni mazingira ya tukio hilo. Dereva wa Lissu alieleza kwamba kuna gari
jeupe lilikuwa linawafuatilia kutoka bungeni mpaka nyumbani kwa Lissu, eneo
ambalo wanakaa wabunge na mawaziri.
Kwa
maelezo yake ni kwamba yeye ndiye aliyemzuia Lissu asishuke ndani ya gari na
kumtaka alaze kiti wakati risasi zikipigwa kwenye gari lao.
Watu hao
walikuwa wakimfuata kila siku hadi nyumbani? Na kama siku hiyo pekee walimfuata
hadi anaanza kuelekea nyumbani, dereva hakuona hali ni tofauti na kuamua
kupeleka gari sehemu salama au kutumia mbinu ambayo ingemthibitishia kuwepo kwa
nia ovu?
Kingine
kinachozua utata ni kufuatiliwa kwa gari la Lissu tangu bungeni. Hii ina maana
kuwa watu hao wenye nia mbaya walikuwepo kwa muda mrefu kwenye viunga au eneo
la jirani na Bunge wakimsubiri waliyemtaka.
Je, askari
wanaolinda hapo na madereva wengine wa wabunge hawakuliona na kulitilia shaka
gari hilo kwa siku zote kama Spika Job Ndugai alivyolieleza Bunge kuwa maeneo
ya chombo hicho yako salama?
Swali
jingine ni kuhusu hali ya usalama katika eneo la makazi ya wabunge na mawaziri.
Je, viongozi hao wako salama? Kama washambuliaji walimudu kufyatua risasi
takriban 32 na kufanikiwa kuondoka, bado wabunge na mawaziri wako salama?
Eneo
wanalokaa vigogo hao lina ulinzi na wafanyakazi wa ndani. Wote hao hawakuona
tukio hilo.
Kama kuna
ulinzi au walinzi, walifanya juhudi gani kusaidia kudhibiti washambuliaji au
kutoa taarifa ambazo zingewezesha polisi kuwabana mapema?
Hata
hivyo, Jeshi la Polisi jana lilisema linawahoji baadhi ya majirani kuhusu tukio
hilo.
Spika
Ndugai alisema watu hao walifyatua risasi kati ya 28 na 32, kwa nini walitumia
idadi hiyo kubwa kumshambulia mtu asiye na silaha?
Mwenyekiti
wa Chadema, Freeman Mbowe alisema shambulio hilo ni la kisiasa kwa kuwa Lissu
hana adui nje ya siasa.
Hao maadui
ndani ya siasa ni nani? Ni wanasiasa wa chama kingine au walio ndani ya
Chadema? Ni maadui katika ngazi gani ya kisiasa ambayo inaweza kufikia kiwango
cha kutaka kumuua mpinzani?
Katika
hatua nyingine, taarifa zilizopatikana jana jioni kabla ya kwenda mitamboni
zilisema Lissu alikuwa bado kwenye chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa
karibu wa madaktari katika hospitali ya Aga Khan jijini Nairobi.
Hakuna
kiongozi wa Chadema wala ndugu aliyekuwa tayari au kupatikana kuzungumzia
maendeleo ya hali yake.
Lissu,
mwanasheria wa kujitegemea na mwanaharakati wa haki za binadamu na mazingira,
amejipatia umaarufu zaidi katika miaka ya karibuni, hasa kutokana na misimamo
yake mikali na matukio ya kukamatwa kila mara na polisi na wakati mwingine
kufunguiliwa mashtaka, hasa ya uchochezi.
No comments:
Post a Comment