Monday, 11 September 2017

Wadau watoa Sh228 bilioni kwa Wizara ya Afya.


Balozi wa Denmark nchini, Einar Jensen akikabidhi fedha za mfuko wa maendeleo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Mpoki Ulisubisya. Picha na Herieth Makwetta. 
Wadau wa maendeleo wametoa mabilioni ya fedha kusaidia miradi ya sekta ya afya.
Wadau wa maendeleo wamekabidhi Sh227.76 bilioni kwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa ajili ya miradi ya sekta ya afya.
Fedha hizo za mfuko wa pamoja zimekabidhiwa leo Jumatatu na Balozi wa Denmark nchini, Einar Jensen kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Mpoki Ulisubisya.
Akizungumza baada ya makabidhiano  yaliyofanyika Hazina, Dk Ulisubisya amesema mfuko huo ulioanzishwa mwaka 1999 unalenga kuongeza nguvu za Serikali katika kupeleka mahitaji ya afya kwa wananchi.
Amesema fedha hizo hupokewa na Wizara ya Fedha na kupelekwa Wizara ya Afya na ya Tamisemi.
Dk Ulisubisya amesema asilimia 80 ya fedha hupelekwa moja kwa moja kwenye maeneo yanayotoa huduma za afya kwa wananchi katika halmashauri na vituo vya kutolea huduma.
Amesema asilimia 20 inayobaki ni kwa ajili ya shughuli za utawala na ufuatiliaji wa makubaliano ya madhumuni ya fedha hizo.
“Mwaka huu tumekubaliana fedha zinakwenda kuangalia huduma za afya kwa ajili ya mama na mtoto, uzazi pingamizi na huduma za chanjo kwa sababu ni afua muhimu kuzuia maradhi, pia kupunguza vifo vya akina mama,” amesema.


Balozi wa Denmark nchini, Jensen amesema wataendelea kuiunga mkono Serikali kwa fedha za wadau wa maendeleo.
@habari na mwananchi

No comments:

Featured post

MASIKINI WEEE!!!!! KICHANGA CHA SIKU MOJA CHAOKOTWA KATIKA KIWANJA CHA MPIRA AZIMIO

Na;Ezelina Yuda Mtoto mchanga mwenye jinsia ya Kike anayekadiriwa kuwa wa siku 1 ameokotwa akiwa hai kandokando ya uwanja wa azimio  ...