MAZUNGUMZO yanaendelea ili kuuza mahindi kwenye Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) na Sudan Kusini.
Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William ole Nasha alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy (CCM) aliyetaka kujua kwa nini serikali inazuia wakulima kuuza mazao yao nje ya nchi. Keissy alisema kama itaendelea hivyo, basi pia iwabane wafanyakazi wasitumie hovyo mishahara yao. Nasha alisema lengo la serikali kuzuia kuuza mazao nje ya nchi ni kuhakikisha nchi inakuwa na usalama wa chakula nchi nzima.
Kutokana na uwepo wa chakula za ziada, aliwataka wafanyabiashara watumie fursa hiyo ya kununua mazao maeneo hayo na kusambaza katika mikoa yenye chakula kidogo kama Simiyu, Mwanza na Shinyanga.
Akijibu swali la msingi la Mbunge wa Mbeya Vijijini, Oran Njeza (CCM), aliyetaka kujua Benki ya Wakulima Tanzania itaanza lini kutoa mikopo kwa wakulima wadogo wa Mbeya Vijijini, Nasha alisema hadi kufikia Juni mwaka huu, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imefikisha mtaji wake kupanda hadi Sh bilioni 65.6 kutoka Sh bilioni 65.3 za robo ya kwanza ya mwaka huu.
Alisema kutokana na udhamini wa serikali, benki hiyo imepata mkopo wa bei nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) wa Sh bilioni 209.5. Aidha, hadi kufikia Juni mwaka huu, TABD imetoa mikopo ya Sh bilioni 7.46 katika mikoa ya Tanga, Morogoro na Iringa, ambapo wakulima 2,252 wamenufaika na mikopo hiyo.
Nasha alisema TADB, inalenga kufungua ofisi za Kanda nchi nzima ili kurahisisha na kupunguza gharama za upatikanaji wa mikopo. Benki hiyo itaanzisha ofisi ya Kanda mkoani Mbeya, lakini na wakulima walio katika vikundi watanufaika na mikopo ya benki hiyo kuanzia msimu ujao wa kilimo.
No comments:
Post a Comment